Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-17 15:31:31    
Mwongoza wa michezo ya kuigiza wa China, Lin Yihua

cri

Tokea mwaka 2000 "Kukutana mjini Beijing" ni tamasha la wasanii ambalo linafanyika kila mwaka katika majira ya Spring, mjini Beijing. Kwa bahati mwaka huu tamasha hilo linafanyika wakati China inapoadhimisha miaka mia moja ya mchezo wa kuigiza nchini China. Wasanii wa michezo ya kuigiza pamoja na wasanii wengine kutoka China bara, Hong Kong na Taiwan wanakusanyika mjini Beijing na wameleta michezo mingi ya kuigiza inayovutia. Mmoja kati ya wasanii hao ni Bw. Li Yihua na mchezo wa kuigiza alioleta na alioongoza uandaaji wake ni "Akina Bibi Bovary".

Bw. Lin Yihua alizaliwa Hong Kong, alianza kuandika michezo ya kuigiza alipokuwa kijana, na ni mmoja wa waanzilishi wa shirikisho kubwa la wanatamthilia wa Hong Kong. Katika muda wa miaka zaidi ya 20 iliyopita, Bw. Lin Yihua alihariri na kuongoza utengenezaji wa michezo ya kuigiza zaidi ya 40 zinazohusu mambo ya vijana, elimu, siasa na mahusiano kati ya wanaume na wanawake. Kwenye tamasha hilo Bw. Lin Yihua ameleta mchezo wa kuigiza wake mpya uitwayo "Akina bibi Bovary". Alisema,.

"Nimepata msukumo kutoka kwenye riwaya ya Kifaransa inayoitwa 'Bibi Bovary'. Hii ni riwaya iliyoandikwa na mwandishi mkubwa wa Ufaransa Bw. Gustave Flaubert miaka 150 iliyopita. Niliposoma riwaya hiyo niliona mhusika mkuu katika riwaya hiyo Bi. Bovary anafanana na baadhi ya wanawake wa siku hizi, iliibadilisha na kumfanya bibi huyo kuwa mabibi kumi na wawili wenye mavazi ya kisasa na kwa kutumia teknolojia na mawazo ya kisasa nilihariri na kuongoza utengenezaji wa mchezo huo wa kuigiza."

Miaka 150 iliyopita, mwandishi Gustave Flaubert alipokuwa anasoma gazeti moja la Ufaransa aliona habari moja ikieleza kuwa, kutokana na kuchoka na maisha ya ndoa, mwanamke mmoja alikopa pesa nyingi na kununua ovyo nguo na vifaa vya nyumbani na alikuwa na mapenzi nje ya ndoa, mwishowe mwanamke huyo alijiua kwa kunywa sumu kutokana na shinikizo kubwa la usumbufu wa mapenzi na deni kubwa. Kutokana na habari hiyo, Bw. Gustave Flaubert alitunga riwaya inayoitwa "Bibi Bovary". Mada ya riwaya hiyo inahusu maadili, matumizi ya pesa, tamaa na kifo ni mafunzo kwa wasomaji. Bw. Lin Yihua amemhamisha Bi. Bovary aliyekuwepo miaka 150 iliyopita kwenye jukwaa, na kuwaasa wanawake wachague njia ya maisha yao kwa busara, hasa wanawake wanaoishi nchini China, nchi ambayo iko katika mabadiliko makubwa ya kiuchumi. Wanawake hao wanakabiliwa na machaguo mengi ambayo yanawasumbua na yanawababaisha.

Kutokana na kubadilisha mazingira, mara jukwaa likawa darasa, mara likawa soko na mara likawa ukumbi.

Waigizaji wanasoma aya fulani anayopenda kutoka riwaya ya "Bibi Bovary" na kuonesha hisia zake huku muziki mwororo unapigwa.

Bw. Lin Yihua alikulia katika familia kubwa yenye wanawake wengi, na alikuwa na uhusiano mzuri na wanawake. Baada ya kuanza kutunga michezo ya kuigiza alianza kuchunguza masuala ya wanawake, katika tamthilia zake kadhaa alieleza fikra zake kuhusu masuala ya ndoa, furaha, heshima na haki na tamaa za wanawake. Alisema,

"Hivi leo matangazo ya biashara yanaonekana kila mahali barabarani na madukani, na mengi ya matangazo hayo yanalenga wanawake ambao ni kama Bibi Bavary. Kwa ufupi, wanawake wanaona furaha wakiwa wanapendwa na wengine, kwa hiyo wanajitahidi kujiremba, hii ni asili ya wanawake toka siku za kale, lakini tofauti na hali ya zamani ni kuwa, wanawake wa siku hizi wamekuwa na machaguo mengi ambayo hawajui wachague lipi na waache lipi, mwishowe wanakumbwa na usumbufu na hasira."

Bw. Lin Yihua ni hodari kwenye sanaa za aina nyingi, aliwahi kutunga maneno ya nyimbo, na kuandika makala za uhakiki kwa ajili ya magazeti kuhusu mambo ya fesheni. Alisema,

"Watu wengi wanataka kuonesha uwezo wao, wanaona wakiwa na mavazi au mapambo wanavutia watu na wanasikia furaha na ufahari."

Bw. Lin Yihua ana mpango wa kuhariri riwaya nne kubwa za China ya kale yaani "Safari ya Kwenda Magharibi", "Mashujaa kwenye Vinamasi", "Madola Matatu ya Kifalme" na "Ndoto kwenye Jumba Jekundu" kuwa michezo ya kuigiza. Mwaka jana tamthiliya yake ya riwaya ya "Mashujaa kwenye Vinamasi" ilioneshwa kisiwani Taiwan na ilisifiwa sana. Riwaya ifuatayo anayotaka kuhariri kuwa mchezo wa kuigiza ni "Safari ya Kwenda Magharibi".

Idhaa ya kiswahili 2007-12-17