Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-14 15:15:09    
Kauli ya Bibi Benazir Bhutto yasababisha wasiwasi wa kisiasa nchini Pakistan

cri

Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Umma cha Pakistan Bibi Benazir Bhutto, tarehe 13 huko Lahore alisema huenda Chama cha Umma anachokiongoza hakitashiriki kwenye uchaguzi wa bunge. Kauli hiyo imesababisha hali ya wasiwasi wa kisiasa nchini Pakistan.

Tokea tarehe 3 Bw. Pervez Musharraf alipotangaza hali ya hatari nchini Pakistan, sasa anakumbwa na shinikizo kutoka nchini na nchi za nje. Kwanza ni shinikizo kutoka nchini Pakistan. Vyama vya wapinzani vinamtaka Bw. Musharraf aondoe hali ya hatari, na hasa chama kikubwa cha upinzani kinachoongozwa na Bibi Benezir Bhutto, Chama cha Umma, ambacho kinamtaka Bw. Musharraf aondoe hali ya hatari na aachie wadhifa wake wa jeshi.

Bibi Benazir Bhutto kwenye makazi yake ya muda mjini Lahore alipozungumza na waandishi wa habari alisema, "Chama cha Umma pengine hakitashiriki kwenye uchaguzi wa bunge utakaofanyika hivi karibuni." Alisema kama Bw. Musharraf atakuwa rais hatashiriki kwenye serikali yake, alimtaka Musharraf aachie wadhifa wa urais. Hii ni mara ya kwanza kwa Bibi Benazir Bhutto kumtaka Bw Musharraf aachie wadhifa wa urais. Bibi Bhutto alisema Chama cha Umma kitaanzisha muungano na vyama vingine vya upinzani kiwemo chama kinachoongozwa na waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Bw Nawaz Sharif. Habari zinasema Bw. Nawaz Sharif alionesha furaha baada ya kusikia kauli hiyo ya Bibi Bhutto, alisema "Hii ni hatua nzuri ya kutimiza lengo pamoja la vyama vya upinzani."

Pili shinikizo kutoka nchi za nje. Marekani mara nyingi inamhimiza Bw Musharraf aondoe hali ya hatari nchini Pakistan na kufanya uchaguzi wa bunge kwa wakati uliopangwa, na kusema kwamba itafikiria upya kuhusu misaada inayoitoa kwa Pakistan. Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Jumuiya ya Madola hivi karibuni walifanya mkutano mahsusi huko London, waliitaka Pakistan iondoe hali ya hatari kabla ya tarehe 22, ama sivyo Pakistan itasimamishwa uanachama wa Jumuiya ya Madola.

Ili kukabiliana na shinikizo kutoka nchini na nchi za nje, Bw. Musharraf kwa upande mmoja anajitahidi kuungana na vyama vya upinzani nchini ili kupata uungaji mkono wao. Kwa upande mwingine ametangaza kufanyika kwa uchaguzi wa bunge kabla ya tarehe 9 Januari mwaka kesho. Hatua hiyo imekaribishwa na Bibi Bhutto na jumuiya ya kimataifa, hasa Marekani. Kwa sababu awamu ya urais ya Musharraf itamalizika tarehe 15 mwezi huu, na kabla ya hapo pengine mahakama kuu ya Pakistan itakuwa imetoa hukumu ya mwisho kuhusu hadhi yake ya kugombea tena urais. Kama mambo yote yatakuwa shwari anaweza kutimiza ahadi yake kwamba ataapishwa kuwa rais akiwa raia. Hivi sasa ingawa Bw. Musharraf hajatangaza lini ataondoa hali ya hatari nchini Pakistan, lakini Mwendeshaji mashtaka mkuu wa Pakistan Bw. Malik Qayum alisema, huenda hali hiyo itaondolewa ndani ya muda wa mwezi mmoja.

Hapo mwanzo Bw Pervez Musharraf alipotangaza hali ya hatari Bibi Bhutto alisema anataka uchaguzi ufanyike kwa haki, wazi na uhuru na kumtaka Bw Musharraf aachishe wadhifa wa kijeshi. Lakini sasa amekuwa vingine kabisa, kwamba anataka jumuiya ya kimataifa iache kumwunga mkono Bw Musharraf na anamtaka ajiuzulu urais. Mabadiliko ya msimamo wake yamesababisha hali ya kisiasa nchini Pakistan kuwa ya utatanishi. Zaidi ya hayo, ingawa maandamano yamepigwa marufuku, na Bi. Bhutto anazuiliwa ndani ya makazi yake ya muda, lakini Chama cha Umma kimefanikiwa kuongoza msafara wa magari 200 kufanya maandamano kutoka Lahore, hii ni changamoto nyingine kwa Bw. Musharraf.

Wachambuzi wanaona kuwa kwa upande mmoja mabadiliko ya msimamo wa Bibi Bhutto yamesababisha wasiwasi wa kisiasa nchini Pakistan, lakini kwa upande mwingine pia inawezekana atashirikiana na Bw. Musharraf. Siku chache zilizopita kwenye mkutano na waandishi wa habari Bw. Musharraf alisema, matokeo ya uchaguzi yataamua "atasimama na nani kwenye handaki moja la kivita".

Idhaa ya kiswahili 2007-11-14