Mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika ulifanyika mjini Beijing tarehe 4 hadi tarehe 5 mwezi Novemba mwaka 2006. Mkutano huo uliamua uhusiano wa kimkakati wa kiwenzi kati ya China na Afrika, hasa ushirikiano wa kiuchumi wa kunufaishana kati ya pande hizo mbili. Mwaka mmoja tangu mkutano huo ufanyike, China imetekeleza kwa makini sera nane za kuzisaidia nchi za Afrika zilizotolewa na Rais Hu Jintao kwenye mkutano huo, na imesifiwa na nchi zinazopata msaada. Kutokana na juhudi za pamoja za pande mbili, maendeleo ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika yamefikia kiwango kipya.
Habari zinasema kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Julai mwaka huu, uwekezaji wa moja kwa moja wa makampuni ya China barani Afrika ulikuwa dola za kimarekani milioni 485, na thamani ya biashara kati ya China na Afrika ilikuwa dola za kimarekani bilioni 39.3, ambayo iliongezeka kwa asilimia 30 kuliko mwaka jana wakati kama huu. China pia imeanzisha mfuko wa maendeleo ya China na Afrika ili kuyasaidia makampuni ya China kufanya uwekezaji barani Afrika. Tarehe mosi mwaka Julai, China ilifuta ushuru wa kuingia kwenye soko la China kwa bidhaa aina 454 kutoka nchi 26 zilizo nyuma kimaendeleo zaidi duniani; hatua za kujenga maeneo ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, vituo vya kielelezo vya ufundi wa kilimo na vituo vya kinga na matibabu ya malaria zinatekelezwa hatua kwa hatua; China imewaandaa wataalamu 4,150 kutoka nchi 49 za Afrika; kuzipatia bure nchi 18 dawa za kutibu malaria, kuwatuma vijana 75 wanaojitolea kwenye nchi 3.
Profesa Lucas Njoroge wa Idara ya uhusiano wa kimataifa wa chuo kikuu cha Nairobi, Kenya alipozungumzia utekelezaji wa miradi hiyo mbalimbali alisema,
"China imeongeza uwekezaji wa moja kwa moja barani Afrika, fedha hizo zinatumiwa katika viwanda mbalimbali, miradi ya ujenzi ukiwemo ujenzi wa miundo mbinu, na miradi ya nishati ukiwemo uchimbaji wa mafuta. China inazipatia nchi za Afrika chaguo jipya. Nchi za magharibi zinatoa msaada pamoja na masharti mengi. Hivyo nasema China imeipatia Afrika njia rahisi ya kupata msaada. Kushirikiana na China ni njia ya kupata maendeleo, tunatiwa moyo sana tunapopata maendeleo pamoja na China."
Mwanzoni mwa mwaka 2007, Rais Hu Jintao wa China anafanya ziara katika nchi 8 za Afrika. Ziara hiyo ilianzisha utekelezaji wa hatua nane katika pande zote, ambazo zimesukuma mbele ongezeko la uwekezaji wa China barani Afrika na kupanua ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara. Balozi wa China nchini Misri Bw. Wu Sike alipoeleza ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Misri alisema,
"Thamani ya biashara kati ya China na Misri iliongezeka kuwa dola za kimarekani bilioni 3.19 mwaka jana kutoka dola za kimarekani bilioni 1 miaka minne iliyopita. Mwaka huu inatazamiwa kufikia dola za kimarekani bilioni 4."
Kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika, mkurugenzi wa ofisi ya utafiti wa Afrika ya idara ya utafiti wa Asia ya Magharibi na Afrika ya taasisi ya sayansi ya jamii ya China Bibi. He Wenping alisema,
"Uchumi wa China ni sehemu moja ya uchumi wa dunia, uchumi wa Afrika pia ni sehemu ya uchumi wa dunia. Maendeleo ya uchumi wa China na Afrika yatahimiza utandawazi wa uchumi duniani."
|