Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-05 15:12:05    
Kabila la Washui mkoani Guizhou, China

cri

Miongoni mwa makabila mbalimbali nchini China, watu wa kabila la Washui wanaoishi kwenye mkoa wa Guizhou, kusini magharibi mwa China wana lugha yao na maandishi ya lugha, makabila kama hilo ni machache nchini China.

Wapendwa wasikilizaji, mliousikia ni wimbo wa kabila la Washui ambao ni wa kutakiana heri wakati wa kunywa pombe. Watu wa kabila hilo ni wachangamfu na wakarimu, wanapowakaribisha wageni waliotoka sehemu ya mbali, wanaandaa pombe hata kabla ya wageni hao kuingia kijijini. Wilaya inayojiendesha ya kabila la Washui ya Sandu mkoani Guizhou ni wilaya pekee ya kabila hilo nchini China. Wilaya hiyo sasa ni sehemu maarufu ya utalii mkoani Guizhou kutokana na kuwa na historia ndefu, utamaduni maalumu na mandhari nzuri ya kimaumbile. Mwaka 2006, kijiji cha Shuige cha wilaya hiyo kilichaguliwa kuwa moja kati ya vijiji vya majaribio ya ujenzi wa vijiji vya aina mpya mkoani Guizhou, ambapo shughuli za utalii hasa zinatiliwa mkazo katika kijiji hicho. Ofisa wa serikali ya sehemu hiyo Bibi Hu Xueli alisema, hivi sasa mabadiliko makubwa yametokea kwenye kijiji cha Shuige, alisema,

"Serikali ya wilaya ya Sandu ilianza kuendeleza shughuli za utalii kwenye kijiji cha Shuige mwaka 2005. Sasa miaka mitatu imepita, na mabadiliko makubwa yametokea kwenye kijiji hicho, mabadiliko hayo ni ya pande mbalimbali kuhusu uzalishaji, desturi, demokrasia, mazingira na hasa maisha ya wanakijiji, ambapo nyumba nzuri zimejengwa. Baada ya kuendeleza shughuli za utalii, serikali ya wilaya pia imewasaidia wanakijiji kuboresha maisha kwa kurekebisha miundo mbinu ya utoaji maji na umeme. Mwaka jana mapato ya mwanakijiji wa Shuige kwa wastani yalifikia yuan 1883. Baada ya kuendeleza shughuli za utalii, wageni wanaotembelea kijiji cha Shuige wameongezeka, ambapo mapato ya wanakijiji pia yameongezeka."

Bibi Hu Xueli alisema shughuli za utalii zimekifanya kijiji cha Shuige kijulikane siku hadi siku, vitu vyenye umaalumu wa kabila la Washui kama vile nyumba zilizojengwa kwa mbao, mashamba ya matuta, maandishi ya hieroglifu, nyimbo nzuri za kabila la Washui, vitambaa vilivyotiwa nakshi kwa kutumia manyoya ya mkia wa farasi, vinawavutia sana watalii. Kwa upande wa wakulima wanaoishi kwenye kijiji hicho, kufanya mawasiliano na wageni hao kumepanua upeo wao, na kuwafanya waanze kujua sehemu za nje. Wanakijiji hao walitambua kuwa mila na desturi zao ndizo zinazowavutia watalii wengi, hivyo mila na desturi zile zilizowahi kusahauliwa sasa zimekuwa na nguvu mpya ya uhai.

Maendeleo ya shughuli za utalii yamewahimiza wakazi wa kijiji cha Shuige walinde mila na desturi zao, watoto wanajifunza ufundi wa sanaa kutoka kwa wazazi wao, hata shule ya kijiji hicho kimeanza kufundisha wanafunzi ufundi huo wa kutia nakshi vitambaa kwa kutumia manyoya ya mkia wa farasi. Baadhi ya wanakijiji waliokwenda mijini kufanya vibarua wanarudi nyumbani, na wanapiga muziki na kucheza ngoma kama wanavyofanya wakati wa sikukuu kwa ajili ya wageni kutoka nchini na nchi za nje. Bw. Wu Hongzhuan ni mmoja kati ya wachezaji wa kikundi cha kuwakaribisha wageni cha kijiji cha Shuige, alisema,

"Kikundi cha kuwakaribisha wageni cha kijiji chetu kina wachezaji zaidi ya 50, tunafanya michezo kwa mara tatu hadi tano kila wiki. Sasa tumekuwa wakulima wasanii."

Bw. Wu Hongzhuan alisema, mila na desturi zinahimizana na shughuli za utalii, zimeboresha maisha ya wakazi wa kijiji hicho na kuwaletea burudani. Shughuli za utalii zimejaza furaha kwa wanakijiji wa Shuige. Alisema watu wa makabila madogo madogo wanaishuruku serikali kuwasaidia kupata maisha bora.

Mafanikio ya kijiji cha Shuige yanatokana na juhudi za serikali ya Guizhou za kuhimiza shughuli za utalii na kulinda utamaduni wa makabila madogo madogo. Chini ya uongozi wa serikali ya China katika ngazi mbalimbali, vijiji vya makabila madogo madogo mkoani Guizhou vilipata njia za kujiendeleza kutokana na umaalumu wao. Naibu katibu wa kamati ya chama ya mkoa wa Guizhou Bw. Wang Fuyu alisema, sehemu za makabila madogo madogo mkoani humo zimeendeleza shughuli za utalii kwa kutegemea umaalumu wao tofauti, njia hiyo haiendelezi uchumi tu, bali pia imelinda utamaduni wa makabila hayo. Alisema,

"Kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira, mkoa wa Guizhou umeendeleza shughuli za utalii kwenye vijiji vya makabila madogo madogo kwa kutegemea mandhari nzuri na mila za asili. Mwaka 2006 watalii waliotembelea mkoa huo waliongezeka kwa asilimia 40, na wakulima wamenufaika sana na ongezeko hilo la watalii. Mapato kutokana na shughuli za utalii mkoani Guizhou yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 kwa miaka mitatu mfululizo."

Kijiji cha Shuige sasa kimekuwa mfano mzuri wa shughuli za utalii zinazowanufaisha wakazi mkoani Guizhou. Familia zote za wanakijiji wa Shuige zimejenga nyumba mpya, wazee wanaishi maisha mazuri, watoto wanakua kwa furaha, na maisha ya wanakijiji wote yameboreshwa sana. Kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Oktoba mwaka huu, kijiji hicho kiliwapokea watalii zaidi ya laki moja, na mapato yaliyotokana na shughuli za utalii yalifikia yuan milioni mbili. Mwanakijiji wa Shuige Bw. Meng Zekun alisema,

"Kabla ya kuanza kwa shughuli za utalii, nilikuwa mjini kufanya kazi za vibarua, na niliweza kupata mapato ya yuan elfu moja tu kwa mwezi. Sasa ninafanya kazi za utalii nyumbani, na mapato yangu yameongezeka kuwa yuan zaidi ya elfu mbili."

Idhaa ya kiswahili 2007-12-05