Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-30 16:06:45    
Kikosi cha kulinda amani cha China chaanza kutekeleza majukumu kwenye sehemu ya Darfur

cri

Kikosi cha utangulizi cha askari wa uhandisi cha China kitakachojiunga na jeshi la mseto la kulinda amani la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, tarehe 23 usiku kilifunga safari kwenda Sudan kutoka mji wa Zhengzhou mkoani Henan nchini China. Hicho ni kikosi cha kwanza cha kulinda amani kinachotumwa na China kwenda kwenye sehemu ya Darfur, pia ni kikosi cha kwanza cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kwenye sehemu hiyo.

"Askari wote, kulia geuka! Panda ndege! "

Kikosi hicho kinachoundwa na askari 135 kinaongozwa na ujumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kwenye sehemu ya Darfur, kikosi hicho kinaundwa na vikundi vya uongozi, upimaji wa vyanzo vya maji, barabara na madaraja, ujenzi na utengenezaji, uhakikishaji wa misaada, na ulinzi.

Mkuu wa kikosi hicho Bw. Shangguan Linhong alijulisha kuwa, askari hao waliandaa mipango zaidi ya kumi, na kukamilisha mazoezi ya saa 609, pia walipokea mafunzo ya namna ya kulinda amani na sheria na kanuni husika, wote wanajua kutumia maneno machache ya lugha ya Kiingereza na Kiarabu kufanya mawasiliano. Bw. Shuangguan alisema,

"Kwanza, tuliimarisha mazoezi ya ulinzi, uwezo wa kujilinda wa askari na uwezo wa ulinzi wa kikosi umeongezeka. Pili tulifanya mazoezi ya ufundi maalumu, kiwango cha kujizatiti kwa maofisa na askari kimeongezeka, na uwezo wa kikosi chetu wa kukabiliana na hali ya dharura na kushughulikia miradi pia umeimarishwa. Tatu, tuliimarisha mafunzo ya elimu ya kawaida ya kulinda amani, kuimarisha mtazamo wa askari kuhusu kufuata kanuni na sheria, na kuinua uwezo wao wa kuwasiliana na watu wengine na kushughulikia masuala mbalimbali."

Baada ya kuwasili nchini Sudan, kikosi cha askari wa uhandisi cha kulinda amani cha China kitawekwa mjini Niyala, mkoani Darfur Kusini. Kikosi hicho kitatekeleza majukumu ya kuhakikisha ujenzi wa miradi kama vile kujenga na kuratibu barabara, madaraja, majengo, na viwanja vya ndege, na kutafuta chanzo cha maji, ili kuweka mazingira mazuri kwa operesheni ya mseto ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika. Askari hao wote waliona fahari kutekeleza majukumu ya kulinda amani kwenye sehemu ya Darfur.

"Nafurahi sana kuiwakilisha nchi yangu kutekeleza majukumu hayo. " 

"Nikiwa mwanajeshi, niko tayari kujitoa mhanga kwa ajili ya maslahi ya taifa."

"Kupewa majukumu hayo ni uaminifu wa taifa kwetu."

"Tukiwa askari wa kikosi cha kwanza cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kwenye sehemu ya Darfur, tunaona kuwa ni majukumu muhimu. Tutakamilisha majukumu mbalimbali ya Umoja wa Mataifa, na kujenga msingi imara kwa vikosi vya kulinda amani vitakavyowekwa. Tutatoa mchango mkubwa katika kuhimiza utulivu na maendeleo ya sehemu ya Darfur nchini Sudan, na kulinda amani ya dunia."

Tarehe 31 mwezi Julai mwaka huu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio No.1769, na kuamua kutuma jeshi la mseto la kulinda amani la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika lenye askari elfu 26 kwenye sehemu ya Darfur. Kwa mujibu wa mwaliko wa Umoja wa Mataifa, serikali ya China mwezi Aprili mwaka huu iliamua kutuma kikosi cha askari wa uhandisi kwenye sehemu ya Darfur. kikosi hicho chenye askari 315 kiliundwa rasmi mwezi Juni.

