Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-14 16:51:05    
Juhudi za Kampuni ya Touch Africa katika kuutangaza utamaduni na  utalii wa Afrika kwa wachina

cri

Ni mwaka mmoja sasa umepita tangu mkutano wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika ufanyike hapa Beijing. Kwenye mkutano huo uliofanyika mwezi Novemba mwaka jana, serikali ya China ilitangaza hatua nane za kuimarisha ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika na kuzisaidia nchi za Afrika kujiletea maendeleo, ambazo utekelezaji wake unaendelea vizuri katika nchi mbalimbali za Afrika. Mbali na utekelezaji unaofanywa na serikali ya China, sekta binafsi pia imekuwa inaonesha juhudi zake katika kuimarisha ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika.


Ikiwa ni sehemu ya juhudi zinazoendelea kufanywa na serikali ya China na wachina kuimarisha ushirikiano na maelewano kati ya wachina na waafrika, mwezi huu hapa Beijing, Kampuni ya Touch Africa Culture Development Co. LTD iliandaa tamasha la kwanza la kuutangaza utamaduni na utalii wa Afrika kwa wananchi wa China linaloitwa "Touch Africa". Tamasha hili lilifanyika kwenye supamaketi moja kubwa kabisa hapa Beijing, iliyopo kwenye sehemu ya magharibi ya mji wa Beijing. Mwaka 2005 tukiwa katika matembezi ya kawaida, tulipata bahati ya kutembelea supamaketi hiyo. Tukiwa ndani ya supamaketi hiyo tulibahatika kuona vibanda vya msonge. Kweli ni jambo la ajabu kuona kibanda cha msonge nchini China, hasa kwenye mji ulioendelea kama Beijing. Vibanda hivyo vilivutia ufuatiliaji wetu, na vilevile viliwavutia wachina wengi ambao wamezoea kuviona kwenye picha na televisheni tu. Watu wengi walioviona vibanda hivyo walikuwa wanavutiwa na kusogea kuangalia vimetengenezwa vipi. Lakini baada ya kufika kwenye vibanda hivyo, waliweza kuona vitu mbalimbali kama vile vinyago vya mpingo kutoka Afrika, nguo, chai nyeusi, kahawa ya Africafe na vitu vingine ambavyo viliwavutia. Hivi ni baadhi ya vitu kutoka Afrika vinavyowavutia watu hapa China.

Kampuni iliyoandaa maonesho hayo imekuwa inajihusisha na biashara, mambo ya utalii na utamaduni yanayohusu Afrika kwa miaka zaidi ya nane, na mkuu wa Kampuni hiyo Bwana Cheng Hui kila mwaka anatembelea Afrika mara tano au sita hivi. Alipokuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Bwana Cheng alisomea mambo ya sanaa, na baada ya kumaliza masomo yake alitembelea bara la Afrika. Alipokuwa huko Afrika kila alipoangalia sanaa za Afrika alivutiwa sana, na hatimaye aliamua kufanya kazi zinazohusu utamaduni na biashara kati ya China na Afrika, huo ndio mwanzo wa uhusiano kati yake na mambo ya Afrika!
Mwaka 2004 alianzisha duka la kahawa ya Afrika hapa mjini Beijing, mbali na kahawa ya Afrika, duka lake lilikuwa linauza vitu vingi vya sanaa vya Afrika. Hivi sasa ana maduka ya kahawa ya Afrika zaidi ya kumi, na pia amekuwa na maduka kadhaa ya sanaa za Afrika hapa China. Mbali na hayo, mwaka huu amepanga kujenga mtaa wa Afrika mjini Beijing. Kutokana na mpango wake, kwenye mtaa huo watalii wataweza kununua vitu vya Afrika, kula chakula cha Afrika, kunywa pombe na kahawa za Afrika na hata kina dada wa China wataweza kutengeneza nywele kama wanavyofanya kina dada wa Afrika. Pamoja na hayo Bw Cheng alizungumzia mambo yanayotatiza maendeleo ya uhusiano kati ya China na nchi za Afrika, akisema,

"Hivi sasa kuna mambo mawili makubwa ambayo yanakwamisha wachina kutalii barani Afrika. Kwanza ni kuwa wachina hawaifahamu vizuri Afrika; pili, ndege zinazokwenda Afrika kutoka China ni chache sana, hivyo bei ya tiketi ni kubwa sana ikilinganishwa na sehemu nyingine kama nchi za Asia, Ulaya na hata Amerika. Madhumuni ya maonesho hayo ni kuwasaidia wachina wengi zaidi waifahamu Afrika. Kupitia maonesho hayo, wachina waliangalia picha za mandhari na wanyama wa Afrika, walijaribu kahawa na chakula cha Afrika na kuangalia maonesho ya ngoma za Afrika".

Kama alivyosema Bw Cheng, moja kati ya tatizo lililopo kwenye ushirikiano kati ya China na Afrika, ni uelewa mdogo wa wachina wa kawaida kuhusu Afrika. Viongozi wa China wanaifahamu Afrika vizuri sana, na mara nyingi wanatembelea nchi Afrika, na mara kwa mara wanakutana na viongozi wa nchi za Afrika kwenye mikutano ya kimataifa. Kutokana na hali hiyo nchi za Afrika zimekuwa zinafanya juhudi za kutangaza vivutio vyao vya utalii kwa wachina wa kawaida, na hali hii imekuwa motomoto zaidi tangu China iziweke nchi 16 za Afrika kwenye orodha ya nchi zinazoweza kupokea watalii kutoka China. Balozi wa Kenya nchini Bibi Ruth Solitei ambaye pia alihudhuria maonesho hayo, tulipomuuliza ni juhudi gani zinafanywa na ubalozi wa Kenya kutangaza vivutio vya Kenya hapa China, alisema

Aliyosema balozi wa Kenya sio tu yanafanywa na ubalozi wa Kenya hapa China, bali pia nchi nyingine za Afrika zimekuwa zinafanya juhudi kama Kenya kutangaza vivutio vyao vya utalii kwa njia mbalimbali na kwenye miji mbalimbali ya China.
   Kwenye maonesho hayo hali motomoto ya kupenda kujua mambo ya Afrika ilioneshwa na wachina wengi. Kwenye mabanda mbalimbali yaliyokuwepo, wachina wengi walionekana kuvutiwa na mambo waliyokuwa wanayoona. Kuna waliotamani kuonja kahawa ya Ethiopia na Uganda, kuna waliopenda kujua vivutio vya utalii vya Tanzania, na hata kutaka kujua wanaweza vipi kununua mavazi ya Kiafrika. Bwana Fred kutoka Kenya mmasai ambaye alikuwa kwenye banda la Kenya alikuwa na pilikapilika nyingi za kuwaelezea watu waliokuwa wanatembelea banda la Kenya, alisema:
   Maonesho hayo yamefanyika siku chache baada ya mkutano mkubwa wa kimataifa unaohusu kuutangaza utalii kufanyika hapa Beijing. Washiriki kutoka nchi mbalimbali za Afrika waliokuja hapa Beijing, pia walitumia fursa hiyo kufanya mawasiliano na kuanzisha ushirikiano na makampuni mbalimbali ya China yanayojihusisha na mambo ya utalii.
    Hali iliyoonekana nchini China katika mwaka mmoja uliopita, inaonesha kuwa juhudi za kimataifa, kitaifa na hata juhudi za makampuni binafsi, kwa sasa zote zinahimiza ushirikiano kwenye mambo ya utalii kati ya China na nchi za Afrika, bila shaka ushirikiano huu utazidi kupiga hatua.

Idhaa ya kiswahili 2007-12-14