Suala la nyuklia la peninsula la Korea bado ni suala linalofuatiliwa sana na jumuiya ya kimataifa. Kutokana na pande mbalimbali kufanya juhudi nyingi, mazungumzo ya pande sita kuhusu suala hilo yamepata maendeleo makubwa.
"Kabla ya tarehe 31 Desemba mwaka 2007 kinu cha kufanyia majaribio chenye uwezo wa megawati tano pamoja na kiwanda cha kutengenezea vifaa vya kutumia nishati ya nyuklia vitabomolewa. Kwa mujibu wa "Waraka wa Pamoja wa Tarehe 13 Februari" Korea ya Kaskazini imekubali kutoa ripoti yake kamili kuhusu mpango wa nyuklia, na Marekani itatimiza ahadi yake ya kuiondoa Korea ya Kaskazini kutoka kwenye orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi na kuanza kuondoa "sheria ya kibiashara kwa nchi adui"
Huu ni waraka wa pamoja uliotolewa baada ya mazungumzo ya tarehe 3 Oktoba mwaka 2007. Waraka huo umedhihirisha kuwa mazungumzo ya pande sita yamepata maendeleo halisi katika utatuzi wa suala la nyuklia la peninsula ya Korea. Profesa Jun Bong-geun wa taasisi ya utafiti wa hali ya usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara ya Korea Kusini hivi karibuni alipozungumza na waandishi wa habari alisema,
"Kweli ni vigumu kutatua suala la nyuklia la peninsula ya Korea, lakini mwaka huu utatuzi wake umepata maendeleo makubwa. Mazungumzo ya pande sita yamefikia 'Waraka wa Pamoja wa Tarehe 13 Februari' na 'Waraka wa Pamoja wa Tarehe 3 Oktoba' katika mazungumzo yaliyofanyika Februari na Oktoba, na pande zote zimechukua hatua, mchakato wa kutatua kabisa suala la nyuklia la peninsula ya Korea umeharakishwa."
Maendeleo hayo makubwa yamepatikana kutokana na mazungumzo ya aina nyingi na mara nyingi. China ikiwa ni mwenyeji wa mazungumzo hayo, siku zote inajitahidi kutoa mchango wake kwa ajili ya kusukuma mbele mchakato huo wa mazungumzo. Profesa Jun Bong-geun alisema,
"Kila mazungumzo yalipokumbwa na matatizo, China iliyakwamua na kuyafanya mazungumzo yaweze kuendelea. Katika siku za usoni China itaendelea kutoa mchango wake."
Baada ya "Waraka wa Pamoja wa Tarehe 3 Oktoba" kutangazwa, pande husika mara zilianza kutekeleza mambo yaliyomo ndani ya waraka huo, ahadi ya kuondoa uwezo wa zana za nyukli inatimizwa na Korea ya Kaskazini kama ilivyopangwa na kukubaliwa na pande zote. Mmoja wa maofisa wa kikundi cha Marekani cha kuondoa mpango wa nyuklia Bw. Kim Sung alisema,
"Vizuri sana, tulitembelea zana za nyuklia zilizoko mlimani tunaona kazi ya kuondoa mpango wa nyuklia imekuwa ikiendelea."
Kadiri siku ya kutoa ripoti kamili kuhusu mpango wa nyuklia inavyokaribia, jamii ya kimataifa inafuatilia sana kama mambo yaliyoandikwa kwenye 'waraka wa pamoja wa tarehe 3 Oktoba' yanaweza kutimizwa au la. Naibu mkuu wa taasisi ya utafiti wa mambo ya Japan katika Chuo cha Sayansi ya Jamii ya China Bw. Jin Xide anaona kuwa kutokana na sababu za kiufundi na za kisiasa, ni vigumu kutimiza ahadi za kuondoa kabisa uwezo wa nyuklia na kutoa ripoti kamili kuhusu mpango wa nyuklia. Alisema,
"Suala linalojitokeza hivi sasa ni la kiufundi. Kwa mfano, kabla ya hapo, pande mbalimbali zilifikiri kirahisi kazi ya kuondoa uwezo wa mpango wa nyuklia, hali ilivyo ni kwamba kazi ya kuondoa uwezo huo inahitaji muda na fedha nyingi. Pili, haiwezekani kuboresha mara moja hali ya kutoamiana kwa muda mrefu kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini."
Bw. Jin Xide alisema, suala la nyuklia la peninsula ya Korea linatakiwa kutendewa kwa utulivu na busara. Kwa mtazamo wa mbali suala hilo ni mkondo wa kihistoria, lakini utatuzi wake hautakuwa shwari. Aliendelea kusema,
"Safari ya kutatua suala la nyuklia la peninsula ya Korea ni ya kupindapinda lakini inaendelea, moja ya sababu zinazoathiri utatuzi wa suala hilo ni siasa ya Marekani, mwaka kesho Marekani itafanya uchaguzi mkuu, ingawa kutokuwepo kwa silaha za nyuklia ni mkondo mkuu, lakini safari ya kufikia lengo hilo haiwezi kukamilishwa kama iliyowekwa kwenye waraka."
Idhaa ya kiswahili 2007-12-17
|