Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-20 15:01:11    
Kabla ya kufanyika kwa mkutano wa amani wa Mashariki ya Kati pande husika zajitahidi kuleta mazingira bora ili kuufanikisha

cri
Mkutano wa kimataifa wenye lengo la kusukuma mchakato wa mazungumzo kati ya Palestina na Israel na amani ya Mashariki ya Kati, utafanyika mwishoni mwa mwezi huu huko Annapolis, Marekani. Kabla ya mkutano huo kufanyika pande husika zinajitahidi kuleta mazingira mazuri ili kuufanikisha mkutano huo.

Waziri mkuu wa Israel Bw Ehud Olmert na mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas tarehe 19 huko Jerusalem walifanya mazungumzo kwa muda wa saa mbili. Msemaji wa serikali ya Israel Bibi Miri Eisin alisema, pande mbili zimefikia makubaliano fulani katika rasimu ya taarifa ya pamoja. Mjumbe wa kwanza wa mazungumzo wa Palestina Bw. Saeb Erekat alisema, kwenye mazungumzo hayo viongozi wa pande mbili walitoa mapendekezo mapya kuhusu namna ya kuondoa tofauti kati yao, na vilevile walitaka vikundi vya kazi vya kila upande viendelee na majadiliano katika siku hiyo ili kupunguza zaidi tofauti kati yao.

Aidha siku hiyo Israel ilichukua hatua mbili za kuonesha urafiki kwa Palestina. Moja ya hatua hizo mbili ni kuwa baraza la mawaziri la Israel limeamua kuwaachia huru wafungwa 441 wa Palestina. Hatua hiyo ni jibu kwa ombi la Mahmoud Abbas la kutaka kuwaachia huru wafungwa wa Palestina 2000 kabla ya mkutano wa kimataifa wa amani ya Mashariki ya Kati. Hatua nyingine kati ya hatua hizo mbili ni kuwa Bw Ehud Olmert ameahidi kusimamisha ujenzi wa makazi ya wayahudi kwa mujibu wa matakwa ya "ramani ya amani", na haitajenga makazi mapya kwenye ukingo wa magharibi wa Mto Jordan wala kupanua zaidi eneo la ardhi. Kadhalika serikali ya Israel itaondoa makazi yaliyojengwa bila ruhusa ya serikali. Hii ni mara ya kwanza kwa Bw Ehud Olmert kutoa ahadi hiyo hadharani kuhusu suala la makazi tokea vikundi vya mazungumzo vya Palestina na Israel vilipotaka kutekeleza kipindi cha kwanza cha mpango wa "ramani ya amani" kabla ya kusaini makubaliano yoyote tarehe 8. Kabla ya hapo Palestina iliwahi kuiambia Marekani kuwa kusimamisha kabisa ujenzi wa makazi ni matakwa ya kimsingi ya Palestina kabla ya mkutano wa amani ya Mashariki ya Kati. Na matakwa hayo pia sharti muhimu kwa Saudi Arabia, nchi ambayo ni muhimu ili kufanikisha mkutano huo. Kutokana na hayo, ahadi ya Bw Ehud Olmert inasaidia kupunguza migongano kati ya Palestina na Israel na inasaidia mkutano huo uungwe mkono na Saudi Arabia na nchi nyingine jirani za Kiarabu.

Imefahamika kuwa ili kusukuma mbele mazungumzo ya amani kati ya Palestina na Israel, Umoja wa Ulaya pia ulichukua hatua mpya. Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Umoja wa Ulaya tarehe 19 uliidhinisha ripoti iliyotolewa na mjumbe wa mambo ya nje wa Umoja huo Bibi Benita Ferrero-Waldner na mjumbe mwandamizi anayeshughulikia sera za kidiplomasia mambo ya usalama Bw. Javier Solana, na kuahidi kuunga mkono makubaliano yoyote yatakayopatikana katika mkutano huo wa amani ya Mashariki ya Kati, na huku mkutano huo ukihimiza nchi za Kiarabu zitoe misaada ya kiuchumi kwa Palestina. Zaidi ya hayo, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Nchi za Kiarabu tarehe 22 pia watafanya mkutano wa kusawazisha misimamo yao kuhusu masuala ya Mashariki ya Kati na mambo mengine.

Ingawa mazingira hayo yanasaidia kufanikisha mkutano huo wa amani ya Mashariki ya Kati, lakini vyombo vya habari pia vina wasiwasi kuhusu mkutano huo. Kwanza, kuhusu taarifa ya pamoja, ingawa vikundi vya mazungumzo vilifanya mazungumzo mara nyingi tokea tarehe 8 lakini tofauti bado ni nyingi.

Pili, Palestina haijaridhika na ahadi za waziri mkuu wa Israel kuhusu suala la makazi. Mjumbe wa kwanza wa mazungumzo wa Palestina Bw Saeb Erekat alisema kama Israel haitasimamisha kabisa ujenzi wa makazi kwenye ardhi yote iliyonyakuliwa na Israel, ahadi za Ehud Olmert hazina maana yoyote.

Tatu, Mpaka sasa nchi za Kiarabu ikiwa pamoja na Saudi Arabia hazijaamua kama zitashiriki kwenye mkutano huo, au la.

Idhaa ya kiswahili 2007-11-20