Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-17 17:15:55    
Mtu mashuhuri katika historia ya China, Xu Xiake

cri

Bw. Xu Xiake alikuwa msafiri mashuhuri wa China katika karne ya 17, alitumia miaka zaidi ya 30 katika safari zake na aliandika kitabu chake cha "Kumbukumbu za Safari za Xu Xiake" ambacho ni kitabu muhimu kwenye utafiti wa kisayansi.

Xu Xiake alizaliwa mwaka 1586 mkoani Jiangsu, mashariki mwa China. Katika China ya kale wasomi karibu wote walifuata njia ya kushiriki mtihani wa kifalme ili wachaguliwe kuwa maofisa, lakini Xu Xiake hakuwa hivyo. Ingawa alizaliwa katika ukoo wa maofisa lakini Xu Xiake hakuwa na hamu ya kusoma na kuwa ofisa, bali alifurahia elimu kuhusu maumbile na kusafiri huku na huko kufanya uchunguzi. Kupenda kufanya hivyo kulitokana na kuathiriwa na baba yake ambaye mara kwa mara alimchukua na kwenda naye kutembelea sehemu za utalii na zenye kumbukumbu za kale. Xu Xiake alipenda kusoma, lakini vitabu alivyosoma vyote vilihusu jiografia na makala za utalii. Mama yake alikuwa mpole, alielewa vizuri mambo ambayo mtoto wake anapenda. Kwa mujibu wa mila za kale, mzazi fulani akifariki, mtoto wa kiume alipaswa kukaa karibu na kaburi kwa miaka mitatu bila kusafiri mbali. Lakini baada ya baba yake kufariki mama yake alimruhusu kusafiri, alisema mtoto wa kiume lazima awe na nia ya kujipatia mustakbali popote alipo na asizuiliwe na adha ya nyumbani. Kutokana na kuungwa mkono na mama yake Xu Xiake alitumia karibu miaka yote maishani mwake kusafiri huku na huko nchini China.

Xu Xiake alianza kusafiri alipokuwa na umri wa miaka 22 hadi alipofariki katika miaka yake ya 56, alisafiri karibu sehemu zote nchini China toka kaskazini hadi kusini na toka mashariki hadi maghharibi mwa China. Safari yake ilikuwa ngumu na ya hatari na mara kadhaa alinusurika kufa akiwa safarini, lakini alishikilia nia yake bila wasiwasi. Maneno aliyosema mara nyingi ni kuwa "Nikiwa na sepeto mkononi, naweza kujichimbia kaburi langu popote nifikapo."

Xu Xiake hakutaka kusafiri kwa kufuata njia waliyotumia wasafiri wengine, kama akipanda kwenye kilele cha mlima, ni lazima apande kile kilicho kirefu kabisa, na akienda kwenye mapango ya milima lazima aingie mapango makubwa ambayo wengine hwakuthubutu kuingia. Alikuwa haamini wengine waliyosema bali lazima ajionee mwenyewe na kisha kufanya utafiti na kuandika maoni yake kwenye daftari. Alipofanya uchunguzi mkoani Hunan alisikia fununu iliyoenea miongoni mwa wenyeji kuwa ndani ya pango moja kubwa kuna shetani na hakuna mtu yeyote aliyethubutu kuingia ndani ya pango hilo, lakini Xu Xiake hakuamini, alitaka kujionea hali ilivyo. Baada ya kuingia aligundua mawe mengi ya chokaa yiliyonying'inia kutoka kwenye paa la pango, alipotoka nje salama kutoka pango hilo wenyeji waliomsubiri kwa wasiwasi walistaajabu na kumheshimu sana. Kwenye daftari lake aliandika kuhusu mawe ya chokaa aliyoziona pangoni. Baadaye alikagua mapango mengi na aliandika mambo mengi ya ajabu aliyoyaona.

Xu Xiake alikuwa na tabia ya kusafiri mchana na kuandika hali ya safari na mambo aliyoona wakati wa usiku. Lakini bahati mbaya makala zake zaidi ya nusu zilipotea baada ya yeye kufariki, na zilizobaki zilichapishwa kwenye kitabu baada ya kuhaririwa na rafiki yake. Kitabu hicho kinaitwa "Kumbukumbu za Safari ya Xu Xiake" ambacho kina maneno zaidi ya laki nne, na kimetoa habari nyingi kuhusu hali ya hewa, mimea na wanyama, hali ya uchumi na jamii, mila na desturi, ambazo zina thamani kubwa kwa ajili ya utafiti wa mambo ya hali ya hewa na utapakaji wa aina za mimea kijiografia. Mtaalamu wa Uingereza Bw. Joseph Needham katika kitabu chake cha "Historia ya Teknolojia ya China" kuwa aliandika "Kitabu cha Kumbukumbu za Safari ya Xu Xiake hakionekani kama ni kitabu kilichoandikwa katika karne ya 17, bali kinaonekana kama ni kitabu kilichoandikwa katika karne ya 20."

Katika miaka mia kadhaa iliyopita, Bw. Xu Xiake aliheshimiwa sana na Wachina. Katika mahali alipoandika kumbukumbu zake mji wa Haining mkoani Zhejiang, serikali imeanzisha siku ya maadhimisho ya msafiri Xu Xiake, hadi sasa imefanyika kwa miaka minne, siku hiyo imekuwa tamasha kubwa la watalii wengi.

Idhaa ya kiswahili 2007-12-17