Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-26 20:49:59    
Serikali ya China yatoa waraka "Hali na Sera ya Nishati ya China"

cri

Ofisi ya habari ya baraza la serikali ya China tarehe 26 mwezi Desemba ilitoa waraka "Hali na Sera ya Nishati ya China" ukieleza hali, mkakati na lengo la maendeleo ya nishati ya China. Waraka wa serikali unasema, katika miaka ya hivi karibuni harakati za kuokoa nishati zilipata ufanisi mkubwa, vitu vya uchafuzi vinavyotolewa vimeweza kudhibitiwa. Katika siku za baadaye China itaendelea kuhimiza uokoaji wa nishati, kuendeleza matumizi ya nishati endelevu na kujenga mfumo wa nishati ulio tulivu, safi, salama na wenye kubana matumizi.

Huu ni waraka uliotolewa kwa mara ya kwanza na serikali ya China katika miaka ya hivi karibuni kuhusu hali na sera ya nishati. Waraka wa serikali umetoa maelezo kamili kuhusu hali ya maendeleo ya nishati, mkakati na lengo la maendeleo ya nishati, kuendeleza uokoaji wa nishati, kuinua uwezo wa utoaji wa nishati, kuhimiza maendeleo yenye uwiano ya sekta ya nishati na hifadhi ya mazingira pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa wa eneo la nishati.

Waraka wa serikali unasema, tokea mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita, sekta ya nishati ya China ilipata maendeleo ya kasi, na utoaji nishati ulichukua nafasi ya pili duniani. Kiongozi wa taasisi ya utafiti wa nishati ya kamati ya maendeleo na mageuzi ya taifa, Bw. Han Wenke alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema, maendeleo ya sekta ya nishati ya China ni matokeo ya kufungua mlango na juhudi zinazofanywa na China, alisema:-

"Sekta ya nishati ya China imejenga msingi imara, na imefikia kiwango cha juu zaidi cha historia, uwezo wa utoaji nishati nchini China pia umeimarika. Maendeleo hayo yanatokana na jitihada za kutilia mkazo uvumbuzi wa sayansi, teknolojia na kufungua mlango, mbali na jitihada za China za kuhimiza wa maendeleo.

Hivi sasa, China imejenga kimsingi mfumo bora wa utoaji nishati, ambao unatoa uungaji mkono muhimu kwa maendeleo ya uchumi na jamii ya China. Tokea mwaka 1980 hadi mwaka 2006, matumizi ya nishati nchini China yaliongezeka kwa wastani wa 5.6% kwa mwaka, ambayo yaliunga mkono ongezeko la wastani wa 9.8% kwa mwaka la uchumi wa taifa.

Waraka wa serikali unasema, China ikiwa nchi inayoendelea na inayowajibika, inazingatia sana maendeleo ya uwiano kati ya nishati na hifadhi ya mazingira, inachukua hatua kuhimiza uokoaji wa nishati na kupunguza utoaji wa vitu vya uchafuzi kwa mazingira. Matumizi ya makaa ya mawe katika uzalishaji wa bidhaa zenye thamani ya Yuan elfu 10 wa nchini yalishuka hadi tani 1.21 mwaka 2006 kutoka tani 3.39 mwaka 1980, na uokoaji nishati umefikia wastani wa 3.9% kwa mwaka. Ufanisi wa usindikaji, ubadilishaji, uwekaji akiba na usafirishaji wa nishati umeinuka kwa udhahiri ikilinganishwa na mwaka 1980, ambapo pengo lililopo katika matumizi ya nishati katika uzalishaji wa chuma cha pua na saruji, pamoja na uzalishaji wa umeme ikilinganishwa na kiwango cha kisasa duniani pia linaendelea kupungua.

Bw. Han Wenke alisema, tokea mwanzoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita, serikali ya China ilichukulia uokoaji wa nishati kuwa mambo muhimu katika ubunifu wa kila mpango wa maendeleo wa miaka mitano, inaendeleza uzalishaji wenye kuokoa nishati na kuzingatia kuinua ufanisi wa nishati. Mbali na hayo, serikali pia imetunga sera nyingi ili kuimarisha nguvu za uokoaji nishati na upunguzaji wa vitu vya uchafuzi. Alisema,

"Kwanza ni kuimarisha nguvu ya ushawishi wa serikali, serikali inavishawishi viwanda na wateja kuokoa nishati kwa njia ya kujenga mradi wa mfano wa kuigwa. Pili, kuingiza uzoefu wa kisasa wa nchi za nje. Tatu, serikali nayo ilitoa sera za kutoza kodi kubwa na kutotoa uidhinishaji kwa uzalishaji mali unaotumia nishati kwa wingi."

Waraka umeeleza wazi kuwa ili kuhimiza hifadhi ya mazingira, China inazingatia kuboresha muundo wa matumizi ya nishati na kutilia mkazo maendeleo ya nishati endelevu. Waraka unasisitiza kuwa, China siyo tishio kwa usalama wa nishati kwa hivi sasa, katika siku za nyuma wala katika siku za baadaye. Unasema serikali ya China itashirikiana na nchi zote duniani, ili kulinda utulivu na usalama wa nishati, kuleta maendeleo ya kunufaishana na kuhifadhi maskani ya binadamu.