Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-20 16:02:12    
Mchango wa baiskeli katika kupunguza msongamano barabarani

cri

Ukweli wa mambo unaonesha kuwa baiskeli ni njia rahisi ya mawasiliano katika hali ya msongamano wa barabarani. Kwa mfano mjini Beijing, kwenye kipindi pilikapilika nyingi za matumizi ya magari barabarani, magari yanakwenda kwa kasi ya wastani wa kilomita 8 hadi 12 kwa saa, wakati baiskeli zinaweza kwenda kwa kilomita 15 kwa saa.

Mtaalamu wa mazingira Bibi Zhang Lingge alitoa maoni yake kuwa, bila kujali kutumia njia ipi ya mawasiliano, watu wanaweza kufanya safari zao zisichafue mazingira. Alitoa ushauri akisema"Ukiendesha gari unaweza kutumia gari lisilotoa uchafuzi kwa wingi, unapochukua teksi unaweza kushirikiana na wengine kupanda gari moja ili kuongeza ufanisi. Zaidi ya hayo unaweza kutumia subway, mabasi ya umma, au kutumia baiskeli, ama kwenda kwa miguu. Jambo muhimu ni kuchukua njia inayofaa ya mawasiliano katika hali tofauti."

Hivi sasa Bibi Hu Min anatumia zaidi baiskeli. Alinunua baiskeli inayoweza kukunjwa. Wakati ambapo hatumii baiskeli hiyo, anaikunja na kuingia nayo kwenye gari, au kuichukua anapotumia subway au mabasi ya umma. Bibi Hu Min alizungumza mengi kuhusu urahisi wa baiskeli. "Kwa maoni yangu baiskeli ni njia nzuri ya mawasiliano kuliko nyingine. Hakuna wasiwasi wa kukumbwa na msongamano barabarani wala muda wa kusubiri teksi. Hivi sasa watu wengi wanapenda kutumia teksi, kwa hiyo inachukua muda mrefu kupata teksi. Lakini ukitumia baiskeli, unaweza kusimama wakati wowote unaopenda, kwa mfano kama hujapata kifungua kinywa, basi unaweza kupata kando ya barabara. Zaidi ya hayo, kutumia baiskeli ni njia nzuri ya kujenga mwili, kwa hiyo naweza kupunguza muda ninaotumia kwenye jumba la mazoezi."

Hivi sasa katika miji mikubwa mingi nchini China, baiskeli si kama tu ni njia ya mawasiliano, bali pia ni ishara ya mtindo wa maisha unaosaidia kujenga afya. Watu wengi wanaopenda baiskeli wameungana, wanafunga safari kwenda kwenye vitongoji kwa pamoja katika wikiendi. Bw. Zhou Bin ni kiongozi wa shirikisho moja la wapanda baiskeli.

Anasema "Sisi ni mashabiki wa kuteleza katika theluji na baiskeli. Zinapofika siku za joto, tunajadili shughuli gani tungefanya, na shughuli hizo lazima zisichafue mazingira bali zihifadhi mazingira, basi tukaamua kuanzisha shirikisho moja, tutembelee vivutio vya utalii mbalimbali vya Beijing tujionee kama kuna shughuli zinazochafua mazingira. Kwa mfano tuliona mabango ya kibiashara yaliyobandikwa ovyo ukutani, tulipiga picha na kuwaambia watu vitendo kama hivi si sahihi."

Hivi sasa wakati michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 inakaribia kufunguliwa, Beijing ukiwa mji mwenyeji wa michezo hiyo, wakazi wengi wa mji huo wameanza kutumia baiskeli ili hewa safi zaidi izidi kupatikana. Lakini watu hao wanakumbwa na tatizo kwamba, kuna njia chache za baiskeli, hata baiskeli zinapaswa kutumia njia pamoja na magari, hali ambayo ni hatari kwa waendesha baiskeli.

Bibi Hu Min anasema  "Zaidi ya hayo baadhi ya magari yanakwenda kwa kasi sana. Kutokana na hali hii, ni hatari sana kwa watu wanaotumia baiskeli."

Mkazi mwingine wa Beijing Bw. Wang Hongbin alitoa ufumbuzi wa tatizo hilo. Anasema "Naona katika sehemu kadhaa wanatumia mbinu nzuri ya kutenganisha njia ya baiskeli na ya magari kwa kutumia wigo."

Bibi Hu Min alisema hivi sasa anakwenda kazini kwa kutumia baiskeli, ni rahisi sana na inachukua nusu saa tu. Akikumbusha njia za mawasiliano alizochagua tangu aanze kutumia baiskeli hapo mwanzo, baadaye magari na hivi sasa baiskeli tena, aliona ana mengi ya kusema. "Naona watu wanaamua kutumia njia ya mawasilino kutokana na mahitaji yao. Kwa mfano kama mtu anakaa kwenye kitongoji, hawezi kwenda kazini kwa kupanda basi barabarani, hali kadhalika kwa mtu mwingine anatakiwa kumpeleka mtoto wake shuleni kila asubuhi. Kwa hiyo naona watu wanachagua njia ya mawasiliano baada ya kufikiri kwa makini. Kiuchumi, gharama za kumiliki gari huenda ni kubwa zaidi kuliko kutumia teksi. Naona si kawaida watu wakiamua kutumia njia ya mawasiliano ya umma kwa sababu tu wanaona wanapaswa kubeba wajibu kwa jamii au kuhifadhi mazingira. Kwa hiyo serikali inapaswa kutoa sera zinazowahamasisha watu watumie zaidi baiskeli au kupanda mabasi barabarani au subway."

Idara husika za serikali ya China zimetambua kuwa, baiskeli inasaidia kutimiza lengo la kujenga miji yenye mazingira mazuri na matumizi kidogo ya nishati. Kwa mujibu wa mpangilio wa mji wa Beijing kati ya mwaka 2004 na 2020, serikali ya Beijing inaona kuwa baiskeli itaendelea na hadhi muhimu miongoni mwa njia za mawasiliano ya mjini katika siku zijazo. Tarehe 22 Septemba mwaka huu, kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya kutotumia magari duniani, naibu mkurugenzi wa kamati ya mawasiliano ya serikali ya Beijing Bw. Liu Xiaoming alieleza kuwa, serikali inatunga mpango ili wakazi wapate urahisi wanapotumia baiskeli barabarani.

Anasema  "Tutaandaa hali inayofaa matumizi ya baiskeli katika mawasiliano ya mji."

Sauti ya kengele za baiskeli inayosikika barabarani inaonesha kuwa, watu wengi wameanza kutumia baiskeli, ambayo ni njia ya mawasiliano isiyochafua mazingira badala yake inajenga afya.

Idhaa ya kiswahili 2007-12-20