Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-06 18:53:59    
Barua 1104

cri

Michezo ya 29 ya Olimpiki ya majira ya joto itafunguliwa mwezi Agosti mwaka 2008. Ili kuwawezesha wasikilizaji wetu waelewe vizuri zaidi na kushiriki kwenye Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008 na kuenzi moyo wa Michezo ya Olimpiki, kuanzia tarehe 1 Novemba mwaka 2007 hadi tarehe 25 Aprili mwaka 2008, idhaa mbalimbali za Radio China Kimataifa zinatangaza makala 4 za Mashindano ya chemsha bongo yasemayo: Tukutane Beijing mwaka 2008 kwenye Michezo ya Olimpiki, makala hizo zinahusu "Maendeleo ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing", "Kauli mbiu ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing na wanasesere wa alama ya Baraka ya michezo hiyo", Viwanja na majumba ya michezo ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing" na "Miji mingine itakayoshirikiana na Beijing kuandaa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008".

Kama ilivyokuwa kwenye mashindano ya miaka iliyopita, kila baada ya kusoma makala moja, tutauliza maswali mawili. Baadaye kamati yetu ya uthibitishaji itachagua wasikilizaji washindi wa nafasi ya kwanza, pili na tatu pamoja na nafasi maalum.

Kila mshiriki wa mashindano hayo ya chemsha bongo atapata kadi moja ya kumbukumbu; washindi watakaopata nafasi za kwanza, pili na tatu watapewa kadi ya kumbukumbu na zawadi; na wasikilizaji washindi watakaopata nafasi maalum wataalikwa kuja China ambapo watapewa tuzo ya kikombe na kadi, watatembelea mji wa Beijing kwa siku 10, watatembelea viwanja na majumba ya Michezo ya Olimpiki na kukutana na wachezaji maarufu wa China.

Kuanzia tarehe 11 Novemba, kwenye Kipindi cha Sanduku la Barua, Idhaa ya Kiswahili itatangaza rasmi makala nne za mashindano ya chemsha bongo zisemazo: Tukutane Beijing mwaka 2008 kwenye Michezo ya Olimpiki. Na matangazo ya makala hizo nne yatarudiwa kuanzia tarehe 9 Desemba mwaka huu, msikose kutusikiliza.

Sasa tunawaletea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Bw. Edward Kavai Abuogi wa sanduku la Posta 838 Kitale, nchini Kenya anaanza barua yake kwa kutaka tupokee salamu zake na kutupongeza tunavyoandaa kipindi hiki cha sanduku la barua. Anaomba kama tunavyouliza maswali katika ile sehemu ya chemsha bongo, tumtumie nakala au kijikaratasi cha maelezo mbali na maswali.

Anasema kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi hapati nafasi ya kusikiliza Radio, ila tu kwa siku za Jumapili anapokuwa na mapumziko. Pia anaomba tumtumie vitabu au kitabu kinachoeleza kuhusu nchi ya China, kanda na picha nzuri ya sehemu maalumu inayopendeza nchini China.

Msikilizaji wetu mwingine ni Bw. Mwidadi Hassan wa sanduku la Posta 271 Kilifi, nchini Kenya anaanza barua yake kwa kutoa pongezi nyingi kwa yote tuliyomfanyia tangu ajiunge na Radio China Kimataifa. Anasema mashabiki wengi wa Radio China Kimataifa ni wenye matatizo ya kiuchumi. Vituo vingi vya Radio nchini Kenya vimeanzisha zawadi za kutoa zawadi ili kuwavutia wasikilizaji wengi. Hivyo anapendekeza kuwe na mshindi wa wiki na apewe zawadi, ili wasikilizaji waweze kutuma kadi nyingi. Vile vile kama kuna fomu maalumu za mikopo kwa malipo ya pole pole ili kuwasaidia mashabiki wa Radio China kimataifa wenye matatizo ya kiuchumi, anaomba ziweze kutumwa kwa wasikilizaji.

Mwisho anamaliza barua yake kwa kutaka kujua atawezaje kutuma barua pepe akiwa huko kijijini ambako hakuna umeme wala kompyuta, lakini pia na namba yetu ya simu haifahamu?

Tunawashukuru Bw. Edward Kavai Abuogi na Bw. Mwidadi Hassan kwa barua zao zinazotueleza kuhusu usikilizaji wao wa vipindi vyetu kama kipindi hiki cha sanduku la barua. Tunapenda mjue kuwa nia yetu ni kuandaa vipindi vya kuwafurahisha zaidi wasikilizaji wetu, wasikilizaji wetu wakifurahia vipindi vyetu, kweli tunatiwa moyo na tutachapa kazi zaidi. Kuhusu suala la Bw. Mwidadi Hassan namna ya kutuma barua pepe akiwa huko kijijini, ambako hakuna umeme wala kompyuta, na hata namba yetu ya simu hajui, tunaona hivi sasa tunaweza kuvumilia tu, lakini mwanga upo.Hivi karibuni Mkutano wa mawasiliano ya habari kuhusu "kuunganisha Afrika" umefungwa huko Kigali hivi karibuni, washirika wa Mkutano huo wameahidi kulisaidia bara la Afrika kuendeleza mawasiliano ya habari na mtandao wa internet, wamesema watatimiza ahadi, sisi tusubiri utekelezaji wa mpango, bila shaka baada ya hapo mambo yatakuwa mazuri.

