Shirika la maendeleo na mipango la Umoja wa Mataifa tarehe 27 lilitoa mwito wa kuzitaka nchi mbalimbali duniani zichukue hatua za dharura, ili kukabiliana kwa pamoja na suala la kuongezeka kwa joto duniani, kwani suala hilo limezidi kuleta shinikizo kubwa kwa binadamu siku hadi siku, ili kulinda matunda ya maendeleo ya binadamu yasiharibiwe kabisa katika maafa ya hali inayoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Tokea mwaka 1990, Shirika la maendeleo na mipango la Umoja wa Mataifa kila mwaka linawashirikisha wataalamu na watafiti wa sehemu mbalimbali duniani katika kuandika na kutoa "Ripoti kuhusu maendeleo ya binadamu", na kuchambua na kutathimini masuala makubwa kuhusu maendeleo ya dunia nzima na hali ya sasa ya maendeleo ya jamii ya binadamu. Kama ilivyokuwa mwaka jana, "Ripoti kuhusu maendeleo ya binadamu" iliyotolewa tarehe 27 mwezi huu huko Geneva ilizungumzia zaidi suala la mabadiliko ya hali ya hewa. Ripoti hiyo imesema, mabadiliko ya hali ya hewa yamekuwa hali halisi, tishio lake dhidi ya binadamu limeonekana kuwa ni dhahiri siku hadi siku, hivyo kazi ya dharura ni kukabiliana na suala hilo; dunia ya hivi sasa bado ni dunia yenye ncha mbili za umaskini na utajiri, kutokana na hali ya hivi sasa na mwelekeo wa siku za baadaye, nchi zinazoendelea zitaathiriwa vibaya zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa, kwani hali ya umaskini wa sehemu ziliko nchi hizo imezidishwa na kutishia utimizaji wa malengo ya maendeleo ya milenia ya Umoja wa Mataifa; na ni vigumu kwa nchi moja peke yake au sehemu pekee kukabiliana na suala la mabadiliko ya hali ya hewa, nchi za dunia nzima lazima zishirikiane na kusaidiana ili kupata mafanikio katika utatuzi wa suala hilo.
Ripoti hiyo inasema, suala la kuongezeka kwa joto kote duniani limekuwa moja kati ya changamoto kubwa zaidi zinazoyakabili maendeleo ya binadamu katika siku za baadaye, athari ya suala hilo inaonekana siku hadi siku, ambapo milima ya barafu inayoyeyuka, na bahari ya kaskazini iliyoganda ambayo inaanza kuyeyuka, yote hayo yamekuwa ishara ya athari hiyo, na mwaka huu maafa makubwa ya ukame, mafuriko na kimbunga yalitokea mara kwa mara kote duniani, hali hii imeonesha vya kutosha athari ya mabadiliko ya hali ya hewa. Utafiti husika umeonesha kuwa, sasa imebaki zaidi ya miaka 10 tu kwa binadamu kutatua suala la kupunguza athari mbaya ya mabadiliko ya hali ya hewa kwa dunia nzima, kama binadamu watashindwa kudhibiti mwelekeo wa kuongezeka kwa joto duniani katika muda huo wa zaidi ya miaka 10, basi matokeo yake yatakuwa mabaya kabisa hata ni ya kuangamia kwa vitu vingi, na watu wa vizazi vya baadaye vya binadamu watashindwa kuvumilia matokeo hayo, huenda baada ya miongo kadhaa, hali mbaya ya kurudi nyuma kwa maendeleo ya binadamu itatokea duniani.
Ripoti hiyo imesema matokeo ya kuongezeka kwa joto duniani yatayoonekana zaidi ni kuongezeka zaidi kwa halijoto duniani, kuinuka kwa usawa wa bahari, na maafa ya ukame na mafuriko kutokea mara kwa mara. Nchi nyingi zinazoendelea zimetapakaa kwenye ukanda wa tropiki wa latitudo chini, ukanda wa nusu tropiki na kwenye visiwa, nchi hizo zitaathiriwa vibaya zaidi na matokeo hayo mabaya. Kwa kuwa nchi hizo ziko katika kipindi cha kujiendeleza, uwezo wao wa kukabiliana na maafa ni dhaifu sana ikilinganishwa na nchi zilizoendelea, hivyo zitapata hasara kubwa zaidi za maisha na mali. Ripoti hiyo inasema, kubeba matokeo mabaya makubwa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kabisa ni hali isiyo ya haki kwa nchi zinazoendelea. Kwani sababu za kuongezeka kwa joto duniani zinatokana na utandawazi wa viwanda katika nchi za magharibi katika miaka 200 iliyopita. Katika utoaji wa hewa zinazosababisha kuongezeka kwa joto duniani, nchi zilizoendelea ambazo idadi ya watu wake ni chini ya moja kati ya 6 lakini zimetoa nusu ya hewa hizo. Ripoti hiyo imesisitiza kuwa, nchi za magharibi zilizoendelea zinapaswa kutambua wajibu wao na jukumu lao la kihistoria katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, na zinatakiwa kupunguza utoaji wa hewa zinazosababisha mabadiliko ya hali ya hewa, tena zinapaswa kuharakisha mchakato huo.
Ripoti hiyo pia imetoa mapendekezo kadhaa halisi kama vile kuanzisha vituo vingi vya hali ya hewa barani Afrika, kuimarisha kazi ya kupashana habari kuhusu hali ya hewa, kuongeza uwezo wa kukinga maafa na kuanzisha mfumo kamili zaidi wa huduma za jamii.
|