Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-29 17:32:27    
Mabadiliko ya aina za burudani katika jamii ya China (sehemu ya pili)

cri

Miaka zaidi ya 20 iliyopita, wakati ambapo watu wa China walikuwa wanajitahidi kujikimu katika maisha, burudani katika jamii ya China zilikuwa chache. Wakati huo watu wengi wakimaliza kazi, walikuwa wanakaa nyumbani kusoma vitabu au kusikiliza vipindi vya radio, na marafiki walikuwa wanakaa pamoja na kucheza karata na chesi tu.

Baada ya China kuanza kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango, maendeleo ya kasi ya uchumi yamekuwa yakiinua kiwango cha maisha ya wananchi na kuleta mabadiliko makubwa katika jamii ya China. Burudani za aina mbalimbali zilianza kuingia na kuchukua nafasi muhimu kwenye maisha ya watu wa China, ambapo watu wengi walijiwekea malengo mapya kutokana na burudani na kujitambua kuwa wao wana uwezo mkubwa zaidi.

Bi. Wang Qiqi anayefanya kazi katika kiwanda kikubwa cha serikali, anatumia muda wa mapumziko kuwa darasani. Dada huyo mwenye umri wa miaka 26 ni mtulivu. Aliwahi kusoma kwenye chuo kikuu kimoja cha lugha za kigeni, na mwezi mmoja uliopita, alijiandikisha kwenye somo la lugha ya Kifaransa wakati wa mwisho wa wiki.

Kwa dada huyo ni nadra kutumia lugha ya Kifaransa kazini, hata hivyo anaona kujifunza ni furaha ya maisha. Alisema"Najifunza lugha ya Kifaransa kwa lengo moja tu la kujiburudisha. Navutiwa na utamaduni wa Kifaransa, ninapenda kupata ufahamu mwingi kuhusu utamaduni huo kwa kupitia kujifunza lugha hiyo. Zamani kulikuwa na watu wanaojifunza lugha za kigeni wakati wa mapumziko, lakini wengi walikuwa na lengo la kwenda nchi za nje kuendelea na masomo au kuzitumia lugha hizo kazini. Hivi sasa watu wengi hawasomi kutokana na shinikizo la nje, bali wanataka kujiburudisha baada ya kazi, kupata ujuzi mwingi zaidi na kuinua uwezo wao."

Kama dada huyo alivyosema, nchini China sambamba na kuinuka kwa kiwango cha maisha, watu wameanza kuzingatia burudani badala ya kujikimu tu. Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu wenye nia ya kushiriki kwenye mafunzo wakati wa mapumziko, shule nyingi zinazotoa mafunzo hayo zimejitokeza, na mafunzo hayo yanahusu mambo mbalimbali, kama vile lugha za kigeni, upigaji vinanda, upigaji picha, ngoma, mchezo wa yoga, hata usani wa mapambo ya maua na chai, hivi sasa mafunzo hayo yanawavutia watu wengi. Tofauti na hali ya miaka 30 iliyopita China ilipoanza kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango, wakati ambapo kulitokea wimbi la watu kupata mafunzo wakati wa mapumziko kwa lengo la kuinua ujuzi wao, ili kupata ajira nzuri yenye mapato makubwa zaidi na kuinua kiwango cha maisha.

Kuna watu wanaotumia muda wa mapumziko kujiburudisha, pia kuna wengine wanaotumia muda huo kutoa huduma kwa jamii. Bw. Li Yongfeng ni mkazi wa mtaa wa Lugu hapa mjini Beijing, yeye anajitolea kutoa huduma mtaani katika siku za mapumziko. Mara baada ya kuanzishwa kwa kituo cha huduma za watu wanaojitolea cha mtaa wa Lugu mwezi Agosti mwaka 2004, Bw. Li mwenye umri wa miaka 37 alijiandikisha kwenye kituo hicho.

Bw. Li anafanya kazi zinazohusu sheria, anafahamu taaluma ya sheria, kwa hiyo aliteuliwa kuwa mkuu wa kikundi cha kueneza ujuzi wa sheria cha mtaa huo. Chini ya uongozi wake, wanachama wa kikundi hicho wanatoa mafunzo na huduma za kisheria kwa wakazi wa mtaani. Bw. Li alisema  "Mwezi Aprili mwaka huu tuliandaa harakati za kueneza ujuzi wa sheria shuleni, pia tuliwafundisha wanafunzi ujuzi kuhusu usalama wa barabarani, jinsi ya kujikinga na majanga ya moto, na jinsi ya kulinda maslahi yao halali. Mbali na hayo tunatoa mafunzo yanayolenga matatizo yanayoweza kutokea wakati watoto wanapokua."

Hivi karibuni nyumba ya wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 80 kutoka familia moja iliporwa na jamaa zao, wazee hao hawakujua namna ya kulinda maslahi yao, kwa hiyo walitafuta msaada kutoka kwa watu wanaojitolea. Bw. Li akitumia ujuzi wake, aliwasaidia wazee kupata nyumba yao. Shukrani alizopata kutoka kwa wazee hao zilimtia moyo sana. Wakazi wengine pia walianza kuiga mfano wake na kujiunga na kikundi cha watu wanaojitolea kutoa huduma. Hivi sasa katika mtaa huo, wakazi zaidi ya 600 wamejiandikisha kutoa huduma ya kujitolea, mbali na harakati kubwa za mara tano hadi sita zinazofanyika kila mwaka huko mtaani, wakazi hao pia wanatoa huduma mbalimbali katika siku za mapumziko.

Akijumuisha miaka mitatu iliyopita tangu aanze kujitolea kuwahudumia wengine, Bw. Li Yongfeng alisema kwa fahari. "Katika siku za mapumziko, tofauti na wengine mimi sikufanya shughuli za kujiburudisha, bali nilijitolea kuwahudumia wengine. Naona furaha kubwa na kuishi maisha yenye thamani. Hivi sasa ni kipindi ambacho ujenzi wa mambo ya kisheria unatiliwa maanani nchini China, nilivyofanya ni mchango wangu kwa ajili ya ujenzi wa mambo ya kisheria hapa nchini."

Burudani safi za aina mbalimbali si kama tu zinasaidia kupunguza shinikizo kubwa linalotokana na maendeleo ya kasi ya uchumi kwa watu wa China, bali pia zinawaletea furaha kubwa.

Idhaa ya kiswahili 2007-11-29