Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-03 15:37:16    
Moja ya vipindi 24 katika kalenda ya kilimo ya China, Kuanguka kwa Theluji Nyembamba

cri

Katika kalenda ya kilimo ya China kuna vipindi 24 kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa nchini China. Tunaposema siku ya kipindi Fulani tuna maana ya siku ya kuanza kwa kipindi hicho. Kugawa vipindi hivyo 24 katika kalenda ya kilimo ya China kunatokana na busara za Wachina wa kale na elimu yao ya unajimu, vipindi hivyo vinasaidia sana kupanga shughuli za kilimo. Kwa mujibu wa historia, mapema miaka zaidi ya 2,000 iliyopita watu wa China walikuwa wamepata vipindi hivyo 24, yaani vipindi viwili kila mwezi.

Kipindi cha Kuanguka kwa Theluji Nyembamba kinaanzia tarehe 23 au 24 Oktoba, mwaka huu siku ya kuanza kwa kipindi hicho ni tarehe 24. Kuanguka kwa Theluji Nyembamba ni kipindi cha mwisho katika majira ya Autumn yaani majira ya kupukutika kwa majani nchini China. Kipindi hicho kinaashiria kwamba halijoto inakuwa imebadilika na kuwa baridi, na umande unaanza kuganda na kuwa kama theluji nyembamba juu ya majani. Kutokana na halijoto kupungua na kuwa chini hadi nyuzi sufuri au chini zaidi na hewa karibu na ardhi inakuwa na unyevunyevu, umande unaganda na kuwa theluji nyembamba.

Kipindi cha Kuanguka kwa Theluji Nyembamba ni muhimu kwa shughuli za kilimo. Tokea kipindi kilichopita yaani Umande wa Baridi hadi kipindi hicho ni muda wa nusu mwezi, huu ni muda mzuri kwa wakulima kushughulika na mavuno. Wachina wanasema, "Ni mapema kuvuna viazi vitamu katika kipindi cha Umande wa Baridi, na utakuwa umechelewa kama utaanza kuvuna baada ya siku ya kuanza kwa Majira ya Badiri, wakati unaofaa kuvuna viazi vitamu ni kipindi cha Kuanguka kwa Theluji Nyembamba". Kwa sababu katika kipindi cha Umande wa Baridi viazi vitamu vinakuwa bado havijakomaa, na vikivunwa baada ya mwezi mmoja yaani Majira ya Baridi kuanza, itachelewesha upandaji wa mbegu za ngano katika mashamba ya viazi, kwa hiyo ni wakati huo tu ndio unaofaa kuvuna viazi, tena viazi vya wakati huo vina wanga mwingi na lishe nyingi. Katika sehemu kubwa ya kaskazini ya China siku kabla na baada ya kipindi hicho pia ni siku za kuvuna pamba na kupanda mbegu za ngano inayopitia Majira ya Baridi.

Katika kipindi hicho alfajiri na usiku kunakuwa na baridi na hata theluji inaweza kuanguka katika mikoa ya Xinjiang na Qinghai, kaskazini magharibi mwa China. Theluji nyembamba inaweza kutokea juu ya majani ya mboga. Wachina wanasema "Theluji nyembamba inaharibu mimea", kwa hiyo katika kipindi hicho wakulima wanazingatia sana kukinga baridi kwa mimea na wanyama, idara ya utabiri wa hali ya hewa pia inatangaza utabiri wake kuwaambia wakulima kama yatatokea mabadiliko ya hali ya hewa.

Elimu ya tiba ya Kichina inasema, baada ya kuanza kwa majira ya Autumn inafaa kula chakula kinacholeta joto mwilini. Kutokana na halijoto kubadilika kuwa baridi mwili unahitaji joto. Lakini kuongeza joto kwa chakula katika siku za baridi kali si busara kama kula nyama ya ng'ombe na mbuzi na kulimbikiza joto jingi mwilini na kuharibu uwiano kati ya joto la mwilini na nje, kwa hiyo kuna msemo ulioenea miongoni mwa Wachina unasema, "ni bora kufidia afya katika kipindi cha Kuanguka kwa Theluji Nyembamba kuliko katika majira ya baridi". Chakula kinachotumika sana katika kipindi hicho ni supu ya nyama ya mbuzi, ambayo inapikwa kwa kuchemsha pole pole maji yenye tangawizi na tende.

Katika China ya kale, kipindi cha Kuanguka kwa Theluji Nyembamba pia ni siku za kuzuru makaburi, mbali na siku ya Qingming yaani "Siku ya Kuzuru Makaburi" mwezi Aprili. Katika siku hiyo Wachina wanatoa heshima au kufanya tambiko mbele ya makaburi ya mababu zao, hivi leo mila hiyo haionekani sana. Zaidi ya hayo, katika sehemu ya kabila la Wazhuang mkoani Guangxi wenyeji wanaendelea na mila ya kufanya sherehe katika siku ya tisa baada ya siku ya kuanza kwa kipindi cha Kuanguka kwa Theluji Nyembamba, siku hiyo wanaimba huku wanapiga ngoma kusherehekea mavuno mazuri.