Mikutano mbalimbali kati ya viongozi wa nchi za Asia ya mashariki ilifungwa tarehe 22 nchini Singapore. Waziri mkuu wa Singapore Bw. Lee Hsien Loong aliitisha Mkutano na waandishi wa habari akifanya majumuisho ya mikutano hiyo. Alisema mikutano mbalimbali kati ya viongozi wa nchi za Asia ya mashariki imepata mafanikio makubwa. Bw. Lee Hsien Loong alisema, kwenye mikutano hiyo viongozi wa nchi mbalimbali za Asia ya mashariki walisaini taarifa na mikataba kadha wa kadha, na mikutano hiyo imepata matunda kemkem. Alisema:
"Madhumuni yetu ni kuimarisha utandawazi wa uchumi wa Umoja wa Asia ya kusini mashariki, ambayo yanalingana pia na ushirikiano wa kikanda wa Asia. Kwenye mikutano hiyo tumepiga hatua kubwa, tumesaini "Katiba ya Umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki", na kupitisha "Mpango wa uchumi wa Umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki". Mikutano hiyo pia imeimarisha mawasiliano kati yetu na nchi washirika wetu".
Kwenye Mkutano wa 13 wa wakuu wa nchi za Umoja wa Asia ya kusini mashariki, "Katiba ya Umoja wa Asia ya kusini mashariki" imesainiwa bila matatizo, katiba hiyo ilijadiliwa mara kwa mara na nchi wanachama wa umoja huo katika miaka miwili iliyopita. Katiba hiyo imeweka bayana kwa mara ya kwanza malengo ya kimkakati ya umoja huo, na pia kuweka vifungu kadha wa kadha kuhusu malengo ya maendeleo ya Umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki, kanuni na hadhi ya umoja huo. Katiba hiyo pia imeweka kanuni mpya kuhusu uanzishaji wa mashirika kadha wa kadha ya Umoja wa Asia ya kusini mashariki na ajenda zinazohusika. Msemaji wa Mkutano huo Bw. Anderew Tan alizungumzia umuhimu wa katiba hiyo, akisema:
"Nchi 10 wanachama wa Umoja wa Asia ya kusini mashariki zimesaini katiba ya umoja huo, tukio hili limefungua ukurasa mpya wa Umoja wa Asia ya kusini mashariki. Katiba hiyo itauwezesha umoja huo uwe jumuiya yenye nguvu zaidi ya mshikamano, yenye ufanisi mkubwa zaidi na inayofuata msingi wa taratibu na kanuni zake".
Kwenye Mkutano huo, viongozi wa nchi 10 za Umoja wa Asia ya kusini mashariki pia walisaini "Mpango wa uchumi wa Umoja wa Asia ya kusini mashariki", mpango huo ni waraka wa uelekezaji kwa ujenzi wa utandawazi wa uchumi wa umoja huo. Kutokana na mpango huo, ifikapo mwaka 2015, soko la pamoja na vituo vya pamoja vya uzalishaji vitaanzishwa kwenye sehemu ya nchi za Umoja wa Asia ya kusini mashariki, ambapo nchi za sehemu hiyo zitatimiza mzunguko huria wa bidhaa, huduma, uwekezaji na wafanyakazi, pamoja na mawasiliano huria ya mitaji kati ya nchi wanachama. Kwa kuwa nchi za umoja huo zina viwango tofauti vya maendeleo, hivyo "Mpango wa uchumi wa Umoja wa nchi za Asia ya kusini mashariki" pia umeonesha unyumbufu wa lazima wakati wa kuhimiza utandawazi wa uchumi wa umoja huo
Aidha, kwenye Mkutano huo waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao na nchi za Umoja wa Asia ya kusini mashariki pamoja na Japan, Korea ya kusini, India, Australia, New Zealand walisaini "Taarifa ya Singapore" kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, nishati na uhifadhi wa mazingira. Taarifa hiyo imeeleza nia ya kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, mambo ya nishati na uhifadhi wa mazingira.
Bw. Lee Hsien Loong alisema, viongozi wa nchi mbalimbali wameahidi kutekeleza majukumu na wajibu wao ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Alisema:
"Tumejadili vilivyo kuhusu masuala ya nishati, mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa, na nchi mbalimbali zilizohudhuria Mkutano zote zimeahidi kufanya juhudi za aina mbalimbali ili kutatua masuala ya nishati, mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa".
Waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao alitoa hotuba kwenye Mkutano wa 3 wa viongozi wa nchi za Umoja wa Asia ya kusini mashariki akidhihirisha kuwa, serikali ya China itafuata wazo la kujiendeleza kwa njia ya kisayansi kwenye mambo ya utawala wake, na imechukua sera na hatua mbalimbali na kupata maendeleo makubwa. Alisisitiza kuwa China itafuata mikataba na makubaliano na kubeba wajibu na majukumu yake inayostahili kuyabeba duniani.
|