Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-29 17:59:38    
Mfuko wa watoto wa China waweka masanduku zaidi 300 kwa ajili ya kutoa michango ya kuwasaidia watoto wenye uwezo dhaifu wa kuona

cri

  

Mfuko wa watoto wa China na kampuni ya New World Department Store ya China hivi karibuni zilisaini makubaliano kuhusu "shughuli za siku nzuri zijazo, kuwajengea dunia mpya kwa watoto wenye uwezo dhaifu wa kuona". Kutokana na makubaliano hayo kampuni hiyo itaweka masanduku zaidi ya 300 ya kuchangisha fedha kwenye maduka yake mbalimbali nchini China, fedha zitakazochangiwa zitawasilishwa kwenye mfuko wa watoto wa China kutumika katika kuwasaidia watoto wenye uwezo dhaifu wa kuona wanaotoka kwenye familia zenye matatizo ya kiuchumi.

Habari zinasema mwezi Juni mwaka 2002 mfuko wa watoto wa China ulianzisha "mfuko maalumu kwa watoto wenye uwezo dhaifu wa kuona". Hatua hii imeungwa mkono kwa nguvu na watu kutoka sekta mbalimbali za jamii na watu kutoka Hongkong. Miaka mitano iliyopita, mfuko huo ulichangia zaidi ya yuan milioni 7, na kuwasaidia watoto 1100 kutoka miji 17 wenye uwezo dhaifu wa kuona wanaotoka kwenye familia zenye matatizo ya kiuchumi.

Kwenye shughuli ya kusaini makubaliano, mchezaji wa filamu kutoka Hongkong Bw. Zhong Zhentao alisifiwa na mfuko wa watoto wa China kuwa ni balozi wa kueneza shughuli za "siku nzuri zijazo" wa nchi nzima. Alisema, atafanya juhudi kadiri awezavyo kuwasaidia watoto wenye uwezo dhaifu wa kuona.

Na tarehe 17 mwezi Oktoba Kampuni ya komyuta ya Changchen ya China pia ilianzisha shughuli kubwa ya kuwasaidia watoto wenye uwezo dhaifu wa kuona wanaotoka kwenye familia zenye matatizo ya kiuchumi. Kampuni hiyo itasaidia watoto 80 kupitia mfuko wa watoto wa China.

Mkurugenzi wa Hospitali ya macho ya watoto ya Beijing Bw. Li Zhisheng alitufahamisha kuwa, asilimia 5 ya watoto wana uwezo dhaifu wa kuona, China ina watoto milioni 12 wenye uwezo dhaifu wa kuona. Kipindi mwafaka zaidi cha kutoa matibabu ya tatizo hilo ni umri wa miaka mitatu hadi umri wa miaka sita, na watoto wenye umri wa zaidi ya miaka 13 hawawezi kupona kikamilifu. Hadi sasa, mfuko huo umewasaidia watoto zaidi ya elfu moja.

Wasikilizaji wapendwa, tarehe 25 mwezi Novemba imethibitishwa na Umoja wa Mataifa kuwa ni "siku ya kukomesha matumizi ya nguvu ya kimabavu katika familia duniani". Kiongozi wa idara ya kulinda haki na maslahi ya shirikisho kuu la wanawake wa China, Bi. Jiang Yue'e hivi karibuni alisema, kupambana na matumizi ya nguvu ya kimabavu kwenye familia ni moja ya kazi muhimu ya kulinda haki na maslahi ya wanawake na watoto nchini China, hivi sasa China imeunda kwa hatua ya mwanzo mfumo wa ushirikiano wa idara mbalimbali wa kupambana na matumizi ya nguvu ya kimabavu katika familia.

Habari zinasema mwaka 2001 shirikisho kuu la wanawake wa China lilishirikiana na idara 13 za serikali kuu ya China kuanzisha kikundi cha uratibu cha kulinda haki na maslahi ya wanawake na watoto. Hivi sasa mikoa na miji mingi nchini China imeanzisha vikundi vya uratibu wa kazi ya kulinda haki na maslahi ya wanawake na watoto, na idadi ya miundo ya uratibu iliyopo nchini China imezidi elfu 35, ambayo inafanya kazi muhimu katika ukaguzi wa utekelezaji wa sheria na kushughulikia matukio ya aina hiyo.

Bibi Jiang Yue'e alisema kuanzishwa kwa mfumo huo kunahimiza kazi ya kupambana na matumizi ya nguvu ya kimabavu katika familia iingie katika kazi kuu ya serikali.

Wakati huo huo, idara mbalimbali za serikali ya China pia zinaimarisha ushirikiano, na kuchukua hatua nyingi za kupambana na matumizi ya nguvu ya kimabavu katika familia. Idara za usalama wa umma zilizoko kwenye sehemu nyingi nchini China, zimeanzisha vituo vya kuomba msaada wa polisi kutokana na matumizi ya mabavu katika familia; Idara za mambo ya kiraia za sehemu mbalimbali nchini China pia zimeanzisha vituo vya kuwasaidia watu kutokana na matumizi ya nguvu ya kimabavu katika familia; Idara nyingi za sheria ziliweka vituo vya msaada wa sheria kwa wanawake, na kuteua maofisa wa shirikisho la wanawake katika ngazi ya shina kuwa wasuluhishi, na kufanya kazi yao ya kutatua migogoro kwenye familia.