Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-26 15:37:49    
Tamasha la nane la michezo ya sanaa lachangia ustawi wa utamaduni nchini China

cri

Tamasha la nane la michezo ya sanaa la China linalofanyika kwa siku 16, linaendelea mjini Wuhan, mji mkuu wa mkoa wa Hubei. Kaulimbiu ya tamasha hilo ni "kustawisha utamaduni wa kisasa na kujenga jamii yenye masikilizano ya kiutamaduni". Wakati wa siku za tamasha hilo tuzo kubwa ya michezo ya sanaa itatolewa, licha ya michezo ya sanaa pia kulikuwa na makongamano na shughuli za kutangaza miradi ya utamaduni. Tamasha hili ni mchango mkubwa katika kustawisha utamaduni wa China.

Tamasha la nane la michezo ya sanaa la China lilifunguliwa tarehe 5 jioni, hilo ni tamasha kubwa kabisa kuliko matamasha yote yaliyopita, licha ya kufanyika mjini Wuhan pia kuna matamasha mengine yanayofanyika kwa wakati mmoja katika miji sita mkoani humo.

Wakati wa tamasha hilo watazamaji zaidi ya elfu kumi kutoka nchini China na nchi za nje walifurahia michezo ya sanaa zaidi ya mia moja. Naibu katibu mkuu wa tamasha hilo ambaye pia ni mkuu wa idara ya utamaduni ya mkoa wa Hubei Bw. Du Jianguo alifahamisha kuwa michezo inayoshiriki kwenye tamasha hilo ilionesha wazi mafanikio makubwa ya utamaduni yaliyopatikana katika miaka ya karibuni.

"Michezo yote inayooneshwa kwenye tamasha hilo inatoka kwenye mashindano ya sanaa za aina mbamalimbali kote nchini China, kwa hiyo inawakilisha kiwango cha juu kabisa cha usanii na mafanikio mapya katika sanaa za jukwaani. Michezo hiyo licha ya kuwa na maudhui mazuri, pia inakwenda na wakati na inatia moyo wa maendeleo. Na baadhi ya michezo inachezwa kwa kuunganisha sanaa ya jukwaani pamoja na teknolojia ya kisasa, ambayo ina nguvu kubwa zaidi ya kuwavutia watazamaji, kwa hiyo ni michezo inayoonesha kiwango cha juu zaidi cha tamasha hili la taifa la China."

Kaulimbiu ya tamasha hili ni "Kustawisha utamaduni wa kisasa na kujenga jamii ya masikilizano ya kiutamaduni". Katika tamasha hilo michezo iliyotungwa na makundi 54 itagombea Tuzo ya "Wen Hua" ambayo ni ya ngazi ya juu kabisa katika michezo ya jukwaani nchini China na Tuzo ya "Nyota" iliyotolewa katika mashindano ya michezo ya dansi, opera, picha za kuchorwa na sanaa ya maandiko ya Kichina. Makundi ya wasanii kutoka nchi za nje pia yataonesha michezo yao ya kiwango cha juu. Zaidi ya hayo, makongamano ya kuendeleza uvumbuzi wa aina mpya za utamaduni, na maonesho ya vitu vya kale vya sanaa pia yalifanyika.

Tokea mwaka 1987 tamasha kama hilo limewahi kufanyika katika mji wa Beijing, mikoa ya Yunnan, Gansu, Sichuan, Jiangsu, Zhejiang, na lilitoa fursa kwa wasanii kuonesha uhodari wao, pia lilihimiza ujenzi wa miundombinu ya utamaduni. Ili tamasha la sanaa liweze kufanyika majumba mengi ya michezo ya sanaa na vituo vya utamaduni vimejengwa katika sehemu mbalimbali. Wasanii vijana na wazee walushirikiana katika utunzi kwa kuunganisha utamaduni wa jadi na wa kisasa, na kuifanya michezo iambatane na maisha na kwenda na wakati.

Mkuu wa kitengo cha sanaa katika Wizara ya Utamaduni ya China Bw. Yu Ping aliwahi kushiriki mara nyingi kwenye maandalizi ya matamasha ya utamaduni, anaona kuwa tamasha la sanaa la China litakuwa na nguvu kubwa zaidi ya kuhimiza maendeleo ya utamaduni wa China. Alisema,

"Ni kweli kwamba kwa kufanya tamasha la sita, saba na la nane, ujenzi wa majumba ya michezo ya sanaa umestawi kwa kiasi kikubwa, na utunzi wa michezo ya sanaa pia umepewa kipaumbele. Tuna uhakika kwamba mkoa wa Hubei utakuwa na maendeleo ya haraka katika siku za baadaye."

Tamasha la michezo ya sanaa la taifa linaloandaliwa na Wizara ya Utamaduni ya China ni kubwa na la ngazi ya juu kabisa nchini China. Tamasha hilo linafanyika kila baada ya miaka mitatu. Tamasha linalofanyika sasa litamalizika tarehe 20, na tamasha lifuatalo litafanyika mwaka 2010 huko Guangzhou, mji wa kusini mwa China.

Idhaa ya kiswahili 2007-11-26