Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-27 15:50:23    
Michezo ya Olimpiki imeingia kwenye maisha ya watu wa China

cri

Mwaka 2007 neno la Olimpiki ni neno ambalo limekuwa likitajwa mara kwa mara na watu wa China. Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008 inapokaribia kufunguliwa, mambo yanayohusu Olimpiki yameingia kwenye maisha ya watu wa China.

Mkazi wa mji wa Beijing, Bibi Cao Zuozheng ni mzee mwenye umri wa miaka 103. Ana afya njema na anapenda michezo. Bibi Cao anafurahia mji anaoishi kuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki. Alisema mbali na kutazama mashindano mbalimbali, ana matumaini kuwa ndoto yake itatimia. Alisema  "Napenda kushika mwenge wa michezo ya Olimpiki kwenye mbio za mwenge, napenda kuchangia maandalizi ya michezo ya Olimpiki."

Ndoto ya Bibi Cao ni kuteuliwa kuwa mmoja wa kushika mwenge wa michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008. Watoto wake wanakubali na kumwunga mkono. Mwanaye Bw. Xiao Shengqiang alisema  "Tunamwunga mkono mama yangu ateuliwe kuwa mmoja kati ya watu watakaoshika mwenge wa michezo ya Olimpiki. Kila tunaposoma habari kuhusu michezo hiyo kwenye magazeti na kutazama vipindi vya televisheni, tunamweelezea mama yangu."

Ili kutimiza ndoto yake ya Olimpiki, Bibi Cao anafanya mazoezi kila siku. Anafanya matembezi huku akinyosha mikono ili kuongeza nguvu ya mikono yake. Bibi huyo alisema kama angeweza kuinua juu mwenge wa michezo ya Olimpiki, angeweza kuwaoneshea marafiki kutoka kila pembe ya dunia sura ya mzee mwenye umri mkubwa wa miaka zaidi ya mia moja anayeishi huko Beijing, pamoja na maisha ya watu wa China.

Kama ilivyo kwa Bibi Cao, watu wengine wa China pia wana matumaini yao kuhusu michezo ya Olimpiki. Dada Liang Chen ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo kikuu kimoja hapa Beijing, yeye ni mmoja kati ya watu wanaojitolea kuhudumia michezo ya Olimpiki. Katika mfululizo wa mashindano yajulikanayo kama "good luck Beijing" yaliyofanyika mwaka 2007 ya kupima maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Beijing, dada huyo alitoa huduma akiwa mtu anayejitolea. Alipozungumzia aliyojifunza kutokana na shughuli za kuhudumia katika mashindano hayo, dada Liang Chen alisema  "Habari ninazofuatilia hivi sasa ni tofauti na zamani. Hivi sasa navutiwa zaidi na habari zinazohusu michezo ya Olimpiki, hususan habari kuhusu watu wanaojitolea. Zaidi ya hayo chuo chetu kikuu kipo karibu na jengo la kamati ya maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Beijing. Wanafunzi wenzangu na mimi tumepiga picha katika jengo hilo, na kuzituma picha hizo kwa wazazi wetu, tunaona fahari kubwa. Pia hivi sasa wanafunzi wenzangu wanapenda kuvaa nguo zenye alama za michezo ya Olimpiki ya Beijing, kwa mfano fulana za rangi ya njano zenye maandishi ya 'good luck Beijing', sisi tunafurahia kuvaa nguo ya namna hii."

Kujitolea kuhudumia michezo ya Olimpiki ni matumaini ya watu wengi wa China. Kwa bahati mbaya dada Zeng Shuya kutoka mkoa wa Taiwan, alishindwa kupata nafasi hii. Alisema  "Nilichelewa kupata habari. Ingawa nilikwenda kujiandikisha mara nilipopata habari, lakini wakati huo nafasi za watu wanaojitolea zilikuwa zimekwisha."

Ni sehemu ndogo tu miongoni mwa watu wa China ambao walibahatika kupata nafasi ya kujitolea kuhudumia katika michezo ya Olimpiki ya Beijing. Hata hivyo wachina wengi wanatoa mchango kwa ajili ya michezo hiyo kadiri kwa wawezavyo.

Katika kituo kimoja cha mtaa wa Dongsi, hapa mjini Beijing, mwalimu mwanamke anawafundisha wanafunzi wake namna ya kujibu maswali ya watalii kutoka nchi za nje kwa kutumia lugha ya Kiingereza. Wastani wa umri wa wanafunzi hao 50 hivi ni miaka 59.

Kutokana na mpango wa serikali ya mji wa Beijing, hadi itakapofunguliwa michezo ya Olimpiki ya Beijing, idadi ya wakazi wa Beijing watakaoweza kuongea Kiingereza itafikia milioni 4 hadi 6, idadi ambayo inachukua asilimia 30 ya wakazi wote wa Beijing. Ili kutimiza lengo hilo, serikali ya mji wa Beijing na shule za lugha za watu binafsi zinashirikiana kupata walimu wanaojitolea.

Dada Cao Fang ni mmoja kati ya walimu wanaojitolea kutoa mafunzo ya lugha ya Kiingereza. Alisema katika madarasa ya mitaa mbalimbali, wanafunzi wengi wana umri mkubwa, hata hivyo wanapenda kujifunza. Mwalimu Cao alisema "Katika hali ya kawaida watu wenye umri mkubwa wakijifunza lugha za kigeni, ni vigumu kwao kupata maendeleo makubwa kama vijana. Lakini wakazi wa Beijing wanaonesha hamu kubwa na jitihada kubwa ya kujifunza, kwani mji wao ni mwenyeji wa michezo ya Olimpiki."

Pamoja na kutimiza matumaini, baadhi ya watu wa China wameweza kupata maisha bora zaidi katika mchakato wa maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Beijing. Mama Zhang Jianshu mwenye umri wa miaka 47 ni mkazi wa Kaifeng, mji ulioko katikati ya China. Baada ya kupunguzwa kazini, mama huyo alianzisha kiwanda kidogo cha kutarizi. Hivi sasa kiwanda hicho kimepata idhini ya kutoa bidhaa kwa ajili ya michezo ya Olimpiki ya Beijing kutokana na umaalumu wa bidhaa zake za kutarizi. Mama Zhang alisema kwa furaha kubwa, "Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 itafanyika mjini Beijing. Mimi nilipunguzwa kazini, lakini niliamua kutoa mchango wangu. Ninafahamu ufundi wa kutarizi wenye umaalumu wa Kaifeng, napenda kuwaonesha walimwengu ufundi huo kwa kupitia jukwaa kubwa la michezo ya Olimpiki ya Beijing."

Mwaka 2007 unaokaribia kumalizika utakumbukwa na wachina wengi. Katika mwaka huu walikuwa wakisubiri kukaribia kwa michezo ya Olimpiki, na kujitahdi kutimiza matarajio yao yanayohusu michezo hiyo.

Idhaa ya kiswahili 2007-12-27