Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-27 16:34:44    
Bw. Pervez Musharraf atakuwa rais wa Pakistan

cri

Mwendeshaji mkuu wa mahakama ya Pakistan Bw Malik Muhammad Qayyum tarehe 26 alisema, rais wa sasa Pervez Musharraf tarehe 29 atajiuzulu wadhifa wake wa jenerali na kuwa rais wa kiraia katika kipindi kipya cha miaka mitano. Bw. Malik Muhammad Qayyum alisema, sherehe ya kuapishwa kwa Pervez Musharraf itafanyika katika ikulu mjini Islamabad, jaji mkuu mpya wa nchi hiyo Bw. Abdul Hammed Dogar atashiriki kwenye sherehe hiyo.

Mahakama kuu ya Pakistan iliyoshirikisha majaji 10, tarehe 20 ilibatilisha kesi dhidi ya Pervez Musharraf kuendelea na wadhifa wake wa urais na tarehe 23 ilitoa hukumu kuwa, Bw. Musharraf alikuwa na haki ya kugombea urais. Tarehe 24 tume ya uchaguzi ilithibitisha kuwa Bw. Pervez Musharraf ameshinda katika uchaguzi uliofanyika tarehe 6 Oktoba na kuanza kipindi chake kipya cha miaka mitano.

Tarehe 2 Oktoba wagombea wawili wa urais walitoa mashitaka wakisema Bw. Pervez Musharraf hakustahiki kushiriki kwenye uchaguzi wa urais akiwa jenerali, na kutaka uchaguzi uahirishwe. Mahakama kuu ya Pakistan tarehe 5 Oktoba ilitoa uamuzi kwamba uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa. Kwa mujibu wa habari, Bw. Pervez Musharraf ameshinda katika uchaguzi wa urais uliofanyika tarehe 6 Oktoba.

Sambamba na ushindi wa Bw. Pervez Musharraf, vyama mbalimbali vya upinzani nchini Pakistan vimeanza kugombea nafasi za utawala. Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa na tume ya uchaguzi kuhusu uchaguzi wa bunge wa mikoa, tarehe 26 ni siku ya mwisho ya kuwasilisha maombi ya wagombeaji wa bunge la mikoa. Waziri Mkuu wa zamani ambaye pia ni mwenyekiti wa chama kikubwa cha upinzani cha Pakistan, Chama cha Umma, Bi. Benazir Bhutto katika siku hiyo nyumbani kwake mjini Larkana aliwasilisha ombi lake la kutaka kushiriki kwenye uchaguzi wa bunge la mikoa. Lakini alisema pia kuna uwezekano kwa Chama cha Umma kujiondoa kutoka uchaguzi ili kuonesha upinzani dhidi ya hali ya hatari iliyotangazwa na Pervez Musharraf.

Wakati huo huo waziri mkuu mwinginewa zamani, ambaye ni kiongozi wa chama kingine cha upinzani Bw. Nawaz Shariff tarehe 26 pia aliwasilisha ombi lake la kutaka kushiriki kwenye uchaguzi wa bunge. Bw. Nawaz Shariff aliwahi kuwa waziri mkuu wa Pakistan mara mbili. Mwezi Oktoba mwaka 1999 Bw. Pervez Musharraf aliyekuwa mkuu wa jeshi la Pakistan aliupindua utawala wa Pakistan, Bw. Nawaz Sheriff aliyekuwa waziri mkuu wakati huo alikamatwa. Mwaka wa pili, Nawaz Sheriff pamoja na ndugu yake walihamia uhamishoni nchini Saudi Arabia. Tarehe 10 Oktoba mwaka huu Bw. Nawaz Shariff alipofika kwenye uwanja wa ndege wa Islamabad kutoka London alifukuzwa na serikali ya Pakistan. Tarehe 25 Novemba Bw. Sheriff alirudi nchini Pakistan na kufika kwenye mji wa Lahore kutoka Saudi Arabia. Bi. Benazir Bhutto alionesha kukaribisha kurudi nchi Pakistan kwa Bw. Sheriff. Alisema kurudi nchini kwa Bw. Sheriff ni jambo zuri ambalo linaweza kuchangamsha hali ya siasa nchini humo.

Katika siku hiyo, mwenyekiti wa chama cha Pakistan Muslim League Bw. Chaudhry Shujaat Hussain pia aliwasilisha ombi la kutaka kushiriki kwenye uchaguzi wa bunge la mikoa. Alipozungumza na waandishi wa habari alisema anafurahia kurudi nchini kwa Bibi Benazir Bhutto na Bw. Sheriff, alisema watasaidia kusukuma mbele mchakato wa demokrasia nchini Pakistan.

Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi wa bunge la mikoa, uchaguzi utafanyika tarehe 8 Januari mwaka kesho. Hivi sasa Bw. Musharraf tayari amekuwa rais, lakini athari ya Bi. Benazir Bhutto na Bw. Sheriff kwenye ulingo wa siasa pia ni kubwa. Ingawa Bi. Bhutto aliwahi kusema ataacha kugombea uchaguzi wa bunge, lakini pia amewasilisha ombi lake, mabadiliko hayo ya msimamo yanastahili kuzingatiwa. Zaidi ya hayo mwezi Septemba Bw. Sheriff alipofika tu nchini mara alifukuzwa, lakini safari hii alirudi nchini bila tatizo lolote, mabadiliko hayo ya msimamo wa serikali pia yanastahili kufuatiliwa. Vyombo vya habari vinaona kuwa kadiri siku ya uchaguzi wa bunge la mikoa inavyokaribia, mvutano kati ya watu hao watatu utaendelea kuwepo.

Idhaa ya kiswahili 2007-11-27