Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-03 15:48:25    
Utalii kwenye mlima Huaguo wa mji wa Lianyungang

cri

Kama umewahi kusoma kitabu cha hadithi maarufu ya kale ya China iitwayo "Safari ya Magharibi", hakika unaweza kumkumbuka Sun Wukong, mfalme kima mwenye uwezo mkubwa. Kitabu hicho kinasema, maskani ya Sun Wukong ni mlima wa Mungu unaoitwa mlima Huoguo, neno Huaguo katika lugha ya Kichina lina maana ya maua na matunda, kwa kuwa katika mlima huo kuna maua na matunda katika mwaka mzima. Kuna mlima mmoja unaoitwa Huaguo, kwenye mji wa Lianyungang, mkoani Jiangsu, sehemu ya pwani ya mashariki ya China, inasemekana kuwa mlima Huoguo unaotajwa katika hadithi ya "Safari ya Magharibi", ndiyo mlima wa asili wa Huaguo.

Mlima Huaguo wa mji wa Lianyungang ni sawa na milima ulioelezwa katika hadithi ya "Safari ya Magharibi", hali ya hewa ya huko ni nzuri kwa binadamu, una mandhari nzuri ya ajabu, na ni mahali pazuri kama pepo ya duniani.

Mlima Huoguo una sehemu zaidi ya 100 zenye mandhari nzuri, ambazo nyingi zake ni sawasawa na kama ilivyoelezwa kwenye kitabu cha hadithi ya "Safari ya Magharibi". Kwa mfano, kuna jiwe alikozaliwa Sun Wukong lenye umbo linalofanana na kima, hususan lile pango la kuvutia watalii, ambalo maji yanatiririka kutoka sehemu yake ya juu na kuonekana kama pazia la maji linalosetiri mdomo wa pango la mlimani. Hadithi hiyo pia inasema, pango hilo la mlimani lenye pazia la maji ni maskani yenye furaha ya Sun Wukong na kundi kubwa la kima wadogo. Ukiangalia sehemu ya nje kutoka ndani ya pango hilo, unaweza kuona maji yakianguka kutoka sehemu ya juu ya pango hilo refu na lenye ukimya mwingi, ambalo linaonekana kama limetengwa na dunia. Ndani ya pango hilo, kuna meza ya kimaumbile ya mawe pamoja na viti, jinsi inavyoonekana ni kama Sun Wukong na kima wadogo waliondoka wakati ule ule. Kwa mujibu wa Mwongozaji wa watalii Bi Shen Hailing, huko kuna masimulizi kuhusu pango hilo lenye pazia la maji, alisema:

"Inasemekana kuwa, mwandishi aliyetunga hadithi ya "Safari ya Magharibi" Wu Chengen alipofanya maandalizi ya kubuni hadithi hiyo, alifanya matembezi kwenye mlima Huaguo, na alipumzika ndani ya pango hilo, wakati ule lilikuja kundi la kima, ambao walipekua na kuangalia zile karatasi zilizoandikwa maneno ya hadithi, walisema mzee huyo amekuwa hapa kwa muda mrefu, lakini hataki kuandika hadithi kuhusu sisi, hivyo wakachanua zile karatasi. Baada ya Wu Chengen kuamka kutoka usingizini, karatasi zilizoandikwa maneno ya hadithi pamoja na kalamu na karatasi nyingine nyeupe zote hazikuonekana, ila aliona tu kundi la kima wanaorukaruka kwa furaha, lakini hakukasirika, bali aliwahurumia wale kima, hivyo aliandika kuhusu kundi la kima katika kitabu cha hadithi ya "Safari ya Magharibi"

Kwenye mlima Huaguo, kima wanazungumzwa kila mahali, wao ndio ni wenye mlima Huaguo halisi, kila mtalii aliyefika kwenye mlima Huaguo, anavutiwa na mlima huo. Kima hao watundu ama wanacheza kwa furaha, ama wanaona ajabu na kuwaangalia watalii, wakati mwingine wanafanya masihala na watalii, na hawaogopi wageni. Mwogoza watalii Bi Shen Hailing alisema, kima wanaoishi kwenye mlima Huaguo ni kima pori, wameishi huko kizazi hadi kizazi, na kila kundi la kima lina mfalme wao. Kima mfalme ni kima dume mwenye nguvu, na ana nguvu ya kulidhibiti kabisa kundi la kima, wanapopata chakula, kima mfalme anakula kwanza, licha ya hayo kima vijana jike wazuri wa kundi hilo ni wake zake peke yake. Chini ya uongozi wa kima mfalme, kila kundi la kima lina eneo lake maalumu kwenye mlima Huaguo, alisema.