Msikilizaji wetu wa sasa ni Luciana Omari Akanga wa sanduku la Posta 330, Luanda, nchini Kenya. Yeye anapenda kutoa shukurani zake za dhati kwa wafanyakazi wa Radio China Kimataifa kwa kazi tunayofanya. Anasema akiwa shabiki wa Radio China kimataifa anafurahishwa sana na jinsi tunavyofanya bidii ili kuwaelimisha, kuwafahamisha na kuwaburudisha. Kwa hakika anasema ameweza kujua mambo kadha wa kadha kuhusu nchi ya China kutokana na matangazo yetu.

Anaamini kuwa ataendelea kuyafahamu mengi zaidi anapozidi kusikiliza matangazo ya Radio China Kimataifa. Pia anashukuru sana kwa zawadi tunazoendelea kumtumia. Hadi sasa anasema amepokea picha za wadudu, ndege, wanyama na ukuta mkuu, bila kusahau bahasha zilizolipiwa gharama za stempu, kadi za salamu na kalenda maridadi ya mwaka 2007.

Anamaliza barua yake kwa kusema hakika hayo yote yamempa moyo wa kuendelea kusikiliza Radio China Kimataifa, na anasema mungu aibariki Radio China Kimataifa, na anatuombea wafanyakazi wote afya njema ili tuendelee kuwafahamisha na kuwaunganisha zaidi.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Luciana Omari Akanga kwa barua yake ya kututia moyo, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza matangazo yetu na kutoa maoni na mapendekezo kuhusu vipindi vyetu ili tuandae vizuri matangazo yetu.

Msikilizaji wetu Bw. Francis Nyankaira wa sanduku la Posta 71 Kemogemba, Mara, Tanzania ametuandikia barua yake akianza na salamu kwa wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa, na anasema lengo la barua yake ni kutaka kutusalimia na kutushukuru kwa kusoma barua yake ya maoni aliyoiambatanisha na majibu ya chemsha bongo.

Pia anasema anapenda kumshukuru sana Bw. Ras Manko Ngogo kwa kumwueleza mambo mengi kuhusu China na idhaa ya Kiswahili, kwani baada ya Bw. Ngogo kushinda chemsha bongo mwaka jana, alipata fursa ya kuitembelea China, hivyo amemueleza jinsi studio ya Radio China Kimataifa ilivyo, magari yanavyokimbia, mnara mrefu wa matangazo na michezo mingi ya sarakasi.

Kutokana na maelezo hayo kutoka kwa Bw Ngogo, anasema bila shaka na yeye anatamani kuitembelea China hata sasa au miaka ijayo kama mungu ataendelea kumlinda.

Mwisho anasema anapenda sana sauti za watangazaji wote kwani kila mmoja na kipindi chake ni sawa na samaki na maji, anatuombea mungu atulinde na tuendelee kuwapa habari.

Tunamshukuru Francis Nyankaira kwa barua yake, na pia tunamshukuru Bw. Fras Manco Ngogo kuwaelezea wasikilizaji wetu wengine kuhusu hali ya nchini China na kuwasaidia wenzake kuijua zaidi China. Tunadhani kuwa Bw. Ngogo ana pilikapilika nyingi katika shughuli zake za kila siku, lakini tuna matumaini kuwa anaendelea kusikiliza matangazo yetu, na akipata nafasi anaweza kutuandikia barua. Hapa tunapenda kumtakia kila la heri.

Msikilizaji wetu sasa ni Bw. Sylivanus Angote wa sanduku la Posta 587 Bungoma, nchini Kenya anapenda kuishukuru sana Radio China Kimataifa kwa kuwasadia watu wengi kujifunza mengi kuhusu Radio China Kimataifa. Anasema maoni yake ni kuwa, kusiwe na burudani ya muziki kupita kiasi ili tusijewaudhi baadhi ya wasikilizaji.

Pia anaomba kama kuna uwezekano tubadilishe matangazo ya Radio China Kimataifa yawe yanatangazwa kuanzia saa mbili usiku ili watu wote waweze kusikiliza, ambapo watu wanakuwa hawana shughuli nyingi. Wakati wa mchana ni wachache sana wanaosikiliza. Hivyo, anapenda sana turekebishe muda ili waweze kupata matangazo yetu kila siku na kila wiki.

Tunamshukuru sana Bw. Sylivanus Angote kwa barua yake, maoni yake yametufikia, lakini kwa sasa tuna matangazo yanayosikika kupitia Radio KBC ambayo ni vigumu kwetu kubadilisha mpango uliopo, kwani tumepata nafasi hiyo ni kutokana na mpango wao. Kwenye matangazo yetu ya FM kila siku tuna masaa mawili ya kuanzia saa mbili hadi saa nne usiku, lakini tunasikitika kuwa mkoa Bungoma Kenya hamwezi kupata matangazo yetu kwenye mitabandi ya 91.9 FM ya Nairobi Kenya, labda katika siku za usoni tutaruhusiwa kubadilisha mpango wetu. Tunakuomba utuelewe.