Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-18 19:19:38    
Hali ya uchaguzi mkuu unaobadilika badilika nchini Korea ya Kusini

cri

Uchaguzi mkuu wa Korea ya Kusini utafanyika tarehe 19. matokeo ya uchaguzi huo yataamua mwelekeo wa utawala na mambo ya ndani na ya nje katika kipindi cha miaka mitano ijayo, na ni uchaguzi ambao unahusu amani na utulivu wa peninsula ya Korea.

Tarehe 19 ni siku ya mapumziko kote nchini Korea ya Kusini, ili kuwapa watu nafasi ya kujitokeza kwenda kupiga kura kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni. Watu wenye haki ya kupiga kura ni milioni 37 kati ya watu wote milioni 49, wataamua nani atashika kiti cha urais kati ya wagombea 10. matokeo ya uchaguzi yatatangazwa usiku wa manane wa siku hiyo au alfajiri ya tarehe 20.

Katiba ya Korea ya Kusini inasema, rais ana madaraka ya mkuu wa taifa, mkuu wa serikali na mkuu wa jeshi, kipindi chake kuwa madarakani ni miaka mitano na haruhusiwi kuendelea kuwa rais katika kipindi kifuatacho. Kipindi cha rais wa sasa Roh Moo-hyun kitamalizika Februari mwaka kesho.

Hadi kufikia tarehe 12 Desemba utafiti uliofanywa miongoni mwa raia unaonesha kuwa, wagombea watatu wanaoungwa mkono zaidi ni Lee Myung-bak wa Grand National Party, Bw. Chung Dong-youn anayetoka United New Democratic Party, na mgombea huru Lee Hoi-chang aliyejiondoa kutoka chama cha Grand National Party mwezi Novemba. Wagombea hao wanaungwa mkono kwa kiasi cha 40%, 15% na 10%, hadi kabla ya tarehe 16 vyombo vya habari viliona kuwa Bw. Lee Myung-bak ana nafasi kubwa ya kushinda kwenye uchaguzi huo.

Lakini tarehe 16 hali ilibadilika kiajabu. Siku hiyo kanda ya video ilionesha kuwa Bw. Lee Myung-bak anajihusisha na Kampuni ya BBK. Tukio hilo lilishitusha kote nchini. Kabla ya hapo, Bw. Lee Myung-bak alikana kabisa kuwa na uhusiano wowote na kampuni hiyo ambayo iliwaletea wanahisa hasara kubwa kwa kudhibiti bei ya hisa mwaka 2001. Tarehe 5 mwezi huu, baada ya kufanya uchunguzi vyombo vya sheria pia vilitangaza kuwa Bw. Lee Myung-bak hakujihusisha na kampuni hiyo, lakini Bw. Chung Dong-youn na chama chake the United New democratic Party kinaona uchunguzi huo haukuwa wa haki na kutaka bunge lifanye uchunguzi huru kuhusu tukio hilo.

Tarehe 16 baada ya kanda ya video kutangazwa, Bw. Chung Dong-youn na Lee Hoi-chang walimtaka Lee Myung-bak ajiondoe kutoka kwenye uchaguzi. Siku hiyo Rais Roh Moo-hyun alimtaka waziri wa sheria afikiri kufanya uchunguzi wa kesi ya BBK ili kuwaondolea wasiwasi wananchi na kutoamini vyombo vya sheria. Kisha Bw. Lee Myung-bak alisema amekubali kufanyiwa uchunguzi na bunge la taifa. Bunge la Korea ya Kusini tarehe 17 lilipitisha azimio la kufanya uchunguzi upya kuhusu kesi ya BBK, na matokeo ya uchunguzi huo yatatangazwa tarehe 25 Februari mwaka kesho kabla ya rais mpya kuapishwa.

Bw. Lee Myung-bak mwenye umri wa miaka 66 anachukuliwa kama ni mwakilishi wa kundi la wahafidhina na mrengo wa kati, aliwahi kuwa meneja mkuu wa Kampuni ya Ujenzi wa Kisasa ya Korea ya Kusini na Meya wa mji wa Soeul, kutokana na ufanisi mkubwa wa kampuni yake na utawala wake aliibuka kuwa msimamizi hodari. Alisema akishinda katika uchaguzi ataimarisha uhusiano wa muungano kati ya Korea ya Kusini na Marekani na huku atabadilisha sera ya serikali ya sasa kuipendelea Korea ya Kaskazini katika misaada.

Bw. Chung Dong-youn mwenye umri wa miaka 54 anachukuliwa kama ni mwakilishi wa kundi la mrengo wa kati na la kushoto. Alipokuwa ofisa wa wizara ya Muungano alifanya juhudi nyingi kuboresha uhusiano kati ya Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini.

Bw. Lee Hoi-chang mwenye umri wa miaka 72 anachukuliwa kama ni mwakilishi wa kundi la wahifadhina, aliwahi kuwa jaji mkuu na waziri wa mambo ya ndani. Hii ni mara yake ya tatu kugombea urais, anatetea kurudisha hali ya kuaminiana kati ya Korea ya Kusini na Marekani, na kutowasiliana kiuchumi kabla ya Korea ya Kaskazini kuacha kabisa mpango wa nyuklia.

Tarehe 18 ni siku ya mwisho ya uchaguzi mkuu nchini Korea ya Kusini. Watu wanasubiri hali ya uchaguzi itakuwaje.