Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-08 19:08:42    
Maendeleo ya hali nchini Pakistan yanafuatiliwa na watu duniani

cri

Baraza la chini la bunge la Pakistan kwenye mkutano uliofanyika huko Islamabad tarehe 7 mwezi Novemba, lilipitisha uamuzi wa kuthibitisha uamuzi wa rais Pervez Musharraf wa Pakistan ambaye pia ni mkuu wa jeshi la nchi hiyo, kutangaza hali ya hatari kote nchini na kutekeleza katiba ya muda. Lakini siku hiyo rais Musharraf alisema, ataamua mustakabali wa bunge la hivi sasa tarehe 14 mwezi Novemba, na kutangaza hali ya hatari siyo uamuzi wa kudumu. Wachambuzi wanasema hali ya Pakistan ya hivi sasa iko kwenye "njia panda", na mwelekeo wake unafuatiliwa na watu.

Hali ya dharura iliyotangazwa nchini Pakistan imeingia kwenye siku ya tano, hali ya wasiwasi ya hivi sasa ya nchi hiyo imepungua, maisha ya wakazi yamerejea katika hali ya kawaida. Rais Musharraf anatarajia kudhibiti haraka hali ya nchi kwa kutumia njia ya kutangaza hali ya hatari, ili kupata uungaji mkono wa jumuiya ya kimataifa, na ili aendelee kuwa rais wa nchi na kufanya uchaguzi wa bunge katika mwezi Januari mwakani kama ilivyopangwa. Lakini njia hiyo siyo rahisi, kwani inahusiana na suala la mgawanyo wa madaraka.

Kabla ya hapo Bw. Musharraf alifanya mazungumzo ya mfululizo na waziri mkuu wa zamani nchi hiyo ambaye ni mwenyekiti wa chama cha wananchi Bibi Benazir Bhutto kuhusu kugawana madaraka. Tarehe 5 mwezi Oktoba, Bw. Musharraf alisaini na kutangaza makubaliano ya usuluhishi. Kutokana na makubaliano hayo mashtaka ya ufisadi dhidi ya Bibi Bhutto yataondolewa. Lakini baada ya kutangazwa kwa hali ya dharura nchini Pakistan, Bibi Bhutto amekuwa akimshinikiza Bw Musharraf kuondoa hali hiyo. Katika mkutano na waandishi habari uliofanyika tarehe 7 mwezi Novemba, Bibi Bhutto alimtaka Bw Musharraf ajiuzulu wadhifa wa mkuu wa jeshi la nchi kavu tarehe 15 mwezi huu kabla ya kwisha kwa kipindi cha urais wake, kuondoa hali ya hatari mara moja, kurejesha haraka iwezekanavyo katiba ya nchi, tume ya uchaguzi nayo inatakiwa kutangaza ratiba ya uchaguzi wa bunge la awamu ijayo na kuwaachia huru wanachama na mawakili waliokamatwa baada ya kutangazwa hali ya hatari. Alidokeza kwa makusudi kuwa, chama cha wananchi kitafanya maandamano makubwa tarehe 13 mwezi huu kutoka mji wa Lahore ulioko sehemu ya mashariki hadi mji wa mji mkuu wa Islamabad. Alisema hivi sasa bado hakuna mpango wa kufanya mazungumzo na Musharraf. Kuhusu jambo hilo Bw Musharraf tarehe 7 alisema, anapenda kufanya usuluhisho na vyama vyote vya kisiasa, wala siyo Bibi Benazir Bhutto peke yake. Alisema uamuzi utatolewa baada ya kushauriana na pande mbalimbali husika na kuzingatia maslahi makubwa ya nchi. Hivyo, namna ya kutimiza mgawanyo wa madaraka itakuwa ni kitu kisichokwepeka katika siku za baadaye nchini Pakistan.

Tarehe 5 mwezi Novemba, habari kuhusu Musharraf kuzuiliwa na jeshi zilienea nchini Pakistan, lakini hapo baadaye Bw Musharraf alijitokeza kuonana na mabalozi wa nchi za nje, na uvumi huo ukatoweka. Tarehe 7 mwezi Novemba Bw Musharraf alisema, hivi sasa majeshi yote yanamtii. Lakini baadhi ya wachambuzi wa habari bado wanaamini kuwa habari zile siyo uvumi, bali zitachangia mabadiliko ya utawala wa Pakistan.

Kutangaza hali ya hatari kwa Musharraf kumeleta suala gumu kwa Marekani: Je Marekani inataka sifa ya demokrasia au inataka hali halisi ya kupambana na ugaidi? Baada ya Pakistan kutangaza hali ya hatari, toka rais Bush hadi waziri wa mambo ya nje Condoleezza Rice na waziri wa ulinzi Robert Gates wote walieleza misimamo yao. Tarehe 5 mwezi huu, Bush alimhimiza Bw Musharraf aitishe haraka uchaguzi wa bunge, na kuvua sare ya jeshi. Bibi Rice anatarajia kuwa Bw Musharraf atabadilisha uamuzi wake kuhusu hali ya hatari, na kuitisha uchaguzi mkuu mwezi Januari mwaka kesho. Pia alisema Marekani, haiwezi kusitisha misaada kwa Pakistan. Naye Bw Gates alisema Marekani haitaki kusitisha ushirikiano na Pakistan kwenye mapambano dhidi ya kundi Al Qaeda na makundi mengine yenye silaha. Kwa vyovyote vile, uungaji mkono ni kitu muhimu cha kuamua mwelekeo wa hali ya siasa nchini Pakistan. Mbali na Marekani, Umoja wa Ulaya, Uingereza, Australia na Canada zote zimeeleza ufuatiliaji wake kuhusu hali ya nchini Pakistan.