Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-07 20:03:50    
Michezo ya Olimpiki ya Beijing itaungwa mkono zaidi kwa teknolojia za mtandao wa internet

cri

Katika mkutano wa mtandao wa Internet wa China kwa mwaka 2007 uliofanyika hivi karibuni, mada moja muhimu ya mkutano huo ilikuwa ni namna ya kutumia teknolojia za mtandao wa internet zinazoendelea siku hadi siku, ili kuunga mkono michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwaka 2008 hapa Beijing. Imefahamika kuwa, makampuni mengi ya teknolojia za mtandao wa internet ya China yanaendelea kuongeza uwekezaji katika eneo hilo.

Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008 ni michezo mikubwa itakayofuatiliwa duniani, makampuni mengi yanayotoa huduma za mtandao wa internet ya China yana matumaini ya kuunga mkono na kutangaza michezo hiyo kwa kutumia teknolojia za mtandao wa internet. Kwenye mkutano huo, naibu mkurugenzi wa bodi ya kampuni ya Soho ambayo ni kampuni maarufu katika eneo hilo nchini China Bw. Chen Luming alisema, kampuni ya Sohu ikiwa ni mshiriki wa pekee wa kutoa huduma za Internet kwa ajili ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008, kampuni hiyo ina raslimali nyingi za kutangaza michezo hiyo. Kwa hiyo tovuti yake Sohu itatoa matangazo ya mwaka nzima kuhusu michezo hiyo. Bw. Chen Luming alisema,

"tulianza matangazo yetu kabla ya michezo hiyo hadi mwishoni mwa mwaka huo, matangazo ya kabla ya michezo ni pamoja na shughuli za kukimbiza mwenge, maandalizi ya wachezaji wa China, maandalizi ya michezo hiyo na shughuli mbalimbali za michezo hiyo, na wakati michezo hiyo itakapoanza tunapanga kuweka mkazo katika kutangaza michezo na mahojiano na mabingwa. Tunalenga kutoa matangazo ya michezo na huduma za upashanaji habari kwa kasi, kwa usahihi, kwa kina na kuwajibika."

Bw. Chen Luming pia alisema, mbali na taarifa mbalimbali kuhusu michezo hiyo, tovuti ya Sohu pia imeshirikiana na serikali ya Beijing katika kuanzisha tovuti ya utoaji huduma kwa ajili ya michezo hiyo, ili kutoa taarifa na habari kwa watalii wa sehemu nyingine na wa nchi za nje katika michezo hiyo. Bw. Chen Luming alisema,

"pia tumeshirikiana na serikali ya Beijing katika kuanzisha tovuti kuu ya mji wa Beijing kwenye mtandao wa internet, iitwayo 'Beijing.com'. Tovuti hiyo inaonesha kwa pande zote taarifa mbalimbali kuhusu maisha, utalii, ununuzi na burudani mjini Beijing. Kwa kuwa ni vigumu kwa watazamaji wa kawaida kupata nafasi ya kukaa kwenye hoteli zilizoagizwa kwa ajili ya michezo ya Olimpiki, wengi wao watanunua tiketi na kujiandikisha wenyewe kwenye hoteli, watafuatilia zaidi taarifa mbalimbali kuhusu maisha mjini Beijing kupitia tovuti hiyo. Tovuti hiyo inaweza kukidhi mahitaji yao."

Mbali na makampuni ya kawaida ya mtandao wa Internet, teknolojia mpya za mtandao wa simu za mkononi pia zitatoa huduma kwenye michezo hiyo. Ofisa wa ofisi ya michezo ya Olimpiki ya Kampuni ya China Mobile Bw. Huang Tao alisema, ili kuunga mkono michezo ya Olimpiki ya Beijing, kampuni hiyo itajenga mfumo imara wa mawasiliano ya simu za mkononi na kuanzisha huduma za mtandao kwa kutumia simu za mkononi au kompyuta kwa kupitia njia pana ya mawasiliano kwa ajili ya shughuli mbalimbali, zikiwemo mawasiliano barabarani, ulinzi wa usalama, matibabu na utangazaji wa habari. Bw. Huang Tao alisema, kampuni ya China Mobile ilianzisha tovuti ya kwanza ya kiserikali kwa ajili ya simu za mikononi katika historia ya Olimpiki. Bw. Huang Tao alisema,

