Mkutano wa 36 wa wakuu wa Jumuiya ya Madola ulifungwa tarehe 25 huko Kampala nchini Uganda. Taarifa ya Kampala iliyotolewa kwenye mkutano huo wa siku tatu imesistiza kulinda amani ya dunia, kusukuma mbele maendeleo ya demokrasia na uchumi, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, kufuatilia maendeleo ya vijana na kuhimiza maendeleo ya shughuli mbalimbali za elimu, afya na nyinginezo.
Malkia Elizabeth II wa Uingereza, katibu mkuu wa Jumuiya ya Madola na viongozi wengine au wawakilishi wao wa nchi 48 kati ya nchi 53 wanachama wa jumuiya hiyo, walihudhuria mkutano huo uliofunguliwa tarehe 23. Kauli mbiu ya mkutano huo ilikuwa "nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kupata maendeleo ya siasa, uchumi na binadamu kwa kupitia mageuzi ya jamii". Mkutano huo pia ulizitaka nchi zinazoendelea za jumuiya hiyo zitimize mageuzi ya jamii kwa kufanya marekebisho ya kiuchumi, yaani kubadilika kuwa jamii inayozichukulia shughuli za viwanda na huduma kuwa kazi kuu ya uchumi kutoka jamii inayotegemea kazi kuu ya kilimo.
Kutokana na hali ilivyo nchini Pakistan, uanachama wa nchi hiyo kwenye Jumuiya ya Madola ulifuatiliwa kwenye mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Madola. Usiku kabla ya kufunguliwa kwa mkutano huo, Jumuiya ya Madola ilitangaza kuisimamisha Pakistan uanachama. Hii inamaanisha kuwa kabla ya kurejeshwa uanachama, Pakistan haitaruhusiwa kuhudhuria mkutano wowote wa Jumuiya Madola, wala kupata misaada inayotolewa na jumuiya hiyo. Lakini wachambuzi wanaeleza kuwa baada ya maendeleo ya miaka zaidi ya 70, Jumuiya ya Madola imekuwa jumuiya inayofanya mazungumzo na ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi, na haina mpangilio na uhusiano mkubwa kama ilivyokuwa zamani, hivyo kusimamisha uanachama wa Pakistan ni kama kuonesha ishara fulani.
Kuhusu suala la mabadiliko ya hali ya hewa, muda wa Makubaliano ya Kyoto yaliyosainiwa mwaka 1997 kwa ajili ya kudhibiti utoaji wa hewa zinazosababisha kuongezeka kwa joto utamalizika mwaka 2012, na ili kujadili makubaliano mapya, mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu suala la mabadiliko ya hali ya hewa utafanyika mwanzoni mwa mwezi Desemba kwenye kisiwa cha Bali nchini Indonesia. Je, Jumuiya ya Madola yenye nchi 53 wanachama na theluthi moja ya idadi ya watu duniani itafanya kazi gani katika suala la mabadiliko ya hali ya hewa? Na mkutano wa wakuu wa jumuiya hiyo utapata mafanikio gani kuhusu suala hilo? Hayo yamefuatiliwa sana na watu.
Kwenye mkutano huo, nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola ziliahidi kuwa, zitadumisha msimamo mmoja katika suala la mabadiliko ya hali ya hewa. Mkutano huo pia ulipitisha mpango wa Ziwa Victoria wa Jumuiya ya Madola kuhusu hatua za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, ili kuzidisha ushirikiano wa kati ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuhusu suala la hilo. Mpango huo ulisisitiza kuwa nchi hizo zina majukumu ya pamoja, lakini yenye tofauti, katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, majukumu hayo yanapaswa kugawanyika kwa haki na kwa mujibu wa uwezo na kiwango cha maendeleo cha nchi tofauti, na hayapaswi kuzidisha umaskini kwa nchi zinazoendelea, na nchi zilizoendelea zinapaswa kufanya kazi ya mfano katika juhudi za kukabiliana na suala hilo. Inasemekana kuwa nchi kadhaa wanachama wa Jumuiya ya Madola zilitaka kutoa taarifa yenye nguvu zaidi kabla ya mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu suala hilo kufanyika, lakini katibu mkuu wa jumuiya hiyo Bw. Donald McKinnon alisema Mpango wa Ziwa Victoria uliofikiwa na nchi 53 wanachama wa jumuiya hiyo, unaonesha nia ya pamoja, na ina maana muhimu. Hivyo katika kukabiliana na suala la mabadiliko ya hali ya hewa, hivi sasa Jumuiya ya Madola haitachukua hatua nyingine.
Aidha kusaidia nchi ndogo zinazoendelea za jumuiya ya Madola kujiendeleza, na hali ya vijana wanaochukua nusu ya idadi ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo pia imejadiliwa sana kwenye mkutano huo. Mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Madola unafanyika kila baada ya mwaka mmoja, na mkutano ujao utafanyika huko Port of Spain nchini Trinidad and Tobago mwaka 2009.
Idhaa ya kiswahili 2007-11-26
|