Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-18 19:26:14    
Barua 1216

cri

Msikilizaji wetu Ras Flanz Manko Ngogo wa Club ya wasikilizaji ya Kemogemba sanduku la posta 71 Tarime Mara Tanzania ametuletea barua pepe akisema, amefurahia sana kwa kuanzishwa kwa Chuo cha Confucius cha Radio China Kimataifa ambacho kitatoa mafunzo ya lugha ya Kichina, kwa kuwa huu pia ni mpango wa klabu yake wa kujifunza lugha za nje, kwa hivyo anaona huu ni wakati mwafaka kwa kufikia lengo lao. Yeye angefurahi sana kuona wasikilizaji wa klabu yake watakuwa wa kwanza kufikiwa na walimu wa lugha ya Kichina.

Tunamshukuru sana Bw. Ngogo kwa barua yake, kuanzishwa kwa chuo cha Confucius cha CRI kunalenga kutoa mafunzo ya lugha ya Kichina kwa wasikilizaji wake wanaopenda kujifunza lugha ya Kichina. Katika siku za baadaye kwenye kipindi chetu, mafunzo ya lugha ya Kichina yataongezwa muda, ambapo wasikilizaji wa Darasa la Confucius lililoanzishwa huko Nairobi Kenya wataweza kusikiliza matangazo yetu moja kwa moja, na klabu za wasikilizaji wetu zilizoko sehemu mbalimbali katika nchi za Afrika, kama zina uwezo wa kuanzisha darasa, zinaweza kutoa ombi la kuanzisha Darasa la Confucius kwa kufuata utaratibu uliowekwa, halafu walimu wa Kichina wataweza kutumwa kwa sehemu mbalimbali. Tunaona kazi ni kubwa, siyo rahisi kama mlivyosikiliza habari yenyewe. Lakini kwa vyovyote vile sisi tutafanya juhudi kuandaa vizuri kipindi chetu cha kutoa mafunzo ya lugha ya Kichina.

Msikilizaji wetu Gulam Haji Karim wa sanduku la Posta 504 Lindi, nchini Tanzania ameanza barua yake kwa kutoa salamu nyingi sana, akiwa na matumaini kuwa wote hatujambo na tuna afya njema. Kwa upande wake anasema hajambo na kwa sasa amerudi kwa muda kutoka vijijini na yupo Lindi mjini, akisubiri msimu wa korosho. Anasema pamoja na hayo, kama kawaida yake anaendelea kusikiliza matangazo ya Radio China Kimataifa.

Anasema katika kipindi cha sanduku la barua cha Jumapili, Agosti 19, alisikia msikilizaji akilalamika kuhusu kutokuwa na usikivu mzuri wa matangazo ya Radio China Kimataifa katika eneo lake. Kuhusu suala hilo anasema ni kweli kwani Tanzania ni kubwa na ina tofautiana na mazingira ya hali ya hewa.

Anasema yeye yupo sehemu ya kusini mwa Tanzania, ambapo matangazo anayasikia vizuri na safi kabisa na hasa kuanzia saa mbili hadi saa tatu. Hivyo anamaliza barua yake kwa kusema atakuwa anatoa maoni kuhusu usikivu wa matangazo na vipindi vyetu mbali mbali. Tunamshukuru sana Bw. Karimu kwa barua yake ya kutueleza hali ya usikivu wa matangazo yetu huko aliko. Kutokana na hali halisi, kweli sisi tunafanya juhudi ili wasikilizaji wetu wa kila sehemu waweze kusikiliza vizuri matangazo yetu, lakini kutimiza lengo bado kunahitaji muda. Ni matumaini yetu kuwa, wasikilizaji wetu watatuelewa.

