Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-15 18:43:08    
Mabadiliko ya chakula kwenye familia za Wachina

cri
Asubuhi ya siku moja ya Ijumaa, kulikuwa na pilikapilika nyingi kwenye chumba kimoja cha mtaa wa makazi uitwao Yuquan Xili, magharibi mwa mji wa Beijing, ambapo wazee zaidi ya 20 walikuwa kwenye semina kuhusu mafunzo ya lishe. Miongoni mwa wazee hao, mwenye umri mdogo zaidi alikuwa na umri wa miaka 53 na mkubwa zaidi ni mzee mwenye umri wa miaka 81.  Mwalimu wao ni daktari Han Rui kutoka zahanati ya mtaa. Akiwafahamisha wazee hao ujuzi kuhusu vyakula na virutubisho, alisema

"Kila siku tunapaswa kula vyakula vyenye asidi na vyenye alikali. Kwa ufupi, ukila kipande kimoja cha nyama, unatakiwa kula matonge manne hadi saba ya mboga za majani. Na matonge manne ya mboga ni kiwango cha chini kabisa."

Hivi sasa semina kama hiyo inawavutia watu wengi sana nchini China. Zamani Wachina walikuwa wanazingatia tu namna ya kupata shibe, lakini hivi sasa wanatilia maanani lishe na afya njema. Bi. Zhao Guilan aliyehudhuria semina hiyo alisema, "Mimi nafurahia kuhudhuria semina kama hii, naweza kutumia ujuzi niliopata mara ninaporudi nyumbani. Zamani tulikuwa na mtizamo wa kizamani kuwa jambo muhimu ni kupata shibe. Hivi sasa kutokana na kuinuka kwa kiwango cha maisha, inafaa tufahamishwe namna ya kuishi kwa afya njema na kwa raha mustarehe katika siku za uzeeni."

Mbali na wazee kama mama huyo, vijana wengi wa China pia wameanza kuzingatia uwiano wa virutubisho vitokanavyo na vyakula vya aina mbalimbali.

Hapa ni kwenye duka la vitabu lililopo katikati ya mji wa Beijing. Bw. Ma Jianzhong mwenye umri wa miaka zaidi ya 30 alikuwa amesimama mbele ya safu za vitabu vinavyohusu afya na virutubisho, akichagua vitabu anavyotaka. Alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari, Bw. Ma alisema  "Nilipokuwa mwanafunzi sikufuatilia suala hilo, wakati nilipojiona mzima kabisa kama chuma cha pua kutokana na ujana. Baadaye nilipokwenda kusoma nchi za nje, nilianza kuhisi hali yangu ya afya inadidimia. Baada ya kurudi nyumbani, wazazi wangu walikuwa wananipa chakula chenye virutubisho mbalimbali. Mwanzoni niliona ufanisi wa mbinu hizo unajitokeza pole pole, baada ya miezi kadhaa nilihisi kuwa nguvu zimerudi. Nikaanza kukubali ufanisi wa mbinu hizo. Leo nimekuja kwa ajili ya kutafuta vitabu vinavyohusu mbinu hizo ili kujenga mwili."

Bi. Shen Yuanyuan aliyefunga ndoa hivi karibuni ni mteja mwingine aliyekuwa anachagua vitabu vinavyohusu lishe. Alisema "Zamani tulikuwa tunakula kama tunavyopenda. Lakini hivi sasa inafaa kufuata sayansi kuhusu suala la chakula ili kujenga mwili. Na kama katika siku za baadaye nikitaka kuzaa mtoto, hii itasaidia afya ya ujauzito wangu."

Mwaka 1988 serikali ya China ilitoa taarifa kuhusu mwongozo wa lishe kwa lengo la kuwaelekeza wananchi wapate mtizamo wa kisayansi kuhusu vyakula. Lakini je, kwa nini hadi hivi sasa ambapo ni miaka karibu 20 baada ya kutolewa kwa taarifa hiyo ndipo watu wengi wa China wameanza kuzingatia suala la lishe?

Bi. Zhao Xiuying ni mtaalamu aliyewahi kushirki kwenye utungaji wa mwongozo huo. Alijibu swali hilo.  "Mwanzoni mwa miaka ya 1980, watu wa China walikuwa wanajitahidi kupambana na njaa, na walikuwa bado hawajaanza kufuatilia suala la lishe. Lakini kuanzia miaka ya 1990, wizara ya sayansi na teknolojia ya China imekuwa ikitenga fedha nyingi kwa ajili ya utafiti wa mambo ya lishe, na kutokana na kuinuka kwa kiwango cha maisha, wananchi pia wanapenda kupata ujuzi wa lishe ili wawe na afya njema."

Kwenye shule ya awali ya Lingnan hapa mjini Beijing, watoto walikuwa wanasubiri chakula cha mchana. Wapishi wawili wa shule hiyo wanawahudumia watoto 200 wenye umri wa kati ya mwaka mmoja na nusu na miaka 6, ambao wanapata milo mikubwa mitatu na milo midogo miwili kila siku.

Siku hiyo watoto walikula wali, viazi na nyama, pamoja na mboga kama chakula cha mchana. Mkuu wa shule hiyo ya awali Bw. Li Jihua alisema, wizara ya elimu ya China bado haijatoa agizo, lakini shule za awali za China bara zinatoa milo mikubwa mitatu na milo midogo miwili kwa siku, na vyakula mbalimbali vinaandaliwa kwa kufuata mwongozo wa lishe.

Nchini China wanafunzi na wafanyakazi wengi wanakula chakula mabwaloni katika siku za kazi. Habari zinasema hivi sasa vyakula vya mabwaloni bado vina upungufu wa virutubisho, kama vile kutiwa mafuta mengi na chumvi nyingi.

Kuhusu suala hilo mtaalamu wa lishe Bi. Zhao Xiuying aliishauri serikali ipitishe hatua za kuyalazimisha mabwalo yafuate kanuni za virutubisho.  "Hivi sasa kuna upungufu mkubwa wa washauri kuhusu mambo ya lishe kwenye mabwalo yanayowahudumia watu wengi. Naona ni lazima kila bwalo linalowahudumia watu zaidi ya 100, liwe na wataalamu wa mambo ya lishe, zaidi ya hayo mabwalo yanatakiwa kutoa bure vijitabu vya kutangaza ujuzi wa lishe, vikiwaelekeza wananchi wachague vyakula vinavyofaa. Kwa hiyo mwongozo wa lishe utajulikana miongoni mwa watu."

Imefahamika kuwa kutokana na msaada kutoka shirika la taaluma ya virutubisho la China, wizara ya afya ya China imemaliza utungaji wa muswada wa sheria ya kwanza inayohusu lishe iitwayo "utaratibu wa lishe bora". Kabla ya kutolewa kwa utaratibu huo, wizara ya afya ya China tarehe mosi Septemba mwaka huu ilitangaza mradi wa afya unaojulikana kama "121". Mtaalamu wa lishe Bi. Zhai Xiuying alitoa ufafanuzi mfupi juu ya mradi huo, akisema "Moja ya kwanza ni kutembea kwa hatua elfu 10 kwa siku, mbili maana yake ni kudumisha uwiano kati ya vyakula na mazoezi ya kujenga mwili, na moja ya mwisho inamaanisha kuwa na afya njema kwa maisha yote."

Idhaa ya kiswahili 2007-11-15