Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-23 15:48:46    
Madaktari wa China hawataondoka kutokana na homa ya bonde la ufa

cri

Taarifa iliyotolewa tarehe 8 mwezi Novemba inasema, katika mwezi uliopita watu 228 walioambukizwa homa ya bonde la ufa waligunduliwa nchini Sudan, na watu 84 kati yao walikufa. Hospitali ambayo kikosi cha madaktari wa China kinafanya kazi, iko kwenye sehemu iliyokumbwa na homa ya bonde la ufa, lakini madaktari tisa wa kikosi hicho bado wanashikilia kuendelea na kazi zao, hawataondoka kutoka kwenye sehemu hiyo yenye hatari. Walipohojiwa na waandishi wa habari wa shirika la habari la Xinhua, China walisema, ingawa walikuwa na wasiwasi kuhusu hali ya homa ya bonde la ufa, lakini hivi sasa ni wakati ambapo wananchi wa Sudan wanawahitaji zaidi madaktari hao, na wakiwa madaktari wanapaswa kuonesha moyo wa kuhudumia wagonjwa, na kuwasaidia wakazi wa huko kuushinda ugonjwa.

Homa ya bonde la ufa inaenezwa zaidi kati ya ng'ombe na kondoo, pia inaambukiza watu kwa njia ya mbu na kukutana na wanyama walioambukizwa na virusi vya homa hiyo. Hivi sasa bado hakuna dawa maalumu inazoweza kutibu homa hiyo.

Bi. Liu Jing kila siku anakutana na wagonjwa wengi, na anakabiliana na tishio kubwa. Alisema hospitali hiyo tarehe 30 mwezi Oktoba ilipokea mgonjwa aliyekuwa anadhaniwa ameambukizwa virusi vya homa ya bonde la ufa. Kutokana na mazingira mabaya ya hospitali hiyo na hali mbaya ya mgonjwa huyo, mgonjwa huyo alikabidhiwa kwenye hospitali nyingine na kupoteza maisha yake. Mgonjwa wa pili aliyepokewa na hospitali ambaye pia alikuwa anadhaniwa kuambukizwa virusi vya homa ya bonde la ufa, pia alikufa baada ya muda mfupi. Hivi sasa hospitali hiyo imetenga sehemu fulani ili kupokea wagonjwa walioambukizwa virusi vya homa ya bonde la ufa na kuwapatia huduma za matibabu.

Mkuu wa hospitali aliwahi kuwauliza madaktari hao wa China, kama hali ya ugonjwa huo itazidi kuwa mbaya, madaktari hao wa China wataondoka kutoka kwenye hospitali hiyo au la? Madaktari hao wote walijibu kuwa hawataondoka kama hawatapokea amri ya kuondoka.

Madaktari hao tisa wa China waliwasili Sudan mwezi Agosti mwaka huu pamoja na kikundi kipya cha madaktari wa China. Ingawa si muda mrefu walipowasili nchini Sudan, lakini walimudu matatizo mengi ya kuwahudumia wagonjwa, na kusifiwa na wakazi wa huko.

Balozi wa China nchini Msumbiji Bw. Tian Guangfeng tarehe 19 huko Maputo, mji mkuu wa nchi hiyo alipohojiwa na waandishi wa habari wa shirika la habari la Xinhua, China alisema, mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika hapa Beijing mwaka jana ulileta kipindi kipya cha maendeleo ya uhusiano kati ya China na Msumbiji, katika mwaka mmoja uliopita, mawasiliano kati ya nchi hizo mbili yaliongezeka, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo uliimarishwa, na utaratibu wa ushirikiano pia unaendelezwa vizuri.

Bw. Tian Guangfeng alisema katika mwaka mmoja uliopita tangu mkutano wa wakuu wa nchi wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika ufanyike, shughuli za mawasiliano ya siasa ziliongezeka, hasa mwezi Februari mwaka huu ambapo rais Hu Jintao wa China alipofanya ziara nchini Msumbiji, nchi hizo mbili zilisaini makubaliano mengi kuhusu misaada ya kiuchumi na ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara. Bw. Tian Guangfeng alisema, katika miezi kadhaa iliyopita, ubalozi wa China nchini Msumbiji umepokea vikundi zaidi ya 30 vya ujumbe na uchunguzi. Hii ilionesha kuwa serikali ya China na makundi ya kiraia nchini China zote zinatilia maanani maendeleo ya uhusiano kati ya China na Msumbiji. Licha ya hayo, ujumbe wa Msumbiji uliofanya ziara nchini China uliongezeka. Kutembeleana kwa pande hizo mbili kumeimarisha uaminifu wa kisiasa kati ya pande hizo, na kuweka mazingira mazuri kwa nchi hizo mbili kufanya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara wa kunufaishana na usawa.

