Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-24 15:06:01    
Usafiri wa Bahari katika China ya Kale

cri

China ni nchi yenye mwambao mrefu. Katika historia, China iliwahi kuongoza katika usfiri wa bahari duniani.

Katika dunia yetu eneo la bahari ni kubwa sana kuliko eneo la nchi kavu, binadamu walianza kushughulika na mambo ya bahari toka zamani. Hadithi kuhusu usafiri wa bahari iliyoenea sana nchini China ilitokea katika karne ya tatu.

Mwaka 221 K.K. mfalme Qinshihuang wa Enzi ya Qin aliyateka madola mengi madogo madogo na kuunda nchi ya kwanza yenye muungano katika historia ya umwinyi ya China. Ili kupata dawa ya kuishi milele, mfalme huyo alimtuma mganga Xu Fu aongoze msafara wake wa merikebu kwenda kwenye mlima wenye miungu kutafuta dawa ya kuishi milele. Msafara wake wenye watu wanaume na wanawake na mafundi zaidi ya elfu moja ulisafiri na mbegu za mazao. Msafara huo ulielekea mashariki, upande ambao jua linachomoza, lakini haukurudi. Wataalamu wa historia walithibitisha kuwa mahali msafara huo ulipofika palikuwa ni visiwa vya Japan, na watu hao walikuwa wakazi wa mwanzo kabisa katika visiwa hivyo. Hivi leo hadithi nyingi za mapokeo nchini Japan zinahusika na msafara wa Xu Fu.

Hadithi kuhusu Xu Fu imeeleza hamu kubwa ya watu wa China ya kale kutaka kufahamu jinsi bahari ilivyo. Lakini katika zama ambazo sayansi na teknolojia zilizokuwa nyuma na binadamu hawakuwa na elimu ya bahari, usafiri wa bahari ulikuwa ni ndoto tu.

Usafiri wa bahari ulikuwa umepiga hatua kubwa kabla na baada ya kuzaliwa kwa Kristo. Na usafiri huo ulikuwa ni njia ya hariri baharini. Kwa mujibu wa maandishi ya Enzi ya Han ya China "Jiografia", katika karne ya kwanza China ilipokuwa katika Enzi ya Han ilikuweko njia moja ya biashara iliyoanzia kaskazini magharibi mwa China kupitia Asia ya Kati na kufikia Ulaya. Pamoja na njia hiyo, pia kulikuwa na njia nyingine ya biashara baharini. Njia hiyo ilianzia bandari ya Xu Wen mkoani Guangdong na kufikia Viet Nam, Thailand, Myanmar, India, Sri Lanka, na kutoka hapo bidhaa za hariri za China zinasafirishwa kwenda Ulaya na Afrika.

Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, watu wa China walikuwa wamefahamu zaidi elimu ya usafiri wa bahari. Katika karne ya tisa, Wachina walivumbua dira. Uvumbuzi huo ulileta maendeleo makubwa kwa usafiri wa baharini. Katika kipindi hicho, watu wa China walikuwa wamefahamu pepo za msimu na walikuwa na elimu kuhusu sura ya nchi chini ya bahari, na vitabu vingi kuhusu elimu ya bamvua.

Katika karne ya 15 safari za baharini nchini China zilikuwa zimepamba moto. Katika kipindi hicho alitokea msafiri mkubwa wa bahari Zheng He.

Zheng He jina lake la awali ni Ma Sanbao, kutokana na kuagizwa na mfalme wake, aliongoza msafara mkubwa wa merikebu na kusafiri mara saba katika muda wa miaka 28 kuanzia mwaka 1405. safari zake zilimfikisha kwenye mwambao wa Afrika Mashariki na nchi zaidi ya 30 za Asia.

Katika zama za Zheng He China ilikuwa ikiongoza katika utengenezaji wa merikebu. Merikebu aliyotumia Zheng He ilikuwa kubwa na yenye vifaa vya kisasa kwa wakati ule. Mpini wa usukani wa merikebu uliofukuliwa kwenye magofu ya kiwanda cha kutengenezea merikebu karibu na mji wa Nanjing una urefu wa mita 12. Kutokana na urefu huo, merikebu iliyotumia mpini huo wa usukani ilikuwa na uwezo wa kupakia mizigo zaidi ya tani elfu moja ambayo hakika ilikuwa kubwa kabisa duniani katika zama hizo.

Safari za Zheng He ziliimarisha maingiliano ya utamaduni na biashara, urafiki na maelewano kati ya China na ng'ambo. Kutokana na sababu hizo, hadi sasa katika nchi nyingi za Asia ya Kusini Mashariki bado kuna mahekalu ya kumkumbuka Zheng He na barabara zilizopewa jina la Zheng He.

Katika Enzi ya Qing (1616?1911) iliyofuata Enzi ya Ming aliyoishi Zheng He usafiri wa bahari haukuwa na maendeleo. Lakini jambo linalostahili kutajwa ni kuwa mwaka 1661 jemadari Zheng Chenggong aliongoza askari wake kuvuka bahari na kupambana na wakoloni wa Uholanzi katika kisiwa cha Taiwan kwa miezi minane, na mwishowe aliwafukuza na kurudisha kisiwa hicho kilichokaliwa na wakoloni wa Uholanzi kwa miaka 38.

Idhaa ya Kiswahili 2007-12-24