Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-25 16:05:50    
Uvumbuzi wa kujitegemea wa viwanda vya magari nchini China

cri

Katika miaka zaidi ya 10 iliyopita, viwanda vya magari nchini China vinaendelezwa kwa kasi, na vimekuwa nguzo ya uchumi wa taifa la China. Baada ya kuingia katika karne ya 21, serikali ya China imechukua hatua mbalimbali kuunga mkono kazi ya kufanya uvumbuzi wa kutengeneza magari ya aina mpya kwa kujitegemea, na uwezo wa uvumbuzi wa viwanda vya magari nchini China unaimarishwa siku hadi siku.

Watu wengi wanafikiri kuwa sifa ya magari yanayotengenezwa na China sio nzuri, na haiwezi kulingana na magari yenye chapa maarufu duniani. Lakini katika miaka ya hivi karibuni, magari yanayotengenezwa na China yanaendelezwa kwa kasi. Muda mfupi uliopita, gari la milioni 1 lilitengenezwa na kampuni ya magari ya Chery mkoani Anhui, China. Hii inamaanisha kuwa kampuni ya Chery imetimiza lengo la kuvumbua chapa maarufu. Hivi sasa kampuni hiyo inachukua zaidi ya asilimia 7 kwenye soko la magari nchini China, na kuchukua nafasi ya nne katika viwanda vya magari nchini China, na uuzaji wa magari madogo kwa nje pia unachukua nafasi ya kwanza nchini China kwa miaka minne mfululizo.

Meneja mkuu wa kampuni ya magari ya Chery Bw. Yin Tongyao alisema, miaka 10 tangu kampuni hiyo ianzishwe, siku zote inashikilia wazo la kufanya uvumbuzi kwa kujitegemea. Alisema katika ushindani mkubwa wa soko, kampuni hiyo inaimarisha utafiti wa injini na vipuri muhimu vya magari, ili kuimarisha nguvu kubwa ya ushindani. Alisema,

"Utafiti wa injini hizo unaleta manufaa makubwa kwetu. Tunaweza kuendeleza magari ya aina mbalimbali. Hivi sasa tuna injini, injini zinatuletea faida kubwa, kwani zinaweza kuuzwa zikiwa bidhaa za mwishoni. Sasa viwanda vingi vinataka kununua injini zetu, hata tunakaribia kushindwa kukidhi mahitaji."

Baada ya maendeleo ya miaka 10, kampuni ya Chery imekuwa na uwezo wa utafiti wa magari, injini na baadhi ya vipuri muhimu, na inaweza kutengeneza magari laki 6.5 na injini laki 4 kila mwaka. Kampuni hiyo pia ni kampuni ya magari ya kwanza inayouza magari, injini na teknolojia za utengenezaji na zana za magari kwa nchi za nje.

Meneja wa kampuni ya FIAT ya Italia, ambayo ni kampuni maarufu wa utengenezaji wa magari, Bw. Govanni Bartoli alitembelea kampuni ya Chery muda mfupi uliopita kwa ajili ya kununua injini. Aliona kuwa, injini zinazotengenezwa na kampuni ya Chery ni nzuri sana, alisema.

"Tunataka kutafuta mwenzi mzuri wa ushirikiano, na kutaka kununua injini nzuri hapa. Hii ni sababu yetu ya kuja hapa kwenye kampuni ya Chery. Injini za Chery zinatengenezwa vizuri, na zinaweza kuboreshwa na kuwekwa kwenye magari yetu."

Katika miaka ya hivi karibuni, uzalishaji wa magari nchini China unaongezeka kwa asilimia 25 kila mwaka, na mwaka jana ulifikia magari milioni 7.2, ambao ulichukua nafasi ya tatu duniani baada ya Marekani na Japan.

