Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-21 15:27:58    
Mwenyekiti mpya wa Chama cha ANC asema ataendelea na sera za hivi sasa

cri

Mkutano mkuu wa Chama cha ANC ulimalizika tarehe 20 huko Polokwane, mji mkuu wa jimbo la Limpopo nchini Afrika Kusini, mwenyekiti mpya wa chama hicho Bw. Jacob Zuma kwenye mkutano na waandishi wa ahabri alisema, Chama cha ANC kitajitahidi kuondoa tofauti za ndani, kushikilia siasa iliyopo, kulinda maslahi ya wawekezaji, kupunguza umaskini, kupambana na uhalifu, kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa UKIMWI na kulinda haki za wanawake.

Jambo lilalofuatiliwa zaidi kwenye mkutano huo ni uchaguzi wa mwenyekiti mpya wa chama hicho. Kutokana na kuwa Chama cha ANC ni chama kikubwa kabisa nchini Afrika Kusini, na nafasi yake haitikisiki katika ulingo wa siasa nchini humo, vyama vingine vya upinzani haviwezi kuwa na tishio lolote katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2009, na Chama cha ANC kina desturi ya kumfanya mwenyekiti wake kuwa rais, kwa hiyo ni bayana kwamba Bw. Jocob Zuma atashinda kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2009.

Ushindani ulikuwa mkali kati ya mwenyekiti wa Chama cha ANC ambaye ni rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki, na makamu mwenyekiti wa Chama cha ANC ambaye alikuwa makamu wa rais wa Afrika Kusini Bw. Jacob Zuma. Bw. Thabo Mbeki amekuwa rais wa vipindi viwili mfululizo, kwa mujibu wa katiba ya Afrika Kusini baada ya kipindi chake cha pili kwisha, hataruhusiwa kuwa rais, lakini kama angeweza kuendelea kuwa mwenyekiti wa Chama cha ANC angekuwa na haki ya kugombea tena kiti cha urais, na Bw. Jacob Zuma kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama cha ANC, pengine anaweza kuwa rais katika uchaguzi wa mwaka 2009.

Kila mmoja kati ya watu hao wawili ana sifa zake na kundi la watu wanaomwunga mkono. Bw. Thabo Mbeki aliyepata elimu nchini Uingereza aliupatia uchumi maendeleo ya haraka kutokana na sera zake za kibiashara. Katika muda wa miaka mitano iliyopita, Afrika Kusini kwa mara ya kwanza ilipata ongezeko zaidi ya 4.5% kila mwaka katika miaka minne mfululizo, tokea mwaka 2004 pato la kila mwananchi linaongezeka kwa 4% kila mwaka. Kutokana na hayo Bw. Thabo Mbeki anaungwa mkono na watu wenye raslimali na wawekezaji kutoka nchi za nje. Lakini vyombo vya habari vinaona kuwa Bw. Thabo Mbeki hakuzingatia hali ya watu maskini kiasi cha kutosha, na raia wa kawaida hawakunufaika na ustawi wa uchumi. Hivi sasa idadi ya watu wasio na ajira inafikia 26%, na idadi ya watu ambao kwa wastani hawapati dola moja ya Kimarekani imeongezeka hadi kufikia milioni 4.2 mwaka 2005 kutoka milioni 1.89 mwaka 1996. Kinyume na hali yake, Bw. Jacob Zuma aliyezaliwa kwenye familia maskini na hakupata elimu rasmi anazingatia sana maslahi ya watu maskini, kwa hiyo anaungwa mkono na chama cha wafanyakazi. Mwishowe kwenye uchaguzi wa mkutano wa Chama cha ANC Bw. Jacob Zuma alishinda kwa kupata kura 2329 akimzidi Thabo Mbeki kwa kura 1505.

Ingawa Bw. Jacob Zuma amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Chama cha ANC, lakini hii haimaanishi kwamba hakika atakuwa rais wa Afrika Kusini. Mwaka 2005 msaidizi wa Zuma alitiwa gerezani kutokana na kupokea rushwa katika shughuli za ununuzi wa silaha kutoka Ufaransa, ingawa Bw. Zuma alisalimika bila kutiwa gerezani lakini aliondolewa na Bw. Thabo Mbeki wadhifa wa makamu wa rais. Zaidi ya hayo, kabla tukio hilo halijamalizika, mwezi Novemba mwaka huu mahakama moja ya Afrika Kusini ilibainisha kuwa Bw. Zuma anajihusisha na ufisadi unaohusika na tukio la rushwa. Kama Bw. Jacob Zuma akihukumiwa kifungo cha zaidi ya mwaka mmoja, katiba ya taifa haitamruhusu kushiriki kwenye uchaguzi wowote wa wadhifa wa kiserikali.

Wachambuzi wanaona kuwa kutokana na tofauti ndani ya Chama cha ANC kati ya Bw. Thabo Mbeki na Jacob Zuma, kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2009 hali ya siasa nchini Afrika Kusini haitakuwa na utulivu. Namna ya kusuluhisha tofauti ndani ya Chama cha ANC, kutuliza hali ya siasa, na kutekeleza sera zanazosukuma maendeleo ya uchumi, imekuwa changamoto kubwa inayokikabili Chama cha ANC.

Idhaa ya kiswahili 2007-12-21