Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-13 19:19:02    
Baiskeli katika maisha ya watu wa China

cri

Watu wa China wanaifahamu sana baiskeli, njia hiyo ya mawasiliano iliwahi kukuwa na hadhi muhimu katika maisha ya watu wa China. Lakini kutokana na kuinuka kwa kiwango cha maisha na kupanuka kwa maeneo ya miji mbalimbali, hadhi muhimu ya baiskeli ilianza kuchukuliwa na magari. Hata hivyo idadi kubwa ya magari imeleta matatizo mapya ya msongamamo mbaya na uchafuzi wa mazingira. Kutokana na hali hii, hadhi ya baiskeli inaanza kurudi tena katika maisha ya wakazi wa miji ya China.

Katika miaka ya 1970 na 1980, ilikuwa ni hali ya kawaida kwa wakazi wa miji ya China kutumia baiskeli. Wakati huo wageni walipotembelea mji mkuu wa China, Beijing walikuwa wanashuhudia misururu mirefu ya baiskeli kwenye barabara kuu ya Chang'an, walishangaa na kusema, "Kumbe ninyi Wachina ni wenye busara. Mnatumia baiskeli, hali ambayo inasaidia kujenga mwili na kuhifadhi mazingira."

China inajulikana kama nchi ya baiskeli. Kwa mujibu wa takwimu mpya, hivi sasa baiskeli milioni 130 zinatengenezwa kwa mwaka duniani, na asilimia 60 ya baiskeli hizo zinatengenezwa nchini China. Zaidi ya hayo kiasi matumizi ya kununua baiskeli nchini China pia kinashika nafasi ya kwanza duniani.

Bibi Hu Min aliyezaliwa katika miaka ya 70 anapenda sana baiskeli. Anasema "Nilianza kutumia baiskeli nilipokuwa mtoto, wakati huo nilikuwa na ndoto ya kufanya kazi katika shirika la posta, kwa hiyo ningeweza kutumia baiskeli kila siku."

Baadaye Bibi Hu Min alianza masoma kwenye chuo kikuu na kuhamia Beijing kutoka maskani yake, na alikuwa anaendelea kutumia baiskeli.

Anasema "Nilipokuwa mwanafunzi kwenye chuo kikuu nilijisikia vizuri nikitumia baiskeli. Miaka zaidi ya 10 iliyopita, hapa Beijing hewa ilikuwa safi. Nilitumia baiskeli kwenda kwenye mlima Xiangshan au maktaba, ama kutazama maonesho ya sanaa, sikusikia uchovu wowote, bali lilikuwa jambo la kufurahisha."

  

Bibi Hu Min alihitimu masomo mwaka 1997 na kuanza kufanya kazi, wakati ambapo alitumia baiskeli kwenda kazini na kurudi nyumbani.

Anasema "Wakati huo nilitumia baiskeli kutokana na sababu ya pesa, nilipoanza kazi nilikuwa sina pesa za kutosha. Baiskeli ilikuwa njia rahisi ya mawasiliano."

Katika miaka ya 80 na mwanzoni mwa miaka ya 90, katika miji mbalimbali ya China, wakazi wengi kabisa walikuwa wanatumia baiskeli kama alivyofanya Bibi Hu Min. Baadaye kutokana na maendeleo ya uchumi na kuinuka kwa kiwango cha maisha, watu walianza kununua magari. Mwaka 2000 Bibi Hu Min alianza kutumia gari lililotolewa na kampuni aliyofanya kazi, jambo ambalo lilimfurahisha sana.

Anasema "Wakati huo niliona ni fahari kuwa na gari, hata kama kulikuwa si mbali, nilikwenda kwa kuendesha gari, kwani niliona zaidi ya njia ya mawasiliano, kuendesha gari kulinifanya nione fahari."

Nchini China idadi ya magari binafsi inazidi kuongezeka. Katika miji mikubwa mfano wa Beijing, idadi hiyo inaongezeka kwa magari elfu moja hivi kila siku. Hadi hivi sasa Beijing ina magari binafsi milioni 3.1, lakini takwimu za miaka miwili iliyopita zinaonesha kuwa kulikuwa na magari milioni 2.5 tu. Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Beijing imekuwa ikizidi kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya mawasiliano, hata hivyo inashindwa kulingana na ongezeko kubwa la idadi ya magari. Hali kama hii pia ilionekana katika miji mikubwa mbalimbali ya China, na matokeo yake ni kuwepo kwa msongamano barabarani.

Mwaka 2004 Bibi Hu Min alipata ajira katika kampuni nyingine, yeye na mume wake walinunua gari binafsi, ambapo mume wake alikuwa anakwenda kazini kwa kuendesha gari na Bibi Hu Min alikodi teksi. Lakini msongamano barabarani ulikuwa unazidi kuwa mkubwa.

Anasema "Nilishindwa kuvumilia hali mbaya ya msongamano. Umbali wa kilomita 7 tu kati ya nyumbani kwangu na kampuni ulikuwa ukichukua saa moja kwa gari."

Ilikuwa imewadia siku ambapo ni lazima suala la msongamano wa barabarani lipatiwe ufumbuzi. Serikali na jamii zilianza kutafuta mbinu mbalimbali, zikiwemo kuzuia ongezeko la kasi la magari binafsi, kujenga mitaa ya makazi kwenye vitongoji na kuendeleza mawasiliano ya umma.

Katibu mkuu wa Shirikisho la wapanda baiskeli la China Bi. Guo Haiyan alitoa maoni yake kwamba, inatakiwa serikali iwahamasishe wananchi watumie zaidi baiskeli. Anasema "Tumetoa mapendekezo ya kutumia zaidi baiskeli katika safari za umbali mfupi na wa kati, kwani hii ni njia ya kuokoa nishati na kupunguza utoaji wa hewa zinazochafua mazingira."