Kadiri viwanda vya magari vya China vinavyoendelezwa kwa kasi, ndivyo magari yenye hakimiliki ya ubunifu ya China yanavyoongezeka siku hadi siku. Naibu mkurugenzi wa shirikisho la viwanda vya magari la China Bw. Zhang Xiaoyu alifahamisha kuwa,

"Serikali ya China sio tu inavitaka viwanda vya magari viongeze uzalishaji wa magari, bali pia inavitaka viwe na uwezo wa uvumbuzi, na kuvifanya kuwa viwanda vinavyoiwezesha maendeleo makubwa katika kustawisha utengenezaji wa mitambo. Kuanzia sera ya viwanda ya mwaka 1994 hadi sera ya maendeleo ya viwanda vya magari ya mwaka 2004, zote zinasisitiza uvumbuzi wa viwanda vya magari. Katika upande wa sera na fedha, serikali imetoa uungaji mkono mkubwa na sera kwa ajili ya kuhimiza uvumbuzi wa viwanda hivyo."

Imefahamika kuwa idara husika za China zinatoa uungaji mkono mkubwa katika utafiti wa teknolojia ya kimsingi na teknolojia ya elektroniki yenye nguvu kubwa ya ushindani katika viwanda vya magari, na kutoa unafuu katika utozaji kodi kwa viwanda ambavyo vina miradi ya sayansi na teknolojia. Katika uungaji mkono wa serikali na juhudi za viwanda, viwanda vya magari nchini China vimemiliki baadhi ya teknolojia muhimu za utengenezaji wa magari. Katika viwanda vya magari ya ngazi ya juu, zamani China ilitegemea kuingiza teknolojia na kufanya ubia, katika miaka ya karibuni magari ya ngazi ya juu yenye chapa za China na hakimiliki ya ubunifu ya China yameanza kuongezeka kwa kasi, hivi sasa yanachukua asilimia 30 kwenye soko. Katika viwanda vya magari ya biashara kama vile malori ya mizigo na magari ya abiria, magari yenye hakimiliki ya ubunifu ya China yamechukua asilimia 80 kwenye soko.

Wataalam wamesema, baada ya China kujiunga na Shirika la Biashara Duniani, kwa kuwa sehemu ya magari yenye hakimiliki ya ubunifu ya China kwenye soko zinaongezeka kwa kasi, hivyo magari yanayoagizwa kutoka nje hayajaongezeka kwa kiasi kikubwa, lakini magari yanayouzwa nje yameongezeka kwa kiasi kikubwa. Takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2006 magari ya China yaliyouzwa nchi za nje yaliongezeka kwa mara 10 kuliko mwaka 2000.

Lakini viwanda vya magari nchini China pia vinakabiliwa na changamoto nyingi katika maendeleo yake. Katika upande wa matumizi ya teknolojia ya umeme ya magari, China bado ina tofauti kubwa ikilinganishwa na kiwango cha kisasa cha kimataifa, na maendeleo ya viwanda vya magari nchini China pia yanakabiliwa na changamoto za nishati na mazingira. Naibu mkurugenzi wa shirikisho la viwanda vya magari la China Bw. Zhang Xiaoyu alisema, ili kubana matumizi ya nishati na kupungua uchafuzi, China inaweka sera mbalimbali na kuchukua hatua ili kuhimiza viwanda kufanya utafiti wa magari yanayoweza kubana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira. Alisema,

"Kuanzia mwanzo wa utafiti hadi kuuza bidhaa kwenye soko, taifa linapaswa kutekeleza sera mbalimbali ili kuunga mkono magari yenye hakimiliki ya ubunifu yanayotumia nishati mpya na kupunguza utoaji wa hewa chafu. Uungaji mkono wa nchi katika fedha na utozaji kodi, hadi mwishoni katika ununuzi wa serikali, sera wazi ya nchi ni kununua magari yenye hakimiliki ya ubunifu ambayo yanatumia nishati kidogo na kutoa hewa chafu ndogo.

Bw. Zhang Xiaoyu alidokeza kuwa, kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2010, China imepanga kutenga Yuan za RMB bilioni 1.5 kuunga mkono utafiti na utengenezaji wa magari yanayobana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira. Hatua hiyo itahimiza kwa ufanisi utengaji fedha wa viwanda vya utengenezaji wa magari nchini China katika upande huo.

Idhaa ya kiswahili 2007-12-25