Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-09 15:27:35    
Hali mpya imetokea katika uhusiano kati ya nchi tatu za Marekani, Iran na Iraq

cri

Hivi karibuni hali mpya imetokea katika uhusiano kati ya nchi tatu za Marekani, Iran na Iraq. Tarehe 6 msemaji wa jeshi la Marekani Bw. Greg Smith alithibitisha kuwa watu tisa wa Iran waliokuwa wanashikiliwa na jeshi la Marekani nchini Iraq, wataachiwa huru katika siku za karibuni. Kati ya watu hao, wawili walikamatwa na jeshi la Marekani katika sehemu ya kaskazini ya Iraq. Wakati huo jeshi la Marekani liliwakamata watu watano wa Iran kwa kuwashuku kuwa ni watu kutoka kikosi cha Jeshi la Ulinzi la Mapinduzi la Iran waliokuwa wamejificha nchini Iraq kutoa msaada kwa vikosi vya madhehebu ya Shia. Lakini Iran ilitetea kwamba watu hao watano ni wanadiplomasia wa Iran, na kuitaka Marekani iwaachie huru mara moja. Tukio hilo lilisababisha uhusiano kati ya Iran na Marekani kuwa wa wasiwasi zaidi, na liliathiri uhusiano kati ya Iran na Iraq. Kutokana na hayo, tarehe 6 jeshi la Marekani lilitangaza kuwaachia huru watu hao. Uamuzi huo wa jeshi la Marekani mara moja ulikaribishwa na pande mbalimbali.

Siku ya pili, yaani tarehe 7 wizara ya mafuta ya Iraq ilitangaza kuwa Iraq na Iran zimekubaliana kutandika njia mbili za mabomba ya kusafirisha mafuta kutoka bandari ya Basra, kusini mwa Iraq, hadi kwenye bandari ya Abadan nchini Iran. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, njia moja inasafirisha mapipa laki moja ya mafuta kwa siku kutoka Iraq hadi Iran na kuiuzia mafuta Iran kwa bei ya kimataifa, na njia nyingine inasafirisha mafuta kutoka Iran hadi Iraq.

Baada ya matukio hayo mawili kutokea, wachambuzi wanaona kuwa Marekani na Iraq zinaonesha urafiki kwa Iran, mpaka sasa Iran bado haijatoa kauli yoyote kuhusu matukio hayo, lakini kuna habari zinazoonesha kuwa Iran pia imekuwa ikionesha urafiki kwa kiasi fulani. Mwanzoni mwa mwezi huu waziri wa mambo ya nje wa Iran Bw Manouchehr Mottaki alipokuwa ziarani Baghdad aliwahi kusema, ili kuiboresha hali ya usalama nchini Iraq, Iran iko tayari kufanya mazungumzo tena na Marekani.

Kwa kuzingatia jinsi Marekani, Iran na Iraq zilivyoonesha hivi karibuni, inaonekana kuwa uhusiano kati ya nchi hizo tatu unaelekea kuwa mzuri. Wachambuzi wanaona kutokea kwa mwelekeo huo kunalingana na manufaa ya nchi zote tatu.

Kutokana na hali ilivyo nchini Iraq, kuboresha uhusiano kati yake na Iran kutasaidia kutuliza vurugu za Iraq. Kwa sababu ingawa Iran inakanusha kwamba inaunga mkono vikosi vya upinzani nchini Iraq, lakini kuna habari zikisema kuwa kweli ina maingiliano na vikosi vya upinzani kikiwemo kikosi kinachoongozwa na kiongozi wa madhehebu ya Shia Bw. Moqtada al-Sadar. Na hata baadhi ya vyombo vya habari vinasema hivi sasa Bw. Sadar yuko nchini Iran.

Kwa upande wa Marekani, kuwasiliana na Iran pia kutaleta manufaa kwa Marekani. Hivi sasa Marekani imezama ndani ya matope na inashindwa kujinasua, ingawa hivi karibuni idadi ya askari wa Marekani waliouawa na kujeruhiwa imepungua, lakini mwaka huu idadi ya askari waliouawa na kujeruhiwa imezidi 850, idadi ambayo ni kubwa tokea mwaka 2003. Na wananchi wa Marekani wanazidi kutaka jeshi la Marekani liondoke Iraq. Kwa hiyo kama Marekani na Iran zikiweza kupata suluhu, na Iran ikiweza kutoa mchango wake katika utatuzi wa suala la Iraq na kama ikiweza kulegeza msimamo wake mkali, hakika hali hii ni manufaa kwa Marekani.

Kwa upande wa Iran, kama nchi hiyo ikiweza kutoa mchango katika utatuzi wa suala la Iraq na kupunguza upinzani dhidi ya nchi za Magharibi, na kupunguza shinikizo kutoka nchi hizo, pia ni manufaa kwa Iran. Kwa hiyo, wachambuzi wanaona kuwa, hali nzuri kwenye uhusiano kati ya nchi za Marekani, Iran na Iraq imeleta uwezekano wa kufanyika tena kwa mazungumzo.

Idhaa ya kiswahili 2007-11-09