Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-11 18:32:06    
Barua 1211

cri

Msikilizaji wetu Gulam Haji Karim wa sanduku la Posta 504 Lindi,nchini Tanzania.

Ameanza barua yake kwa kutoa salamu nyingi sana, akiwa na matumaini kuwa hatujambo wote na tuna afya njema. Kwa upande wake anasema hajambo na kwa sasa amerudi kwa muda kutoka vijijini na yupo Lindi mjini,anasubiri msimu wa korosho.

Anasema pamoja na hayo, kama kawaida yake anaendelea kusikiliza matangazo ya Radio China Kimataifa. Anasema katika kipindi cha sanduku la barua cha Jumapili,Agosti 19, alisikia msikilizaji akilalamika kuhusu kutokuwa na usikivu mzuri wa matangazo ya Radio China Kimataifa katika eneo lake. Kuhusu suala hilo anasema ni kweli kwani Tanzania ni kubwa na inatofautiana na mazingira ya hali ya hewa.

Anasema yeye yupo sehemu ya kusini mwa Tanzania, ambapo matangazo anayasikia vizuri na safi kabisa na hasa kuanzia saa mbili hadi saa tatu.

Hivyo anamaliza barua yake kwa kusema atakuwa anatoa maoni kuhusu usikivu wa matangazo na vipindi vyetu mbali mbali.

Msikilizaji wetu mwingine ni David Mangwesi wa sanduku la Posta 284 Mwanza,nchini Tanzania.

Ametuandikia barua yake akiwa na matumaini kuwa sisi ni wazima na tunaendelea vizuri na shughuli zetu kama kawaida. Pia yeye anasema kama kawaida yake anaendelea kusikiliza Radio China Kimataifa, na ni mzima.

Anasema lengo la kutuandikia barua hii ni kutaka kutueleza kuwa matangazo yetu anayapata, ingawa si kwa muda mrefu, hivyo anaomba matangazo yetu ayapate kwa muda mrefu kidogo.

Kuhusu mpango wa matangazo yetu kusikika kupitia Radio Tanzania, anasema anaomba tufanye juhudi, kwani vipindi vyetu ni vizuri sana. Anasema vipindi kama vile Tujifunze kichina, Salamu na Nyimbo za asili,vinamfurahisha sana.

Pia anasema kama kuna uwezekano tuwe tunatuma maswali ya chemsha bongo mapema, kwani anapopata maswali anakuta muda wa chemsha bongo unakaribia kwisha, hivyo anashindwa kujibu kwa sababu ya kuchelewa sana. Anasema hajapata majibu yake ya chemsha bongo iliyopita.

Mwisho anaomba tumtumie vitabu na majarida ya lugha ya kichina,kwani ameanza kujua baadhi ya maneno ya kichina.

Msikilizaji wetu ni Yakub Saidi wa sanduku la Posta 124 Kakamega,nchini Kenya.

Ameanza barua yake kwa kutoa salamu kwa wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa,huku akiwa na matumaini kuwa wote ni wazima tunachapa kazi ya kuwahudumia kwa matangazo na vipindi vyetu vya kuelimisha,kutoa habari na kuburudisha. Kuhusu yeye anasema ni mzima, anaendelea na ujenzi wa taifana kusikiliza matangazo yetu.

Anawapongeza watu wa China kwa kuadhimisha miaka kumi toka China kurudisha mamlaka yake huko Hong Kong, kwa kufuata utaratibu wa nchi moja, mifumo miwili, anasema kwa hakika ni mafanikio makubwa kwa China na wakazi wa HongKong, hasa katika maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na maendeleo mbali mbali ya kujenga undugu na uhusinao wa mawasiliano ya kudumu.

Hivyo basi anapenda kuwapa pongezi wananchi wa China na wakazi wa Hong Kong kwa muelekeo huu ambao anasema ni kielelezo kizuri cha kuigwa na wengi katika kdumisha na maelewano kwa ajili ya kufanikisha maendeleo na kujiepusha kulifarakanisha taifa la China.

Anaomba mataifa mengine kuiga mfano huu wa taifa la China katika kuleta uwiano. Pia anaipongeza Radio China Kimataifa kwa mchango wake wa kujenga uhusiano mwema kwa kutangaza kwa umakini,bila kutoa habari za uchochezi. Mbali na hayo, anasema lengo la barua yake ni kutoa shukurani kwa Radio China Kimataifa kwa zawadi ya Fulana yenye nembo ya Radio China KImataifa, baada ya kupata nafasi ya tatu katika chemsha bongo,mwaka jana.

Anasema alipokea kwa furaha kubwa zawadi hiyo, na hivyo kuamua kupiga picha akiwa amevaa fulana na ametutumia picha hiyo kwa ajili ya kumbukumbu zetu

Anaomba tumtumie picha ya watangazaji wote wa idhaa ya Kiswahili na kiingereza,na ana matumaini makubwa kuwa tutajitahidi kumtumia ili awe na kumbukumbu. Pia anaomba tumtumie fulana na kofia zenye nembo ya Radio China Kimataifa ili aweze kuwapa marafiki na mashabiki ambao walifurahishwa sana na fulana tuliyomtumia. Mwisho anatutakia kheri na baraka katika kazi zetu.