Msikilizaji wetu mwingine ni David Mangwesi wa sanduku la Posta 284 Mwanza, nchini Tanzania ametuandikia barua yake akiwa na matumaini kuwa sisi ni wazima na tunaendelea vizuri na shughuli zetu kama kawaida. Pia yeye anasema kama kawaida yake anaendelea kusikiliza Radio China Kimataifa, na ni mzima. Anasema lengo la kutuandikia barua hii ni kutaka kutueleza kuwa matangazo yetu anayapata ingawa si kwa muda mrefu, hivyo anaomba matangazo yetu ayapate kwa muda mrefu kidogo. Kuhusu mpango wa matangazo yetu kusikika kupitia Radio Tanzania, anasema anaomba tufanye juhudi, kwani vipindi vyetu ni vizuri sana. Anasema vipindi kama vile Tujifunze kichina, Salamu na Nyimbo za asili, vinamfurahisha sana.

Pia anasema kama kuna uwezekano tuwe tunatuma maswali ya chemsha bongo mapema, kwani anapopata maswali anakuta muda wa chemsha bongo unakaribia kwisha, hivyo anashindwa kujibu kwa sababu ya kuchelewa sana. Anasema hajapta majibu yake ya chemsha bongo iliyopita. Mwisho anaomba tumtumie vitabu na majarida ya lugha ya kichina, kwani ameanza kujua baadhi ya maneno ya kichina.

Msikilizaji wetu ni Yakub Saidi wa sanduku la Posta 124 Kakamega, nchini Kenya ameanza barua yake kwa kutoa salamu kwa wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa, huku akiwa na matumaini kuwa wote ni wazima tunachapa kazi ya kuwahudumia kwa matangazo na vipindi vyetu vya kuelimisha, kutoa habari na kuburudisha. Kuhusu yeye anasema ni mzima, anaendelea na ujenzi wa taifa na kusikiliza matangazo yetu.

Anawapongeza watu wa China kwa kuadhimisha miaka kumi toka China irudishe mamlaka yake huko Hong Kong, kwa kufuata sera ya nchi moja mifumo miwili. Anasema kwa hakika ni mafanikio makubwa kwa China na watu wa Hong Kong, hasa katika maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na maendeleo mbalimbali ya kujenga undugu na uhusiano wa mawasiliano ya kudumu.

Hivyo basi anapenda kuwapongeza watu wa China na Hong Kong kwa mwelekeo huu ambao anasema ni kielelezo kizuri cha kuigwa na wengi katika kudumisha maelewano kwa ajili ya kufanikisha maendeleo na kujiepusha kulifarakanisha taifa la China. Anaomba mataifa mengine kuiga mfano huu wa taifa la China katika kuleta muungano.

Pia anaipongeza Radio China Kimataifa kwa mchango wake wa kujenga uhusiano mwema kwa kutangaza kwa umakini, bila kutoa habari za uchochezi. Mbali na hayo, anasema lengo la barua yake ni kutoa shukurani kwa Radio China Kimataifa kwa zawadi ya fulana yenye nembo ya Radio China Kimataifa, baada ya kupata nafasi ya tatu katika chemsha bongo, mwaka jana.

Anasema alipokea kwa furaha kubwa zawadi hiyo, na hivyo kuamua kupiga picha akiwa amevaa fulana na ametutumia picha hiyo kwa ajili ya kumbukumbu zetu. Anaomba tumtumie picha ya watangazaji wote wa idhaa ya Kiswahili na Kiingereza, na ana matumaini makubwa kuwa tutajitahidi kumtumia ili awe na kumbukumbu. Pia anaomba tumtumie fulana na kofia zenye nembo ya Radio China Kimataifa ili aweze kuwapa marafiki na mashabiki ambao walifurahishwa sana na fulana tuliyomtumia.

Tunawashukuru Bw. David Mangwesi na Bw. Yakub Saidi kwa barua zao, na ujumbe wao umewasili, hapa tunapenda kuwambia wasikilizaji wetu kuwa, idhaa yetu haina zawadi nyingi, kwa kawaida zawadi tunazopewa kutoka ofisi husika ni kwa ajili ya wasikilizaji wetu wanaopata ushindi katika mashindano ya chemsha bongo, hivyo tunashindwa kuwatumia wasikilizaji wetu zawadi nyingi ili waweze kuwapa marafiki zenu, tunaomba mtuelewe. Tafadhali waambie marafiki zako wasikilize matangazo yetu na kushiriki kwenye chemsha bongo ili nao pia wapate fursa ya kupata ushindi na kupewa zawadi.