"Kima wa kila kundi wanaishi peke yao kwenye eneo lao, na kamwe hawawezi kwenda kwenye eneo la kundi lingine la kima. Endapo kundi moja la kima litaingia kwenye eneo la kundi lingine la kima, vita vinaweza kuzuka wakati wowote, na watapigana kufa na kupona."

Mwongoza watalii alisema, kima wawili watundu wanaoishi kwenye mlima Huaguo, wanapendwa sana na watalii. Siku moja mwongoza watalii alishuhudia kima wadogo wawili wakipanda kwenye mti kuchukua mayai ya ndege, hatimaye vilizuka vita kati ya ndege hao na kima, watalii waliokuwa huko wakati ule walichekeshwa sana na kima wale watundu.

Mlima Huaguo licha ya kuwa na mandhari nzuri ya kuvutia, pia una mabaki mengi ya kiutamaduni, majengo ya kale yaliyoko kwenye mlima ni yenye umaalumu wa kipekee. Mnara wa mfalme A'Yu ulioko chini ya mteremko wa mlima ni jengo la alama ya mlima Huaguo. Mnara huo ulijengwa mwaka 1023, na umeshakuwa na historia ya miaka karibu elfu moja. Mnara huo uliojengwa kwa matofali ni jengo la pande nane lenye ghorofa nane, na lina urefu wa mita 10. Ingawa matetemeko yamewahi kutokea mara nyingi kwenye sehemu hiyo, lakini mnara huo bado ni mzima kabisa. Mbali na hayo, mlima Huaguo una hekalu moja linaloitwa Haining, majengo yote ya hekalu hilo ni yenye mtindo wa kale. Majengo hayo makubwa yalijengwa kwenye mteremko wa mlima, na ni hekalu linalojulikana kwa watu wa mbali, kila siku kuna waumini wanaokwenda huko kuwaabudu mabudha.

Mabaki mengi ya kiutamaduni na mandhari nzuri ya kimaumbile ya mlima Huaguo, vinawavutia watalii kutoka nchi mbalimbali duniani. Bi. Habibah Mohd Samin kutoka Malaysia ni mara yake ya kwanza kufika huko, mlima Huaguo ulimpa kumbukumbu nyingi, alisema:

"Mandhari ya hapa ni nzuri sana, tena hali ya hewa pia ni nzuri, licha ya hayo, kuna vivutio vingi kwenye mlima huo, nimefurahi sana baada ya kufika hapa."

Mlima Huaguo una miti na mimea mingi, na matunda yanapatikana katika majira yote manne ya mwaka, kama vile matunda ya kiwi, Ginseng na Chestnut, hususan mianzi ya Jinxiangyu, ambayo katika lugha ya Kichina ina maana ya "mianzi ya dhahabu iliyotiwa jade", mianzi ya aina hiyo ni ya rangi ya dhahabu, lakini pingili zake ni za rangi ya kijani na zimeingia kidogo kwa ndani, kama vya jade ya rangi ya kijani zilizotiwa kwenye dhahabu.

Mianzi ya aina hiyo inasifiwa kuwa ni moja ya aina nne za mianzi inayopendeza, ambayo inaota kwenye mlima Huaguo tu, wala haiwezi kuota kwenye sehemu nyingine, hivyo imekuwa na thamani kubwa kuliko mianzi ya aina nyingine. Mlima Huoguo una michai ya Yunwu, ambayo katika lugha ya Kichina ni "michai ya mawingu na ukungu". Mtu akinywa chai ya Yunwu iliyotumia maji ya chemchemi ya mlimani, anasikia raha sana. Mkurugenzi wa idara ya utalii ya mji wa Lianyungang, Bw. Li Daoying alisema, michai hiyo inaota kwenye mawingu na ukungu, hivyo michai hiyo inaitwa "michai ya mawingu na ukungu", endapo michai hiyo ingeota kwenye sehemu nyingine isiyo na mawingu na ukungu, basi uzuri wa chai yake usingekuwa sawa na chai hiyo.

Idhaa ya kiswahili 2007-12-03