Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-10 15:46:24    
Ulaya na Afrika zaanzisha uhusiano kiwenzi na kimkakati

cri

Mkutano wa pili wa siku mbili wa viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya na Afrika ulifungwa tarehe 9 huko Lisbon, mji mkuu wa Ureno, nchi mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya. Kwenye mkutano huo viongozi kutoka nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya na nchi 53 za Afrika walijadiliana waraka wa "Uhusiano wa kiwenzi na kimkakati kati ya Afrika na Umoja wa Ulaya" na kuandaa "Mpango wa Utekelezaji kwa Mwaka 2008-2010".

"Taarifa ya Lisbon" iliyotolewa baada ya mkutano huo inasema, baada ya juhudi za miaka 50 tokea Umoja wa Ulaya uanzishwe na harakati za uhuru wa Afrika, leo hii mkutao huo wa viongozi wakuu wa Afrika na Umoja wa Ulaya umeleta nafasi nzuri ya kukabiliana na changamoto kwa pamoja. Kwa kauli moja pande mbili zimekubali kuanzisha uhusiano wa aina mpya ambao ni tofauti kabisa na ule wa zamani kwa msingi wa usawa, kunufaishana na kuheshimiana. Waziri mkuu wa Ureno, nchi mwenyeji wa mkutano huo, Bw. Jose Socrates alisema,

"Nafurahia sana mafanikio yaliyopatikana kwenye mkutano huu, kwa sababu ni mkutano wenye maana ya kihistoria katika uhusiano kati ya Ulaya na Afrika."

Mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika, rais wa Ghana Bw. John Kufuor alisema,

"Baada ya mazungumzo ya siku mbili tumepitisha mpango wa utekelezaji wa wenzi wa kimkakati, uhusiano kati ya Ulaya na Afrika umepata mafanikio makubwa. Utekelezaji wa mkakati huo utafanya uhusiano kati yetu uwe wa kasi na kuisukuma Afrika kwenye utandawazi duniani."

Kwenye mkutano huo washiriki wameanzisha kwanza uhusiano wa kiwenzi katika sekta nane muhimu. Mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya Bw. Jose Manuel Barroso alieleza,

"Mkutano huu umeandaa mpango wa utekelezaji katika muda wa miaka mitatu ijayo, tutaanzisha uhusiano wa kiwenzi katika mambo ya amani na usalama, demokrasia na haki za binadamu, biashara ya kikanda, malengo ya milenia, nishati, mabadiliko ya hali ya hewa, uhamiaji, watu wanaohamahama na ajira, sayansi na upashanaji habari na anga ya juu."

Mkutano wa viongozi wakuu wa Afrika na Ulaya kwa mara ya kwanza ulifanyika mwezi Aprili mwaka 2004, na mkutano wa pili ulipangwa kufanyika mwaka 2003, lakini kutokana na vikwazo vya Ulaya kwa Zimbabwe mkutano huo uliahirishwa mara kadhaa. Mkutano uliofanyika kwa mafanikio umeonesha kuwa Umoja wa Ulaya umekuwa na sera zenye busara kwa Afrika, umetambua kwamba katika miaka ya karibuni Afrika imekuwa na athari kubwa zaidi duniani kutokana na hali ya uchumi na siasa inavyoendelea, umaskini na hali duni sio tena dalili ya Afrika, sera za zamani za kuingilia kati mambo ya Afrika kwa kisingizio cha kuzisaidia nchi za Afrika zimepitwa na wakati, na Ulaya inapaswa kuanzisha uhusiano wa kiwenzi ulio wa usawa na Afrika ili kuhakikisha ustawi wake. Na Afrika pia imetambua kwamba ikitaka kujiimarisha ni lazima ifanye ushirikiano na nchi nyingine ikiwa ni pamoja na nchi za Ulaya. Mkutano huo wa pili umefanyika katika mazingira hayo. Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Bw. Alpha Oumar Konare alisema,

"Afrika sio bara maskini, bali lina maliasili nyingi. Ingawa barani humo bado kuna watu wengi na nchi nyingi maskini, lakini bara hili sio maskini, kwa sababu umaskini sio hatma yetu, bali ni matokeo ya uhusiano usiokuwa na usawa. Nadhani wenzetu wanaelewa ninachosema, sote tunataka kumaliza historia ya ukoloni, na Afrika haifai tena kuwa ni soko tu, mali za Afrika ni lazima zipate bei yake ya haki."

Kwa mujibu wa mpango wa ushirikiano wa wenzi wa kimkakati, mkutano wa viongozi wakuu wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya utafanyika kila baada ya miaka mitatu.