"kwenye msingi wa tovuti ya kawaida ya kiserikali ya Olimpiki inayohudumia watumiaji wa kompyuta, kampuni ya China Mobile imeanzisha tovuti ya kwanza ya Olimpiki kwa ajili ya simu za mikononi kwenye historia ya michezo hiyo, hivi sasa tovuti hiyo imeanza kufanya kazi. Kwenye tovuti hiyo watumiaji wanaweza kupata habari mpya kuhusu matokeo na ratiba ya michezo hiyo."

Teknolojia ya upashanaji habari ya simu za mkononi pia itaifanya michezo ya Olimpiki ya Beijing iendelee kwa ufanisi zaidi. Bw. Huang Tao alisema, kwenye viwanja vya michezo ya Olimpiki na sehemu ambazo watu wanakusanyika katika miji husika, kampuni ya China Mobile itaeneza teknolojia ya Mobile Broadband na kufikia sehemu hizo zote kwa huduma zake. Aidha kampuni hiyo pia itaanzisha mfumo wa upashanaji habari kwa ajili ya maofisa na vyombo vya habari katika michezo hiyo, ili kuwawezesha wafahamu kwa urahisi mambo mbalimbali ya michezo, yakiwemo ratiba ya michezo, uandikishaji wa wachezaji, picha na habari za michezo.

Bw. Huang Tao alisema teknolojia ya Mobile Fax inayotarajiwa kutumika katika mashindano ya mashua itaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa ufanisi wa michezo hiyo. Bw. Huang Tao alisema,

"zamani katika mashindano ya mashua, matokeo yake yalikuwa yanaweza kujulikana tu baada ya mashua kurudi kwenye sehemu ya kuanzia. Kwa hiyo kwa kawaida matokeo yalikuwa yanatolewa baada ya saa 2. Hivi sasa kwa kutumia teknolojia ya Mobile Fax, matokeo yanaweza kufikishwa kwenye kamati ya maandalizi ya michezo hiyo ndani ya dakika kumi kadhaa."

Michezo ya Olimpiki ni michezo mikubwa inayofuatiliwa duniani. Lakini si kila mtu anaweza kupata fursa ya kutazama michezo hiyo moja kwa moja, watazamaji wengi wanafuatilia michezo hiyo kwa njia ya vyombo vya habari, hasa matangazo ya televisheni. Watu bilioni 4 kote duniani wanakadiriwa kutazama matangazo ya michezo ya Olimpiki ya Beijing. Kwa hivyo kituo cha televisheni cha China CCTV ambacho ni kituo cha pekee chenye haki ya kutangaza michezo hiyo kwa njia ya televisheni nchini China, kitatumia channel 7 na kuitangaza michezo hiyo kwa pande zote. Mbali na hayo, tovuti ya CCTV pia itaonesha video zenye picha bora kuhusu michezo hiyo. Maneja mkuu wa kampuni ya CCTV.com Bw. Wang Wenbin alisema:

"hivi sasa tovuti ya CCTV inatangaza video zenye zaidi ya saa 500 zenye hakimiliki na picha bora kila siku, pia ina uwezo wa kuhifadhi na kushughulikia video zenye muda wa zaidi ya saa laki 2.2 kwenye mtandao wa Internet. Kabla ya michezo ya Olimpiki ya Beijing, CCTV.COM itatangaza michezo ya majaribio ya "Good Luck Beijing" kwa njia ya mtandao na simu za mkononi, ili kufanya mazoezi kwa ajili ya kutoa vizuri matangazo kwa njia ya mtandao na televisheni kuhusu michezo hiyo."