Mkutano wa pili wa viongozi wakuu wa Ulaya na Afrika ulioahirishwa kwa miaka minne utafanyika tarehe 8 hadi 9 katika Lisbon, mji mkuu wa Ureno, nchi mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya. Kadiri mkutano huo unavyokaribia, waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown anaendelea kushikilia msimamo wa kutohudhuria mkutano huo kama rais Robert Mugabe wa Zimbabwe atahudhuria, kwa hiyo bado kuna tatizo kama mkutano huo utakuwa kweli ni mkutano wa viongozi wakuu.
Mkutano huo ukiwa kama ni jukwaa la mazungumzo kati ya bara la Ulaya na Afrila ulifanya mkutano wa kwanza huko Cairo, mji mkuu wa Misri. Kwa sababu wakati huo Zimbabwe ilitekeleza sera ya mageuzi ya umiliki wa ardhi ambayo ilidhuru maslahi ya walowezi wa kizungu, waziri mkuu wa Uingereza wa wakati huo Bw. Tony Blair alisusia mkutano huo. Kutokana na athari ya Uingereza, uhusiano kati ya nchi za Magharibi na Zimbabwe mara ulibadilika kuwa mbaya. Mwaka 2002 kwa kisingizio cha serikali ya Zimbabwe kukandamiza demokrasia, kuwadhulumu watu wa upinzani na wizi wa uchaguzi, Umoja wa Ulaya uliiwekea Zimbabwe vikwazo ikiwa ni pamoja na kuzuia mali za nchi hiyo katika nchi za nje na kuwazuia viongozi wa nchi hiyo kusafiri kwenda kwenye nchi za Umoja wa Ulaya. Hatua hizo za Umoja wa Ulaya zilizikasirisha nchi za Afrika, na mkutano wa pili uliopangwa kufanyika mwaka 2003 uliahirishwa mara kwa mara katika muda wa miaka minne kutokana na Umoja wa Ulaya kutomwalika Rais Robert Mugabe kuhudhuria mkutano huo.
Katika miaka ya hivi karibuni kadiri nchi nyingi zinavyozidi kuzingatia Afrika, ndivyo Umoja wa Ulaya unavyozidi kutambua umuhimu wa uhusiano kati yake na Afrika na umeandaa mkakati mpya kwa lengo la kujenga uhusiano ulio sawa wa kiwenzi licha ya kuendelea na ushirikiano uliopo kati yake na nchi za Afrika. Katika hali hiyo, kufanya mkutano huo wa pili mapema zaidi ni matumaini ya pande zote mbili. Ureno ambayo ilikuwa ni moja ya nchi zilizotawala barani Afrika na yenye maslahi katika bara hilo, ilipokuwa nchi mwenyekiti wa Umoja wa Ulala katika nusu ya pili ya mwaka huu, kazi iliyopewa kipaumbele ni kuufanya mkutano huo wa pili ulioachwa kwa miaka minne iliyopita ufanyike katika mji mkuu wake Lisbon. Lakini jambo hilo sio rahisi, kwani suala la haki ya Robert Mugabe kuhudhuria mkutano huo bado ni tatizo kama zamani.
Hali ilivyo ni kwamba Umoja wa Ulaya na Afrika, pande mbili ziliwahi kugongana mara kadhaa katika mazungumzo. Kutokana na kuwa Umoja wa Ulaya unashikilia msimamo dhidi ya Rais Robert Mugabe na kuimarisha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Zimbabwe mikutano kadhaa ya mawaziri iliwahi kufutwa. Umoja wa Afrika kwa mara madhaa uliwahi kusema kwamba mkutano wa viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya na Afrika lazima uzishirikishe nchi zote za Afrika. Nchi za SADC zilitoa taarifa ikisema kama mkutano huo hautamwalika Rais Robert Mugabe zitagoma kuhudhuria mkutano huo. Baada ya kupima hasara na faida, serikali ya Ureno mwishowe imeamua kualika nchi zote za Afrika kwenye mkutano huo. Kwa hiyo imekuwa bayana kwamba Rais Robert Mugabe atahudhuria mkutano huo, suala lililobaki sasa ni kwamba je waziri mkuu wa Uingereza atahudhuria?
Vyombo vya habari vinaona kuwa mkutano huo utakaofanyika mjini Lisbon utakuwa ni fursa nzuri ya kuweka uhusiano mzuri kati ya Umoja wa Ulaya na Afrika, msimamo wowote wa kumkana kiongozi fulani wa nchi au kukataa kushiriki kwenye mkutano huo kutokana na ubaguzi haufai, na hali ya kiongozi yeyote wa nchi kukosa kushiriki kwenye mkutano huo italeta masikitiko kwa mkutano huo ambao haukupatika kiurahisi.
|