Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-24 14:56:57    
Maingiliano ya kiutamaduni kati ya China na nchi za nje kwa mwaka 2007 yalikuwa mengi

cri

Tarehe 21 Novemba"Wiki ya Filamu ya Sri Lanka" ilianza mjini Beijing. Tofauti na filamu za Ulaya, filamu za Sri Lanka ni za aina nyingine kabisa ambazo zinawavutia watazamaji wa China kwa kuonesha mila na desturi na maisha ya kidini ya watu wa Sri Lanka.

Mliyosikia ni sauti ya filamu ya Sri Lanka "Uppalawanna". Filamu hiyo inaeleza mapenzi matamu na ya huzuni kwamba mtawa mrembo Uppalawanna anayependana na mwalimu mmoja wa ngoma, lakini mapenzi yao yalipingwa na wazazi wa Uppalawanna na kusababisha mambo mengi ya kuhuzunisha. Filamu hiyo inaeleza hadithi pole pole na inaonesha sana maisha ya kidini.

Huu ni mwaka wa 50 tokea China na Sri Lanka zianzishe uhusiano wa kibalozi. Mwaka huu 2007 nchi hizo mbili zimekuwa na maingiliano mengi ya kiutamaduni, na kwa mara ya kwanza zimesaini makubaliano ya ushirikiano kuhusu filamu, wiki ya filamu ya Sri Lanka ni moja ya shughuli za ushirikiano huo. Balozi wa Sri Lanka nchini China Bw. Amunugama alisema, ili kuwawezesha Wachina Sri Lanka wajue zaidi, walichagua vizuri filamu za kuoneshwa katika wiki hii. Alisema,

"Tulitafakari sana tuchague filamu gani za kuwaonesha Wachina. Filamu hiyo ni filamu mpya, tunatumai kuonesha filamu nyingi ili kuwafahamisha Wachina kuhusu Sri Lanka kutoka pande mbalimbali. Filamu hiyo imewakilisha hisia zetu na mila zetu, tunatumai watazamaji wa China wataipenda."

"Wiki ya Filamu ya Sri Lanka" ni moja tu kati ya maingiliano mengi ya kiutamaduni kati ya China na nchi za nje. Katika mwaka huu 2007 nchi nyingi zilifanya mwaka wa utamaduni nchini China, na kupitia shughuli za maonesho ya michezo ya sanaa, wiki za filamu na maonesho ya muziki, Wachina wamezidi kuzifahamu nchi hizo. Mwezi Aprili, shughuli za "Spring ya utamaduni wa Ufaransa" zilifanyika katika miji ya Beijing, Shanghai, na miji mingine 14, kwa ujumla na zilifanya michezo ya sanaa kwa mara zaidi ya mia moja katika miji hiyo. Baadaye Japan na Korea ya Kusini zilifanya maonesho ya filamu, vitu vya sanaa na makongamano, kisha shughuli za "Mwaka wa Utamaduni wa Hispania" zilifanyika na ziliwaletea Wachina dansi ya Flamenco na maonesho ya picha za kamera. Tarehe 17 Oktoba "Mwaka wa Utamaduni wa Ugiriki" umeanzishwa nchini China, maonesho ya sanaa za kisasa za Ugiriki yakiwa kama ufunguzi wa mwaka huo yalifanyika katika jumba la makumbusho la Beijing, vitu vilivyooneshwa katika ufunguzi huo ni pamoja na picha za kuchorwa na sanamu zilizofinyangwa. Mwanafunzi wa shahada ya pili wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha China Bw. Yang Ce alisema,

"Mimi sio msanii, lakini baadhi ya picha na sanamu zilizofinyangwa zinafusa sana hisia zangu. Ni ajabu kwamba unapokuwa na mawazo mengi, unaweza kutulia kwa kuangalia sanaa hizo."

Licha ya maonesho katika jumba la makumbusho la Beijing serikali ya Ugiriki ilikodi nyumba karibu na kasri la kifalme la Beijing, kuonesha picha za utamaduni wa nchi yake, ili Wachina waweze kuielewa nchi hiyo kutoka kila upande.

