Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-12 19:45:32    
Hali ya usalama nchini Iraq bado mbaya

cri

Tarehe 11 waziri mkuu wa Iraq alitoa tathmini kwa furaha kuhusu hali ya usalama nchini Iraq akisema, milipuko ya mabomu na ya kujiua nchini Iraq imepungua sana, na migogoro kati ya madhehebu ya kidini imemalizika. Kadhalika jeshi la Marekani nchini Iraq pia lina mtazamo huo huo. Wiki iliyopita amirijeshi wa jeshi la Marekani nchini Iraq Bw. Joseph Fil alisema, tokea mwezi Juni matukio ya mauaji yalianza kupungua na yanaendelea kupungua mwezi hadi mwezi. Lakini wachambuzi wana maoni tofauti na Bw. Joseph Fil, wao wanaona kuwa ingawa milipuko imepungua, hii haimaanishi kuwa chanzo cha milipuko kimetoweka. Wanao migogoro kati ya madhehebu ya kidini nchini Iraq ni sababu kubwa ya kutokea kwa matukio ya mauaji, na migogoro hiyo bado inaendelea kuwepo. Idadi ya waumini wa madhehebu ya Shia nchini Iraq ni kubwa, lakini katika miaka ya utawala wa Saddam walioshika madaraka walikuwa ni watu kutoka madhehebu ya Suni ambayo idadi yake ni ndogo, viongozi wengi wa madhehebu ya Shia na Wakurd walinyanyaswa. Vita vya Marekani dhidi ya Iraq vimevunja hali hiyo ya kisiasa iliyokuwepo wakati wa utawala wa Saddam, madhehebu ya Suni yamepoteza madaraka na madhehebu ya Shia na Wakurd wamemiliki uongozi. Mabadiliko hayo ya madaraka yamezidisha migogoro ya madhehebu ya kidini na tofauti za kikabila. Tokea mwaka huu, kutokana na kurodhirika na utendaji wa serikali, mawaziri sita wanaomwunga mkono kiongozi wa Madhehebu ya Shia Moqtada al-Sadar, mawaziri sita wa "Iraqi Accordance Fraont" cha wafuasi wa madhehebu ya Suni na mawaziri tano wa chama cha "Iraqiya List" kinachoongozwa na waziri mkuu wa zamani Bw Ayad Allawi, kwa nyakati tofauti walitangaza kuipinga serikali ya Iraq na kusababisha karibu nusu ya mawaziri kusimama kufanya kazi zao. Hali inadhihirisha kuwa migogoro kati ya madhehebu sio tu imepungua, bali imezidi kuwa mikali.

Pili, vikundi vya kigaidi vinavyofanya mauaji havijaangamizwa kabisa. Ingawa majeshi ya Iraq na Marekani nchini Iraq yamewahi kufanya misako mara nyingi dhidi ya vikundi vya Al-Qaida na vikundi vingine vya watu wenye silaha, lakini mtandao wa shughuli za kigaidi za kundi la Al-Qaida na vikundi vya watu wenye silaha haujasambaratishwa, baadhi ya magaidi wametorokea nchi za nje na baadhi wanaendelea kuwepo kwenye sehemu mbalimbali nchini Iraq na kufanya mashambulizi. Milipuko kadhaa iliyotokea katika mwezi uliopita mjini Baghdad inasemekana ilifanywa na kundi la Al-Qaida. Zaidi ya hayo, vyombo vya habari vya Magharibi vimedokeza kuwa wafuasi wa kundi la Al-Qaida waliokimbilia nchi za nje sasa wanajiunga na kutaka kurudi nyumbani Iraq.

Isitoshe kuwepo kwa majeshi ya nchi za nje nchini Iraq, pia ni sababu nyingine kubwa inayosababisha kuendelea kwa matukio ya mauaji nchini Iraq. Majeshi ya mataifa yanayoongozwa na jeshi la Marekani nchini Iraq mwezi Machi mwaka 2003 yalianzisha vita dhidi ya Iraq bila idhini ya Umoja wa Mataifa na kusababisha vifo vya watu wengi wa Iraq, hii ni kama mbegu ya chuki iliyopandwa mioyoni mwa watu wa Iraq, kwa hiyo si ajabu kwa majeshi ya mataifa ya nje kushambuliwa mara kwa mara. Ilimradi tu majeshi ya mataifa ya nje yakiendelea kuwepo nchini Iraq, watu wa Iraq watakuwa na chuki na kulipa kisasi na milipuko kando ya barabara na ya kujiua haitapungua.

Si hayo tu, hivi sasa Iraq inakabiliwa na tatizo jipya la usalama, kwamba Uturuki imetuma askari wake laki moja kwenye eneo la mpakani kati ya Uturuki na Iraq, serikali ya Uturuki ikiamrisha askari wake kuvuka mpaka na kushambulia vikosi vya Chama cha PPK cha Kurdistan, itakuwa vigumu kudhibiti hali ya sehemu ya kaskazini mwa Iraq, na huenda italeta matokeo mabaya yasiyoweza kutarajiwa katika sehemu nyingine nchini humo.