Rais Hamid Karzai wa Afghanistan alikuwa na shughuli nyingi katika wikiendi iliyopita, tarehe 22 na 23 mwezi Desemba alikuwa na wageni watatu waheshimiwa wa nchi za magharibi ambao nni rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa, waziri mkuu wa Australia Bw, Kevin Rudd na waziri mkuu wa Italia Bw Romano Prodi. Ni kwanini wakuu hao watatu wa nchi za magharibi waliitembelea ghafla Afghanistan kwa hivi sasa? Vyombo vya habari vinaona, kuna sababu mbalimbali.
Kwanza, sikukuu ya Krismasi, ambayo ni sikukuu kubwa kwa nchi za magharibi inakaribia, wakuu hao watatu wanataka kutoa salamu na kuwapa moyo wanajeshi walioko mstari wa mbele kwenye mapambano dhidi ugaidi. Katika ziara zao fupi, wakuu hao watatu wote walikwenda kuwaangalia askari wa nchi zao walioko nchini Afghanistan.
Pili, ni kutokana na utashi wa mambo ya kisiasa kwenye nchi zao. Katika miaka miwili iliyopita, askari zaidi ya 330 wa nchi za nje walipoteza maisha yao nchini Afghanistan, jambo ambalo lilifunika kivuli kwa nchi zilizotuma majeshi nchini Afghanistan, watu wa nchi hizo wanataka serikali zao ziondoe askari wake kutoka Afghanistan. Kutokana na hali hiyo, ziara za wakuu hao watatu zinaonesha wao kuzingatia suala la Afghanistan, na kupunguza malalamiko ya nchini mwao kwa kutumia nafasi hiyo.
Tatu, ni hali mbaya ya usalama nchini Afghanistan. Wakuu hao watatu wanaona wasiwasi kuhusu msukosuko wa nchini Afghanistan, wanatarajia kufanya utafiti na kufahamu hali halisi ya huko ili kurekebisha sera za serikali zao kuhusu Afghanistan, kuonesha uungaji mkono thabiti kwa serikali ya Afghanistan na kuondoa wasiwasi wa rais Hamid Karzai. Hivi sasa, jumla ya idadi ya askari wa majeshi ya nchini mbalimbali walioko nchini Afghanistan ni kiasi cha elfu 50, kiasi hicho ni mara 3 kuliko kile cha miaka minne iliyopita. Lakini idadi kubwa ya askari walioko nchini Afghanistan haikuboresha hali ya usalama ya nchi hiyo. Mjumbe maalumu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia suala la Afghanistan Bw. Tom Koenigs, tarehe 15 mwezi Oktoba kwenye taarifa aliyoitoa kwa baraza la usalama alisema, tokea mwaka huu, matukio ya mashambulizi ya kimabavu yameongezeka kwa kiasi cha 30% kuliko yale ya mwaka jana, na kusababisha vifo vya watu zaidi ya elfu 6. Tarehe 14 mwezi Desemba, waziri wa ulinzi wa Australia, Bw. Joel Fitzgibbon kwenye mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa nchi 8 uliofanyika huko Edinburgh, Uingereza, alionya kuwa kama NATO haitabadilisha sera zake na kukagua mipango ya kijeshi na maisha ya wananchi watashindwa katika vita hiyo. Tarehe 21 mwezi Desemba, rais Hamid Karzai alisema, Afghanistan ilikumbwa na uharibifu mkubwa, nchi yake inatakiwa kufanya ukarabati kwa muda mrefu zaidi kuliko ilivyokadiriwa, kwa uchache Afghanistan inahitaji uungaji mkono wa majeshi ya nchi za nje katika miaka 10 ijayo. Hivyo, katika ziara yao viongozi wa nchi hizo tatu waliahidi kutoa uungaji mkono wa muda mrefu wa kisiasa, kijeshi na kifedha kwa serikali ya Afghanistan. Katika mazungumzo na rais Karzai, rais Sarkozy alisisitiza kuwa, nchi zao hazijafikiria kuondoa askari, alisema Ufaransa inanuia kufanya uamuzi katika wiki chache zijazo kuhusu kuongeza askari nchini Afghanistan. Waziri mkuu wa Australia, Bw. Kevin Rudd alisema, jeshi la Australia litakaa nchini Afghanistan kwa muda mrefu, alisema atazihimiza nchi nyingine ziendelee kubeba na kuongeza wajibu wao kuhusu Afghanistan, alitangaza kuwa Australia itatoa msaada wa dola za kimarekani milioni 95 kwa Afghanistan, ambao utatumika katika ukarabati wa mkoa wa Uruzgan. Bw. Romano Prodi katika mazungumzo kati yake na rais Karzai alisema, Italia itaendelea kutoa uungaji mkono wa muda mrefu kwa Afghanistan.
Ziara za viongozi hao watatu pia zinakusudia kuionesha Marekani uungaji mkono wao kwa mshirika wao. Rais George Bush wa Marekani tarehe 20 mwezi Desemba kwenye mkutano na waandishi wa habari, alisema wasiwasi wake mkubwa kuhusu suala la Afghanistan ni nchi wanachama wa NATO kuondoa askari wao kutoka Afghanistan.
|