Bw. Tian Guangfeng alisema mradi wa kituo cha mfano wa ufundi wa kilimo unatekelezwa, kazi ya maandalizi ya ujenzi wa uwanja wa michezo wa taifa wa Msumbiji utakaojengwa kwa msaada wa China imekamilika, inatazamiwa kuwa ujenzi wa mradi huo utaanza mwanzoni mwa mwaka kesho, na kutumika kabla ya kombe la dunia la soka mwaka 2010. Nyumba 150 zenye bei nafuu pia zitajengwa kwa msaada wa serikali ya China. Miradi ya mikopo nafuu ya kiserikali inayoshughulikiwa na benki ya uagizaji na usafirishaji ya China vilevile inaendelezwa kwa utaratibu.

Bw. Tian Guangfeng alisema, hivi sasa hali ya siasa ya Msumbiji ni ya utulivu, uchumi wake unaendelezwa kwa kasi, na serikali ya nchi hiyo inashikilia sera ya kutafuta utulivu na maendeleo, hali hii imetoa fursa nyingi kwa China na Msumbiji kupanua ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati yao. Bw. Tian Guangfeng alizitaka kampuni za China zitumie fursa hii, kuharakisha uwekezaji kwenye nchi za nje, na kushiriki kwenye ujenzi wa uchumi wa Msumbiji.

Rais Mwai Kibaki wa Kenya tarehe 19 mjini Nairobi alikutana na naibu mwenyekiti wa kamati kuu ya kijeshi ya China ambaye pia ni mjumbe wa taifa na waziri wa ulinzi wa China Bw. Cao Gangchuan.

Rais Kibaki alimkaribisha Bw. Cao Gangchuan kuitembelea Kenya, alisema maendeleo ya uhusiano kati ya China na Kenya ni mazuri, ziara ya Rais Hu Jintao wa China nchini Kenya imesukuma mbele maendeleo ya uhusiano huo. Kenya ni rafiki mkubwa wa China daima dawamu, na inaifurahia China kuzisaidia Kenya na nchi nyingine za Afrika kupata maendeleo ya pamoja.

Bw. Cao Gangchuan aliwasilisha salamu za kila la heri za Rais Hu Jintao kwa Rais MwaiKibaki. Alisema tangu China na Kenya zianzishe uhusiano wa kibalozi miaka 44 iliyopita, uhusiano kati ya nchi hizo mbili unapata maendeleo siku hadi siku, na mawasiliano na ushirikiano kwenye sekta mbalimbali pia unaimarishwa. Bw Cao Gangchuan tarehe 19 huko Nairobi alifanya mazungumzo na waziri wa ulinzi wa Kenya Bw. Njenga Karume. Alisema uhusiano kati ya China na Kenya unaendelezwa vizuri tangu mwaka 1963 nchi hizo mbili zilipoanzisha uhusiano wa kibalozi, na katika miaka ya hivi karibuni mawasiliano kati ya majeshi ya nchi hizo mbili yameongezeka na ushirikiano kati ya pande hizo mbili unapanuka siku hadi siku. Pia alisema China siku zote inatilia maanani kuimarisha mawasiliano na ushirikiano na Kenya katika mambo ya kijeshi, na kupenda kushirikiana na Kenya kuimarisha na kupanua ushirikiano halisi kati ya majeshi ya nchi hizo mbili.

Bw. Karume alisema Kenya na China zina uhusiano wa kirafiki, viongozi wa nchi hizo mbili wanatembeleana mara kwa mara, na ushirikiano kati ya majeshi ya nchi hizo mbili umekuwa na mafanikio makubwa. Alisema Kenya inatilia maanani kuendeleza uhusiano na China, na ina matumaini ya kupanua ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Idhaa ya kiswahili 2007-11-23