Mkutano wa mawaziri wa jumuiya ya nchi zinazozalisha mafuta duniani, OPEC, ambao ulifanyika tarehe 5 mwezi Desemba mjini Abu Dhabi, uliamua kutoongeza kwa muda uzalishaji wa mafuta. Taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo kumalizika inasema, hivi sasa kwa jumla hakuna mabadiliko katika pande mbili za mahitaji na utoaji wa mafuta kwenye soko la kimataifa, mafuta yaliyopo kwenye soko la kimataifa ni mengi ya kutosha, tena mafuta yaliyoko kwenye mabohari yako kwenye kiwango mwafaka, hivyo OPEC imeamua kudumisha kiwango cha sasa cha uzalishaji wa mafuta. Na kuhusu kama kuna haja ya kuongeza uzalishaji wa mafuta, taarifa inasema suala hilo litaangaliwa kwenye mkutano utakaofanyika mwezi Februari mwaka kesho.
Wachambuzi wanasema kupanda kwa bei ya mafuta kwa hivi sasa, hasa kunatokana na kupungua kwa thamani ya dola ya kimarekani, ulanguzi wa mafuta masokoni pamoja na mambo ya kisiasa ya kikanda, hayo pia ni maoni ya nchi wanachama wa OPEC, hivyo siyo ajabu kufanya uamuzi wa namna hiyo kwenye mkutano huo.
Kwanza, nchi wanachama wa OPEC zinapinga kuongeza uzalishaji wa mafuta. Kwenye ufunguzi wa mkutano wa mawaziri wa tarehe 5 baadhi ya nchi wanachama zilisema, hazitaongeza uzalishaji wa mafuta kutokana na shinikizo la nchi zinazonunua mafuta. Waziri wa mafuta wa Umoja wa falme za kiarabu Bw. Ali Al Naimi alisema, "Sisi hatujaona mahitaji ya kurekebisha uzalishaji wa mafuta." Waziri wa mafuta wa Iran Bw. Gholamhossein Nozari alisema, "Msimamo wetu ni kuwa hivi sasa kuna uwiano mzuri kati ya ununuzi na uzalishaji, na hakuna haja ya kuongeza mafuta kwenye soko la kimataifa." Kabla ya hapo, mawaziri wa mafuta au mawaziri wa nchi za Qatar, Umoja wa falme za kiarabu, Algeria na Venezuela walitoa maelezo kama ya hayo.
Pili, kutokana na kuendelea kupungua kwa bei ya mafuta kwenye soko la kimataifa, shinikizo kutoka nje la kutoka OPEC iongeze uzalishaji wa mafuta, na hata nia yake ya kutaka iongeze uzalishaji wa mafuta imepungua. Baada ya kuvunja rekodi ya juu kabisa katika historia kwa bei ya mafuta tarehe 21 mwezi Novemba, ambayo ilifikia dola za kimarekani 99.29, bei ya mafuta duniani ilishuka kwa udhahiri, katika muda wa karibu wiki moja bei ilishuka kwa karibu kwa dola 10 za kimarekani. Kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta, pia wazo la OPEC la kutaka kuongeza uzalishaji wa mafuta hivi karibuni pia limepungua.
Aidha katika hali ambayo thamani ya dola za kimarekani inapungua, kutokea kwa mfumuko wa bei za vitu na kupanda kwa gharama za uzalishaji wa mafuta, nchi wanachama wa OPEC zinaona ni kwa kupandisha bei ya mafuta tu, ndipo zitaweza kufidia hasara zinazopata nchi zinazotoa mafuta, hivyo nchi wanachama za OPEC, hususan nchi wanachama zilizoko nyuma kiuchumi, hazikubali kushusha bei ya mafuta kwenye soko la kimataifa kwa njia ya kuongeza uzalishaji mafuta.
Mbali na hayo, idara ya upelelezi ya Marekani ilitoa ripoti mpya ya tathmini kuhusu suala la nyukilia la Iran tarehe 3 mwezi Desemba, ambayo huenda inaathiri kuongeza utoaji mafuta wa OPEC. Katika mwezi uliopita, OPEC iliashiria kuwa itaongeza uzalishaji kwa mapipa laki 5 kwa siku. Lakini baada ya kutolewa ripoti hiyo, OPEC haikutaja tena suala la kuongeza uzalishaji mafuta. Kuna wachambuzi wanaosema kuwa sababu yake huenda ni ripoti hiyo kusema Iran iliacha mradi wa uzalishaji wa silaha za nyukilia, tena hadi hivi sasa haijazindua upya mradi huo, jambo hilo limepunguza wasiwasi wa watu kuwa huenda suala la nyukilia la Iran litasababisha wasiwasi wa kikanda, hivyo nchi wanachama za OPEC zinaona, hakuna haja ya kulikabiliana na suala hilo kwa kuongeza uzalishaji mafuta.
Lakini baada ya mkutano wa OPEC kutangaza kutoongeza uzalishaji wa mafuta, bei ya mafuta ilipanda kwa dola 1. Watu wanaona kuwa sera za OPEC kuhusu mafuta ni kitu kinachoathiri bei ya mafuta na uchumi wa dunia.
|