Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-26 19:19:00    
Nyani aina ya De Brazza wanakabiliwa na hatari ya kutoweka

cri

Kuna aina nyingi za nyani duniani, tofauti zao zinatokana na tabia, ukubwa, rangi na hata maisha. Wanasayansi wamewagawanya nyani katika makundi mawili makubwa. Moja ni lile la Nyani wa dunia ya zamani na lingine ni la nyani wa dunia mpya.

Nyani aina ya De Brazza ambao wanakabiliwa na tishio la kutoweka, wapo katika kundi la nyani wa dunia ya zamani, na wanaweza kutoweka kama juhudi za kuwalinda hazijafanyika.

Nyani wa aina hii wako katika kundi la aina nyingine 25 za nyani ambao huenda wakawa historia tu kutokana na mabadiliko ya hali ya hali ya hewa yanayotishia maisha yao.

Kwa wakati mmoja nyani hawa walionekana katika eneo kame la kaskazini mwa Kenya,.

Kwa kawaida De Brazza hupenda mazingira baridi, kando kando ya mito au kwenye misitu mikubwa.

Dkt. Leakey ambaye ni mtafiti mashuhuri nchini Kenya anasema huenda nyani hao walitoka katika misitu ya magharibi mwa Kenya. Lakini hili swala linatakiwa kufanyiwa utafiti zaidi kwani linahusiana na mabadiliko ya hali ya hewa. Katika historia Nyani hawapendi eneo la bonde la ufa nchini Kenya.

Lakini baada ya utafiti wa kina katika milima ya Mathews eneo la Samburu nchini Kenya, takriban nyani 162 walipatikana wakiwa katika makundi 24.

Watafiti wanasema walianza kuona nyani hao katika eneo la Olkaela lililoko kwenye mwinuko wa mita 1, 203 kutoka usawa wa bahari.

Kupatikana kwa nyani hao kumeongeza idadi yao kwa asilimia 16% ya idadi iliyopo sasa nchini Kenya ambayo inafikia 1,000. Utafiti huo uliongozwa na bwana Iregi Mwenja wa mradi wa kulinda nyani katika eneo la Samburu, Kenya. Sehemu kubwa ya nyani hao walipatikana katika maeneo ya katikati ya mlima.

Inakadiriwa kuwa kuna kati ya nyani 200-300, hii ni kutokana na habari zilizokusanywa kwa wakazi wa eneo hilo pamoja na uchunguzi.

Ingawa shughuli za binadamu hazihatarishi sana maisha ya nyani kwa jumla, wale wanaoathirika sana ni hawa wa aina ya De Brazza.

Makazi ya nyani hawa yalioathiriwa zaidi ni yale yanaokaliwa na watu wa nyanda za chini. Majira ya kiangazi huchangia sana kuharibiwa kwa mazingira wanayoishi De Brazza.

Hii ni kwa sababu ukame unapotokea wakazi wa huko, huvamia maeneo yenye majani mengi ili kulisha mifugo yao. Wakazi wanasema kwenye maeneo hayo kuna miti yenye majani mengi ambayo haikauki, ambayo pia ni lishe bora kwa nyani hawa.

Kutoweka kwa nyani hawa kutachangiwa sana na uharibifu wa misitu.

Nchini Kenya na haswa katika maeneo wanakoishi nyani hawa kuna miti mizuri ya mbao.

Hivyo basi Binadamu wameendelea kutumia misitu hiyo kwa kiwango cha juu ili kutosheleza mahitaji yao ya ujenzi na kuni.

Kwenye sehemu nyingine barani Afrika nyani hawa hupatikana kwenye maeneo ya mito nchini Congo, Cameroon, Guinea ya Ikweta na Angola.

Idadi kubwa ya nyani aina ya De Brazza inapatikana Afrika ya kati.

Nyani aina ya De Brazza jike huishi na mama yake maisha yake yote huku madume wakiwaacha mama zao baada ya kukua.

Nyani hawa huwindwa sana na chui, mwewe wakubwa na nyoka.

Kinyume na jamii nyingine za nyani, nyani aina ya De Brazza hawaishi kwa makundi wala kuwasiliana kwa milio fulani. Ili kujiepusha na maadui hao De Brazza's hujikinga kwa kupanda juu ya miti au kujificha kwenye majabali.

Wao hula majani, wadudu, maua, Mijusi, na nafaka. Nyani hawa hawapendi kujumuika na wanyama wengine mwituni.

Nyani dume wa De Brazza wanafikia uzito wa kilo 7.8 na majike wanafikisha uzito wa kilo 4.5.

Asilimia ndogo ya nyani hawa iliyoko nchini Kenya inafaa kutunzwa na kuyalinda mazingira yao ili wasitoweke.

Aidha wawindaji haramu wanatakiwa kukomeshwa ili kuwanusuru viumbe hawa. Mabadiliko ya hali ya hewa yamesababisha kuongezeka kwa joto.

Kwa mfano theluji ya mlima Kenya inaendelea kuyeyuka kwa kiwango cha juu kufuatuia ongezeko la joto.

Karibu asilimia 92% ya theluji imeyeyuka kwa muda wa miaka 100 iliyopita. Wanasayansi wanasema kuwa barafu ya Mlima Kilimanjaro ambao ndio mrefu zaidi Barani Afrika huenda ikaisha ifikapo mwaka wa 2020. Asilimia 82% ya barafu kwenye mlima huo imeyeyuka tangu mwaka wa 1912.

Katika milima ya Ruwenzori nchini Uganda barafu ilianza kupungua tangu miaka ya tisini.

Kupungua kwa theluji kunaashiria ongezeko la joto, na pia ni pigo kubwa kwa mazingira na maisha ya viumbe.