Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-26 15:27:14    
Waziri mkuu wa Japan anata kusukuma uhusiano kati ya Japan na China kwenye kipindi kipya

cri

Waziri mkuu wa Japan Bw. Yasuo Fukuda atakayefanya ziara nchini China, tarehe 25 alipokutana na waandishi wa habari wa China nchini Japan alisema, anataka kusukuma mbele uhusiano kati ya Japan na China kwenye kipindi kipya na kuufanya mwaka wa kesho uwe wa kupiga hatua kubwa ya maendeleo kwenye uhusiano kati ya Japan na China.

Bw. Yasuo Fukuda alisema, anaona furaha kwa kuweza kufanya ziara nchini China katika mwaka wa 35 tangu Japan na China zianzishe uhusiano wa kibalozi. Wakati wa ziara yake nchini China Bw. Fukuda atakutana na rais Hu Jintao, waziri mkuu Wen Jiabao na kufanya nao mazungumzo kuhusu kuanzisha uhusiano wa kimkakati wa kunufaishana pande mbili na kutoa mchango kupitia ushirikiano wa nchi mbili na wa kikanda.

Bw. Fukuda alisema hivi sasa takriban watu milioni tano wa pande mbili wanawasiliana kila mwaka, maingiliano na maelewano kati ya nchi hizo mbili yanasaidia kuimarisha urafiki kati ya nchi hizo mbili. Alisema, uhusiano mzuri kati ya Japan na China sio tu unanufaisha nchi zote mbili, na pia ni muhimu kwa amani na ustawi wa kiuchumi katika kanda ya Asia na Pasifiki. Watu wa Japan na China wana majukumu makubwa na wanapaswa kufanya juhudi kwa ajili ya kutimiza majukumu hayo. Kutokana na ufahamu huo, Japan ingependa kuendeleza zaidi uhusiano wa siku za usoni unaojengwa kwa kuelewana na kuaminiana zaidi kati ya Japan na China.

Aidha Bw. Fukuda alisema, Japan itazingatia historia yake kwa unyenyekevu na kuendelea kwenye njia ya nchi ya amani, na juu ya msingi huo kuendeleza uhusiano wa siku za usoni kati ya Japan na China na kusukuma mbele maingiliano na mazungumzo katika sekta mbalimbali na ngazi mbalimbali, na hasa kati ya vijana wa nchi hizo mbili. Kutokana na hayo, serikali ya Japan imekuwa ikifanya juhudi kwa ajili ya kuimarisha maelewano na imani kati ya nchi hizo mbili. Alisema mwaka huu ni "mwaka wa maingiliano ya utamaduni na michezo kati ya Japan na China", mwezi Septemba shughuli nyingi za "tamasha la utamaduni wa jadi wa China na Japan" zilifanyika mjini Beijing, na mwaka kesho ni mwaka wa kuadhimisha miaka 30 tokea "Mkataba wa Amani na Urafiki wa Japan na China" usainiwe, na nchi zote mbili zimekubali kuufanya mwaka kesho uwe mwaka wa "Maingiliano ya Kirafiki kati ya Vijana wa Japan na China", na ana matumaini kuwa mwaka huo utakuwa mwaka wa kupiga hatua kubwa katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Kuhusu namna ya kuweka uhusiano wa kimkakati wa kunufaishana pande mbili Bw. Fukuda alisema, kutokana na ziara aliyofanya Bw. Shinzo Abe nchini China mwezi Oktoba mwaka jana, mwezi Aprili waziri mkuu Wen Jiabao alifanya ziara nchini Japan, uhusiano kati ya Japan na China umekuwa ukiendelea vizuri. Ili kuufanya uhusiano wa kimkakati uwe wa kuzinufaisha nchi hizo, ni muhimu kwa viongozi wa nchi hizo mbili kutembeleana na kuanzisha uhusiano wa imani. Alisema, atajadiliana na viongozi wa China kuhusu mustakbali wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili, maendeleo ya maliasili kwenye Bahari ya Mashariki, suala la peninsula ya Korea na mabadiliko ya hali ya hewa. Alisema ustawi wa uchumi wa China ni fursa nzuri kwa Japan na jumuyia ya kimataifa, na hasa kwa maendeleo ya uchumi wa Japan.

Bw. Fukuda alisema wakati wa ziara yake nchini China atatembelea maskani ya Confucius. Alisema hivi sasa mji wa Tianjin ni moja ya miji muhimu ya kuendeleza uchumi, na una uhusiano mkubwa na uchumi wa Japan, anataka kujionea uchumi unavyoendelea, na kusema fikra za Confucius zinaathiri sana kwa nchi za Asia ikiwemo Japan. Alisema inafaa kufahamu historia na utamaduni wa nchi, ili kustawisha uhusiano katika shughuli za kidiplomasia.

Idhaa ya kiswahili 2007-12-26