Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-08 20:00:55    
Mkurugenzi wa kamati ya wakazi anayefurahia kazi yake

cri

Katika miji mbalimbali ya China, kuna kamati ya wakazi inayoshughulikia huduma za umma zinazohusiana na wakazi wa mitaa mbalimbali. Siku moja hivi karibuni, wakazi wanaopata misaada ya serikali ya uhakikisho wa kiwango cha msingi cha maisha walikuwa wanakutana kwenye ofisi ya kamati ya wakazi katika mtaa mmoja uliopo mashariki mwa mji wa Beijing. Wakazi hao wanakutana mara moja kwa mwezi, mbali na kupata misaada, pia wanaweza kupata habari kuhusu sera mpya za serikali na nafasi za ajira. Katika miji mbalimbali hapa nchini China, kuna kamati za wakazi kama hiyo karibu elfu 80.

Kazi za kamati ya wakazi ni ndogo ndogo tu, kama vile kutoa misaada ya fedha ya uhakikisho wa kiwango cha msingi cha maisha, kufanya usuluhishi wakati majirani wakiwa na mikwaruzano na kuwasaidia polisi katika kulinda usalama kwenye mitaa. Kutokana na kuwa shughuli hizo ni ndogo zinazohusu sekta mbalimbali na watu wa aina mbalimbali, kwa kawaida ni watu wa makamo au wazee wanaoshika nyadhifa za wakurugenzi wa kamati ya wakazi.

Hata hivyo maelezo haya yanamhusu kijana ambaye ni mkurugenzi wa kamati ya wakazi. Mwanamke huyo anaitwa Wang Xi, ana umri wa miaka 30, ambaye amekuwa akishika nafasi ya mkurugenzi wa kamati ya wakazi kwa miaka 7.

Mwaka 2000 Bi. Wang Xi alistaafu kutoka jeshini. Wakati huo serikali ya mji wa Beijing ilikuwa inatoa nafasi za ajira za makada wa mitaa ya makazi. Bi. Wang Xi alijiandikisha na kufaulu kwenye mitihani iliyofuata, akateuliwa kuwa mkurugenzi wa kamati ya wakazi mwenye umri mdogo kuliko wengine, wakati huo huo alikuwa na umri wa miaka 23 tu. Akikumbusha siku zile alipoanza kazi hiyo, bibi huyo alisema  "Nilipoanza kazi nilikuwa na hamu ya kujua kila kitu, na kila siku nilikuwa nafanya kazi bila kujali uchovu, nilikuwa najiuliza mara kwa mara, ni kwa nini bado hakuna mtu anayekuja kwangu ili nimsaidie?"

Lakini tukio moja lililotokea hapo baadaye lilimpa kijana huyo mtazamo mpya kuhusu wadhifa huo wa mkurugenzi wa kamati ya wakazi. Bi. Wang Xi akikumbusha alisimulia  "Yeye alikasirika na kunimwagia maji ya kikombe. Nilitokwa na machozi mara moja."

Kumbe kamati ya wakazi anakofanya kazi kijana huyo iko kwenye mtaa wa nyumba za zamani hapa mjini Beijing, ambapo kuna idadi kubwa ya familia zenye mapato ya chini na watu wasio na ajira. Kutokana na upinzani kuhusu sera fulani za serikali, baadhi ya wakazi walipotoa malalamiko kwenye kamati ya wakazi, walielekeza hasira zao kwa Bi. Wang Xi. Hii ni sababu ya kijana huyo kukumbwa na tukio la yeye kumwagiwa maji. Ingawa hapo baadaye walifikia maelewano, kijana huyo alijifunza kutokana na tukio hilo. Alitoa maoni yake akisema  "Wakati fulani sisi tunatakiwa kuwaruhusu wakazi waelekeze hasira zao na malalamiko yao kwetu, kwani hii ndiyo kazi yetu."

Lakini matukio yasiyowafurahisha watu si machache. Bw. Si Yaping mwenye umri wa miaka 43 ni naibu mkurugenzi wa kamati ya wakazi, yeye aliingia kwenye kamati hiyo ya wakazi pamoja na Bi. Wang Xi mwaka 2000. Akikumbusha matatizo yaliyowakabili mwanzoni walipoanza kazi, Bw. Si alisema  "Wang Xi alipoanza kazi alikumbwa na shida nyingi. Kwani kwenye mtaa kuna wakazi wa aina mbalimbali, baadhi yao wanakuja ofisini kwetu wakiwa na hasira, ni afadhali kuwasaidia ili wasiondoke wakiwa na hasira."

Wakati huo mara nyingi baada ya kazi kijana Wang Xi alikuwa anabaki peke yake kwenye ofisi ya kamati ya wakazi, akilia. Hata hivyo kijana huyo jasiri hakukubali kushindwa. Kutokana na hali halisi ya mtaa huo ambako kuna idadi kubwa ya familia zenye mapato ya chini na watu wasio na ajira, Wang Xi aliamua kuzingatia kuwasaidia wakazi hao ili waondokane na umaskini pamoja na kuanzisha hali ya maelewano miongoni mwa wakazi. Hatua kwa hatua wakazi wengi wenye shida wakaanza kuhisi ufuatiliaji wa kamati ya wakazi.

Bi. Feng Liyuan ni mkazi wa huko. Baada ya kuachana na mume wake, yeye anamlea mtoto peke yake, zaidi ya hayo anamtunza mama yake mzee ambaye afya yake si nzuri. Mbali na mzigo mkubwa wa maisha, Bibi Feng alikuwa hana ajira ya uhakika. Alisema  "Ninamlea mtoto na kumtunza mama yangu mwenye umri wa miaka zaidi ya 70 peke yangu. Maisha yalikuwa magumu kweli."

Baada ya kufahamishwa hali hiyo, Bi. Wang Xi alimsaidia mama Feng kuomba msaada wa fedha wa serikali wa kuhakikisha kiwango cha msingi cha maisha, na kuwasiliana na mashirika ya vijana ili binti wa mama Feng anayesoma kwenye shule ya sekondari apate msaada wa masomo. Kutokana na juhudi za kamati ya wakazi, familia ya Bibi Feng sasa ina mapato ya uhakika. Mama huyo alimsifu sana Wang Xi. "Mkurugenzi wa kamati yetu ya wakazi ni mzuri sana, anatusaidia kweli."

Ili kuwasaidia wakazi wasio na ajira, Wang Xi aliwasiliana na viwanda vikubwa, kutafuta habari mbalimbali kuhusu nafasi za ajira na kutangaza habari hizo kwa wakati. Kutokana na msaada wake, Bw. Yang Hongbo mwenye umri wa miaka 42 alipata ajira yenye mapato ya uhakika.

Mbali na hayo Wang Xi akiongoza makada wa kamati ya wakazi, waliandaa shughuli mbalimbali za burudani kwa ajili ya wakazi, yakiwemo mazoezi ya kujenga mwili, mashindano ya kupiga picha, mafunzo ya ushonaji na kuwashirikisha wazee kutembelea vivutio kwenye kitongoji. Wang Xi alisema amezoea kuitwa na wakazi "mkurugenzi mdogo", na kupenda kuwahudumia wakazi hao wanaomfanya aone kazi ngumu na kufurahia kazi hiyo.