Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-26 15:45:08    
Kubeba lawama badala ya mwenye makosa

cri

"Kubeba lawama badala ya mwingine mwenye makosa" ni moja ya mbinu 36 za kivita katika China ya kale. Mbinu hiyo ilitokana na hadithi moja inayoeleza kuwa, hapo kale kulikuwa na familia moja ambayo ilikuwa ni tajiri sana, hata ndugu wote watano wa familia hiyo walikuwa ni maofisa wakubwa wakubwa, na kila mmoja akiwa safarini alikuwa analindwa na askari wengi. Lakini baadaye bahati mbaya mmoja kati yao alikumbwa na matatizo, wakati huo ndugu wenzake wanne wote hawakujitokeza kumsaidia. Kwenye mwisho wa hadithi mwandishi alisema binadamu ni lazima kupendana na kusaidiana sembuse ndugu wa tumbo moja. Baadaye hadithi hiyo ilijumuishwa kwenye mbinu 36 za kivita na kuitwa "Kubeba lawama badala ya mwenye makosa".

Mbinu hiyo inapotumika katika vita inamaanisha kuwa kama kwenye mapambano maadui wakiwa na nguvu kubwa, basi hi lazima tutapata hasara, kwa hiyo ni lazima tujaribu kukwepa hasara kubwa na kujaribu kupata ushindi kwa kupata hasara kidogo. Mbinu hiyo ilitumika mara nyingi katika mapambano ya kijeshi na ya kisiasa katika China ya kale.

Katika karne ya tatu K.K. dola la Zhao lilipakana na kabila la Xiongnu kwa upande wa kaskazini, mara kwa mara askari wa kabila hilo walikuwa wanawasumbua wakazi wa mpakani. Mfalme wa dola la Zhao alimtuma jemadari Li Mu kwenda kwenye mji wa Yanmen, mji uliopo mpakani. Mwanzoni jemadari huyo aliwaamrisha askari wake watulie ndani ya mji bila kuruhusiwa kutoka nje kupambana na maadui. Jeshi la kabila la Xiongnu halikuthubutu kufanya lolote kabla ya kufahamu nguvu halisi ya Li Mu. Kwa kutumia muda huo Li Mu aliimarisha nguvu na kufundisha askari wake. Baada ya maandalizi ya miaka kadhaa, nguvu ilikuwa imeimarika na askari wamekuwa hodari na tayari kupambana na maadui. Kabla ya kulishambulia kabila la Xiongnu, Li Mu alituma askari wachache wakifuatana na raia kutoka mjini kupeleka mifugo malishoni. Askari wa Xiongnu walipoona askari wachache walifanya ujambazi bila hofu yoyote, askari wa Li Mu walijaribu kupambana na askari wa Xiongnu na walijidai kushindwa, wakaacha mifugo na kukimbia. Askari wa Xiongnu wakarudi na ushindi mkubwa. Kamanda wa kabila la Xiongnu aliona kwamba kumbe Li Mu pia ni jemadari mwoga, hii ndio sababu yao ya kutothubutu kutoka mjini na kupambana nao. Kutokana na fikra hiyo akaanza kufanya mashambulizi ya kijeuri. Li Mu alipoona mbinu yake imemdanganya kamanda huyo, alipanga vikosi vyake kuficha kwenye njia watakayopitia askari wa jeshi la Xiongnu huku aliwatuma baadhi ya askari kuwavutia askari wa Xiongnu kwenye njia waliyoficha askari wa Li Mu, na kuwavamia maadui katika vikundi vikundi na kukiangamiza kikundi kimoja baada ya kingine. Jeshi la Xiongnu lilishindwa vibaya, sehemu ya mpakani ilikuwa salama.

Na katika ushindani wa biashara, ili kupata ushindi wa muda mrefu, wakati fulani kampuni inalazimika kupata hasara ya muda. Kwa mfano, kampuni ya Bausch & Lomb ya Makerani inayotengeneza lensi za kubandika kwenye mboni za macho, iliwahi kutumia mbinu hiyo ya "kubeba lawama badala ya mwenye makosa". Mwaka 1981, Bw. Daniel Jill alikuwa ni mkuu wa kampuni hiyo. Wakati huo kwa sababu teknolojia ya kampuni hiyo ilikuwa nyuma, uwezo wa ushindani ulikuwa mdogo. Kutokana na hali hiyo mkuu huyo aliamua kufunga na kuuza viwanda vyote vya kampuni hiyo isipokuwa kiwanda kimoja cha kutengenezea lensi za kubandika kwenye mboni za macho, kutumia fedha alizopata kutoka mauzo ya viwanda kugeuza teknolojia na kubadilisha zana za uzalishaji. Kwa kufanya hivyo alihakikisha nafasi ya kuongoza katika utengenezaji wa bidhaa yake. Mwanzoni uamuzi wake ulikuwa haueleweki kwa watu wengi kutokana na kufungwa kwa viwanda, kupunguza wafanyakazi na kupata faida kidogo. Lakini baadaye hali nzuri ya soko ilithibitisha kuwa uamuzi wake ulikuwa ni sahihi. Bidhaa za Bausch & Lomb imekuwa chapa maarufu, na baadaye ilivumbua dawa ya macho na vifaa vya upasuaji wa macho. Hivi sasa kampuni ya Bausch & Lomb imekuwa kubwa duniani.

Bila shaka mbinu hiyo ni lazima itumike kwa makini, kwani ukikosea utajiangamiza.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-06