Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-21 19:10:02    
Mradi wa kuziunganisha China na Marekani kwa kebo ya kupeleka habari chini ya bahari waanza kujengwa

cri

Tetemeko kubwa la ardhi lililotokea mwishoni mwa mwaka 2006 kwenye bahari iliyo kusini ya Taiwan, China lilisababisha kebo 14 za kupeleka habari kukatika, tukio hilo lilikata njia nyingi za upashanaji habari kati ya China na nchi za Marekani, Ulaya na Asia ya kusini mashariki, hata huduma za mtandao wa Internet ziliathiriwa vibaya. Hivi karibuni makampuni matatu ya huduma za mtandao wa Internet ya China yaani China Netcom, China Telecom na China Unicom, yameshirikiana na makampuni ya huduma hiyo ya sehemu ya Taiwan ya China, Marekani na Korea ya Kusini katika kujenga kwa pamoja kebo ya kupeleka habari ya chini ya bahari kati ya China na Marekani. Baada ya kukamilika, mradi huo utainua kidhahiri uwezo wa mawasiliano ya kimataifa kwenye sehemu hizo na pia utatoa huduma za matangazo ya picha safi za televisheni kwa ajili ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008.

Tarehe 22 mwezi Oktoba, sherehe ya uzinduzi wa mradi wa kuunganisha China na Marekani kwa kebo ya kupeleka habari iliyoko chini ya bahari ilifanyika huko Qingdao, mji wa pwani ulioko kaskazini mwa China. Mradi huo unaitwa TPE kwa ufupi, katika kipindi chake cha kwanza, umepanga kuweka kebo yenye urefu wa kilomita laki 1.8 inayounganisha moja kwa moja China bara na Marekani. Kebo hiyo itaanzia mji wa Qingdao na wilaya ya Chongming ya mji wa Shanghai, na kufika pwani ya Nedonna ulioko kwenye mwambao wa magharibi wa Marekani.

Kebo hiyo itainua kwa mara 31 uwezo wa kebo inayotumika hivi sasa kwenye bahari ya Pasifiki. Kwa mujibu wa usanifu wake, kebo hiyo mpya itawezesha watu milioni 40 kupigiana simu kati ya China na Marekani kwa wakati mmoja.

Kipindi cha kwanza cha mradi huo kinatarajiwa kukamilika kabla ya kufunguliwa kwa michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka kesho. Wakati huo, kebo hiyo itainua kidhahiri upana wa njia ya upashanaji habari ya kuvuka bahari ya Pasifiki, na kukidhi mahitaji ya ongezeko la huduma za mtandao wa Internet, data na sauti kati ya sehemu za Asia na Marekani. Naibu meya wa mji wa Qingdao Bw. Wang Xiulin alisema, mwaka 2008 watu bilioni 5 duniani watatazama michezo ya Olimpiki ya Beijing kwa njia ya televisheni. Mradi wa kebo hiyo utakidhi mahitaji makubwa ya mawasiliano na upashanaji wa habari katika michezo hiyo. Bw. Wang Xiulin alisema:

"kebo hiyo itabeba wajibu wa kutoa huduma za upashanaji habari katika michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008 na maonesho ya kimataifa ya Shanghai mwaka 2010. Kukamilika kwa kebo hiyo kutainua kidhahiri upana wa njia ya kupeleka habari ya chini ya bahari ya Pasifiki, na kukidhi mahitaji mbalimbali ya njia pana ikiwemo huduma za matangazo ya picha bora ya televisheni ya michezo hiyo, na shughuli za kuonesha video kwenye mtandao wa Internet."

Kampuni ya China Netcom ikiwa ni mshiriki wa kiserikali wa upashanaji habari wa michezo ya Olimpiki ya Beijing, itatoa huduma za matangazo ya picha bora ya televisheni. Naibu maneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Zhao Jidong alisema,

"Naamini kuwa makampuni ya huduma za upashanaji habari ya China ikiwemo kampuni ya China Netcom yatatumia kikamilifu uwezo wa kebo hiyo, kuendelea kuinua thamani ya mradi huo, na kuahidi kutoa huduma bora na salama kabisa za mawasiliano ya kimataifa katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008, na kuitangaza China Netcom ikiwakilisha chapa ya huduma na sura ya makampuni maarufu ya upashanaji habari ya China katika soko la upashanaji habari duniani."

Mbali na kutoa huduma na uhakikisho wa mawasiliano katika michezo ya Olimpiki, ujenzi wa kebo hiyo pia utakamilisha zaidi mtandao wa upashanaji habari wa kimataifa wa China, kusaidia kuhakikisha usalama wa upashanaji habari wa kimataifa, na kuinua hadhi ya China katika eneo hilo. Naibu mkurugenzi wa idara ya usimamizi wa upashanaji habari katika wizara ya upashanaji habari ya China Bw. Wang Jianwen alisema:

"katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na maendeleo ya siasa, uchumi na mambo ya diplomasia ya China, shughuli za utoaji huduma za upashanaji habari wa kimataifa pia zimedumisha maendeleo ya kasi. Mradi wa kebo hiyo utakamilisha zaidi mtandao wa upashanaji habari wa China, kuinua uwezo wa upashanaji habari wa kimataifa wa China na kuinua kwa kiasi kikubwa kiwango cha usalama na kutegemeka kwa mtandao huo."

Kebo inayotumika hivi sasa kati ya China na Marekani inapita Japan na sehemu ya Taiwan ya China, hali hiyo inasababisha uchelewaji katika kupashana habari. Aidha, kutokana na uwezo usio wa kutosha na kutokea kwa maafa ya kimaumbile ikiwemo tetemeko la ardhi na dhoruba ya baharini, baadhi ya wakati mtandao huo haufanyi kazi vizuri, na hata unaweza kukatika.

Kuhusu hali hiyo, tarehe 18 mwezi Desemba mwaka jana, makampuni 6 ya upashanaji habari ya nchi 3 za China, Marekani na Korea ya kusini yalisaini makubaliano hapa Beijing kuwa yatatoa dola za kimarekani milioni 500 kwa pamoja kwa ajili ya kujenga kebo ya kwanza ya kupeleka habari ya moja kwa moja kati ya China na Marekani. Mkurugenzi wa bodi ya Kampuni ya TYCO ya Marekani ikiwa ni mmoja wa washiriki wa mradi, Bw. Mathlich Rusell alisema,

"mradi huo ukiwa ni kama mwujiza wa zama hizi, umewezesha nchi za China na Marekani kuwasiliana moja kwa moja, pia umejenga daraja jipya la mawasiliano kati ya nchi hizo mbili, umesukuma mbele uhusiano wa kibiashara wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili, kuimarisha uhusiano uliopo kati ya nchi mbili na kuweka msingi imara kwa ujenzi wa jamii yenye masikilizano."