Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-19 20:31:48    
Moja ya mbinu 36, Kufanya urafiki na madola yaliyo mbali na kushambulia yaliyo karibu

cri

Kabla ya kueleza mbinu ya "kufanya urafiki na madola yaliyo mbali na kushambulia yaliyo karibu", kwanza tueleze chanzo cha mbinu hiyo.

Katika karne ya tatu, China ilikuwa katika Kipindi cha Madola ya Kivita, mara kwa mara watawala wa madola walikuwa wanapigana mara kwa mara, na pia walikuwa wanaungana ili kupambana na madola mengine, hali ilikuwa ya utatanishi sana. Katika miaka ya mapambano Dola la Qin lililokuwa katika sehemu ya kaskazini ya China lilistawi haraka, na lilianza kuyaangamiza madola mengine likiwa na lengo la kuitawala China nzima. Wakati huo Dola la Qi lililokuwa katika sehemu ya mashariki ya China pia lilikuwa na nguvu. Mfalme wa dola la Qin alifikiri kwamba dola hilo pengine litakuwa mpinzani wake katika juhudi za kujipatia China nzima, kwa hiyo alitaka kulishambulia dola la Qi. Fan Sui ambaye alikuwa mshauri wa mfalme wa dola la Qin alipinga na kumweleza mfalme wake kwamba, madola ya Qin na Qi yanatengana mbali kijiografia, dola la Qin likishambulia dola la Qi litavuka madola mawili ya Han na Wei. Zaidi ya hayo, kutoka dola la Qin hadi dola la Qi safari ni ndefu, askari wachache wakitumwa itakuwa ni shida kupata ushindi, na askari wakitumwa kwa wingi usalama wa nyumbani utakuwa hatarini, kwa hiyo ni busara kushambulia madola yaliyo karibu ya Han na Wei, kisha kulishambulia dola la Qi, lakini kabla ya kulishambulia dola la Qi ni lazima kufanya urafiki na dola hilo, ili lisishirikiane na madola ya Han na Wei kupambana na dola la Qin kwa pamoja."

Mfalme wa dola la Qin alikubali ushauri wa Fang Sui na kufanya urafiki na dola la Qi, na kuyameza madola madogo yaliyokuwa karibu kuiteka sehemu yote ya kaskazini ya China. Baadaye dola hilo liliangamiza dola la Chu lililokuwa kusini mwa China na mwishowe liliangamiza dola la Qi. Dola la Qin liliitawala China nzima chini ya utawala wa mfalme mmoja.

Katika kitabu cha "Mbinu 36 za Kivita", kuhusu mbinu hiyo ya "kufanya urafiki na madola yaliyo mbali na kushambulia yaliyo karibu" inaeleza hivi, kwamba iwapo nia ya ushambulizi inapozuiliwa kutokana na umbali wa kijiografia, ni busara kuwaangamiza maadui walio karibu kabla ya kuwashambulia maadui walio mbali, isitoshe, ili kuzuia maadui wasishirikiane ni lazima kuwafarakanisha maadui na kuwaangamiza mmoja baada ya mwingine. Ni wazi kwamba mbinu hiyo ni ujanja wa kujipatia muda wa kuwaangamiza maadui walio mbali, na baada ya kuwaangamiza maadui walio karibu, maadui walio mbali watalengwa. Wachina wa zama za kale walieleza sababu ya kuwaangamiza maadui walio karibu, kwamba katika hali ya vurugu za kivita kati ya mataifa maadui walio karibu watakuwa hatari kwako, kwa hiyo ni bora kuwaangamiza kabla ya kuwashambulia maadui walio mbali.

Mbinu ya "kufanya urafiki na madola yaliyo mbali na kushambulia yaliyo karibu" pia inatumika katika mambo yasiyo ya kijeshi. Mwishoni mwa Enzi ya Yuan vilitokea vikundi vingi vya uasi, na Bw. Zhu Yuanzhang pia aliongoza kikundi kimoja kushiriki katika uasi. Katika mapambano, baadhi ya vikundi viliangamizwa na jeshi la mfalme na baadhi vilijiunga na Zhu Yuanzhang, mwishowe Zhu Yuanzhang aliupindua utawala wa Enzi ya Yuan na kuwa mfalme wa Enzi ya Ming. Zhu Yuanzhang alizaliwa katika ukoo maskini sana, baada ya kuwa mfalme alihofia angepinduliwa na majemadari waliofuatana naye katika vita dhidi ya utawala wa Enzi ya Yuan, kwa hiyo alitumia mbinu hiyo ya "kufanya urafiki na madola yaliyo mbali na kushambulia yaliyo karibu", akawafarakanisha na kuwamaliza maofisa wote aliowaona ni hatari kwake, baadaye aliwakusanya watu wasiokuwa na mazingira ya kisiasa na ya kijeshi kuwa maofisa wake. Maofisa hao licha ya kuwa wasingeweza kuwa hatari kwake tena walikuwa na shukurani nyingi kwa mfalme na walikuwa watiifu wakubwa.

Mbinu ya "kufanya urafiki na madola yaliyo mbali na kuangamiza yaliyo karibu" kwa kiasi fulani ina udanganyifu, na udanganyifu huo ni rahisi kugunduliwa. Dola la Qi halikudanganywa kwa mbinu hiyo, ila tu halikuwa na uhakika wa kulishinda dola la Qin kwa hiyo lilikubali kuwa na urafiki nalo.