Sambamba na maonesho ya utamaduni ya nchi za nje kufanyika nchini China, China pia inafanya maonesho ya utamaduni wake katika nchi za nje. Mwezi Septemba, China na Russia zilifanya "Safari ya Mto Volga". Wasanii wa China walianza safari yao kutoka Moscow, walionesha michezo yao ikiwa pamoja na opera ya Beijing, sarakasi, muziki, dansi na maonesho ya vitu vya sanaa za ufundi wa mikono katika miji 11 iliyo karibu na mto huo. Mwezi Oktoba, China ikiwa mgeni rasmi ilishiriki kwenye tamasha la kimataifa la Cerbantino, ambalo ni tamasha kubwa katika Latin Amerika.

Meneja mkuu wa Kampuni ya Kuonesha Maonesho ya Michezo ya Sanaa katika Nchi za Nje Bi. Song Lihong alisema, kutokana na nchi mbalimbali kuvutiwa na utamaduni wa China, China ilialikwa kufanya maonesho mengi nchi za nje. Alisema,

"Shughuli za utamaduni wa China zilikuwa nyingi, kutokana na shughuli hizo watu wa nchi za nje wanaielewa zaidi China. Watu wa nchi za nje wana hamu ya kuijua China pamoja na historia yake na sanaa zake. Opera ya Beijing hapo kabla ilikuwa ni shida kuoneshwa katika nchi za nje, sasa hali imebadilika."

Bi. Song Lihong alieleza, Japan na Korea ya Kusini, nchi ambazo zina athari kubwa ya utamaduni wa China, kila mwaka zinakaribisha makundi mengi ya opera ya Beijing kufanya maonesho. Katika nchi za Magharibi, opera ya Beijing na opera ya Kunqu zinawavutia watazamaji kutokana na utamaduni na uungwana wa michezo hiyo.

Licha ya kuwa opera hizo za jadi, zimewapa kumbukumbu nzuri watazamaji wa nchi za nje, filamu zaidi ya 600 zilizooneshwa katika nchi zaidi ya 39 mwaka huu, pia zimewavutia sana. Kati ya filamu hizo, zaidi ya 20 zilizopigwa chini ya vijana zilipata tuzo zaidi ya 50 za kimataifa. Mkurugenzi wa ofisi ya maingiliano ya kimataifa katika Idara ya Taifa ya Filamu Bw. Luan Guozhi alieleza kuwa, pamoja na filamu nyingi za China kuoneshwa nchi za nje, mafanikio makubwa yamepatikana katika ukusanyaji fedha, ushirikiano wa hadithi za filamu na uenezi wa filamu. Alisema,

"Tunahamasisha kutengeneza filamu kwa ushirikiano na nchi za nje na kuzisambaza kwa kusaidiwa na nchi za nje. Mwaka huu hadi sasa tumetengeneza filamu 35 kwa ushirikiano, filamu hizo sio tu zinaoneshwa sana nchini China bali pia ni filamu muhimu zinazooneshwa nchi za nje."

Mpaka sasa, filamu 27 za China zimeuzwa kwa thamani ya Yuan bilioni mbili nchi za nje. Hizo ni pesa nyingi kuliko miaka yote iliyopita.

Aidha, picha na sanamu zilizofinyangwa pia zinauzwa kwa bei nzuri nchi za nje. Hivi karibuni, kwenye "mnada wa vitu vya sanaa za kisasa" uliofanyika huko Hong Kong "muswada wa picha 14 za sherehe ya fataki" uliuzwa kwa dola za Hong Kong milioni 74.24. Msimamizi mkuu wa Maonesho ya Kimataifa ya Picha ya China Bw. Dong Mengyang anaona kuwa katika miaka ya hivi karibuni sanaa za wasanii wa siku hizi wa China zinavutia sana wahifadhi wa sanaa wa nchini na nchi za nje. Alisema,

"Kwenye mnada wa Sotheby mjini New York, picha ya Fang Lijun iliuzwa kwa dola za Kimarekani zaidi ya milioni nne. Wasanii kama huyo ni wawakilishi wa fikra za vijana wa China ya leo. Watu wa nchi za nje kwa muda mrefu wanawafuatilia hali yao na thamani ya sanaa zao inapanda haraka, wakiona kuwa sanaa zao zinawakilisha fikra za Wachina wa zama hizi."

Michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008 inakaribia siku baada ya siku, mjini Beijing na kwengineko nchini China yatakuwa na maonesho mengi ya utamaduni kuoneshwa nchini China na China pia itafanya maonesho mengi nchi za nje.

Idhaa ya kiswahili 2007-12-24