Siku zote suala la Darfur linazingatiwa sana na jumuiya ya kimataifa. Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mambo ya kulinda amani Bw. Marie Guehenno, ambaye alifanya ziara nchini China hivi karibuni, alieleza kuwa kuweka jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa kwenye sehemu ya Darfur kunakabiliwa na changamoto nyingi. Hivi sasa serikali ya Sudan na makundi ya upinzani ya Sudan yote yanaunga mkono kuwekwa kwa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa. Bw. Guehenno alisema hali hiyo haikutokea katika historia, hivyo Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa una imani imara kuhusu kazi ya kulinda amani kwenye sehemu ya Darfur.

Katika muda uliopita, maoni ya China kuhusu suala la Darfur na umuhimu ilioonesha China katika suala hilo ulitiliwa maanani zaidi na zaidi na jumuiya ya kimataifa. Mkurugenzi wa ofisi ya mambo ya kulinda amani ya wizara ya ulinzi ya China Bw. Shi Zhengbo alisema, China ni nchi ya kwanza iliyojiunga na jeshi la mseto la kulinda amani la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kutokana na mwaliko wa Umoja wa Mataifa, pia ni nchi ya kwanza iliyotuma kikundi cha uchunguzi kwenye sehemu ya Darfur.

Bw. Shi Zhengbo alisema msimamo na sera ya serikali ya China kuhusu suala la Darfur inakubaliwa na serikali za nchi nyingi duniani, zikiwemo nchi za Afrika na nchi nyingi zinazoendelea. Siku zote China inaonesha umuhimu wa kiujenzi katika utatuzi wa suala la Darfur, vilevile inafanya juhudi kushiriki kwenye harakati za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.

Tangu mwaka 1990 China ilipotuma wachunguzi watano wa kijeshi kushiriki kwenye kazi za kulinda amani za Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza, China imeshiriki kwenye harakati 17 za kulinda amani za Umoja wa Mataifa, na kutuma wanajeshi 8,095 wa kulinda amani kwa jumla. Hivi sasa kuna askari 1,648 wanaotekeleza majukumu ya kulinda amani kwenye sehemu 10 za majukumu ya Umoja wa Mataifa na idara ya kulinda amani ya Umoja huo.

Mkurugenzi wa ofisi ya mambo ya kulinda amani ya eneo la kijeshi la Jinan Bw. Wang Encheng alisema, siku zote China inashirikiana na Umoja wa Mataifa kwenye harakati za kulinda amani, na kuonesha sura ya nchi kubwa iliyobeba wajibu.

Bw. Guehenno alisema vikosi vya madaktari na askari wa uhandisi vilichotumwa na China vilisaidia kwa ufanisi kwenye harakati za kulinda amani za Umoja wa Mataifa. Kwa upande wa siasa, China kushiriki kwenye harakati za kulinda amani za Umoja wa Mataifa kumekuwa ni mwelekeo wa sasa, hii inaonesha kuwa si kama tu China inaunga mkono maamuzi husika ya Umoja wa Mataifa, bali pia inaweza kuimarisha utaratibu wa pande nyingi duniani, na kuzifanya harakati za kulinda amani za Umoja wa Mataifa zipate mafanikio makubwa zaidi.

Alipozungumzia mpango wa serikali ya China kuhusu kushiriki kwenye harakati za kulinda amani katika siku za baadaye, Bw. Shi Zhengbo alisema, China itafanya juhudi kuwaandaa kwa pande zote askari watakaotekeleza majukumu ya kulinda amani kwenye sehemu ya Darfur, pia itaendelea kujitokeza kushiriki kwenye utekelezaji wa majukumu ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa.

Idhaa ya kiswahili 2007-11-30