Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-27 19:45:47    
Kwa nini Russia yaonesha nguvu zake za kijeshi?

cri

Kikosi cha ulinzi wa anga cha jeshi la Russia tarehe 25 mwezi Desemba kilitangaza kuwa, kuanzia mwaka 2009jeshi la nchi kavu la Russia litaanza kujizatiti kwa mfumo mpya wa kutungulia ndege wa makombora ya masafa mafupi ya aina ya "Tor-M2".

Katika siku hiyo hiyo, Russia pia ilifanikiwa kurusha satellite 3 za aina ya GLONASS za kuongoza safari za ndege duniani kwa kutumia roketi ya aina ya Proton-M kwenye uwanja wa kurushia satellite wa Baikonour nchini Kazakhstan.

Amirijeshi wa kikosi cha ulinzi wa anga cha jeshi la Russia Jenarali Nikolay Frolov, siku hiyo alisema mfumo wa "Tor-M2" ni bora sana kuliko mfumo wa "Tor-M1" unaotumika hivi sasa. Ikilinganishwa na zana za aina hiyo za nchi za nje, mfumo huo unafaa sana kutumiwa dhidi ya silaha kubwa zinazoongozwa kwa usahihi mkubwa ikiwemo makombora ya Cruise. Alisisitiza kuwa, kazi za majaribio ya mfumo huo zitamalizika kabisa mwaka 2008. Jeshi la Russia litamaliza kazi za kuzatiti rejimenti mbili za kutungulia ndege kutoka ardhini kwa miaka miwili kuanzia mwaka 2009. Baada ya hapo, Russia itazatiti kikosi chote cha ulinzi wa anga kwa mfumo wa "Tor-M2".

Kuhusu mafanikio ya urushaji wa satellite ya mfumo wa kuongoza safari za ndege duniani ya aina ya GLONASS, ofisi ya habari ya idara ya askari wa anga ya juu ilitoa habari ikisema, satellite hizo tatu zitaanza kutumika rasmi mara tu baada ya kufanyiwa marekebisho kwa siku 45, wakati ule mfumo wa GLONASS utafunika 95% ya ardhi ya Russia na 86% ya eneo la dunia. Kabla ya mwaka 2009, mfumo wa GLONASS utamaliza upangaji wa satellite 24, ambapo uongozaji wa safari zote za ndege na uthibitishaji wa mahali zilipo ndege zinazosafiri kwenye anga zitahudumiwa na mfumo huo kwa usahihi, ambao kasoro yake ni ndani ya mita 1.5. Baadhi ya vyombo vya habari vinakadiria kuwa pamoja na kuboreshwa kwa mfululizo kwa mfumo huo wa Russia, Russia itaingia kabisa kwenye soko la kuongoza safari za ndege kwa satellite baada ya muda usio mrefu, na itatoa changamoto kwa mfumo wa GPS wa Marekani.

Wachambuzi wanasema, mafanikio ya urushaji wa satellite 3 za GLONASS na kuzatitiwa kwa mfumo wa "Tor-M2" kwa jeshi la nchi kavu la Russia kuanzia mwaka 2009 ni hatua zinazoonesha nguvu za ulinzi wa Russia. Kuanzia mwaka huu, Russia imekuwa inaonesha nguvu zake mara kwa mara: watafiti wa sayansi wa Russia tarehe 2 mwezi Agosti walichomeka bendera ya Russia iliyotengenezwa kwa Titanium Alloy chini ya bahari ya Arctic, tarehe 12 mwezi Desemba Russia ilisimamisha kwa muda utekelezaji wa "mkataba wa majeshi ya kawaida wa nchi za Ulaya", mwezi Agosti mwaka huu, Russia ilitumia upya manowari kubwa ya kubebea ndege na kurudisha utaratibu wa kufanya doria kwa ndege kubwa za kudondosha mabomu, tarehe 5 mwezi Desemba manowari za Russia zilianza upya safari za mbali za kufanya doria, tarehe 8 mwezi Desemba askari wa makombora wa Russia walifanikiwa kurusha kombora moja ya masafa marefu la aina ya "Topol RS?12M", na tarehe 17 mwezi Desemba nyambizi moja ya jeshi la baharini la Russia ilifanikiwa kurusha kombora moja la masafa marefu ya aina ya RSM?54, mambo yote hayo yaneieleza Marekani kuwa, ikitaka kupuuza kuweko kwa Russia na kubana nafasi za kimkakati za Russia, itakumbana na hatari. Ukweli ni kwamba tokea mwaka huu, Russia inapinga vikali nia ya Marekani ya kubana nafasi za kimkakati za Russia kwa kutumia mbinu za mambo ya kijeshi.

Lakini pia kuna wachambuzi wanaosema kuwa, vitendo vya Russia vya kuonesha nguvu zake za kijeshi mara kwa mara ni kutaka kuweka alama tu wala siyo kutenda vitendo halisi. Huu ni mkakati halisi tofauti na mashindano ya zana za kijeshi, ambayo yalidhoofisha nguvu za Russia katika kipindi cha vita baridi. Ingawa Russia inajitahidi kuimarisha nguvu zake za kijeshi, lakini bado siyo jambo linalowezekana kwa kutaka kufikia na kuzidi kiwango cha sasa cha Marekani. Hivyo licha ya kuchuana na nchi za magharibi, Russia inataka kuleta maendeleo kwa kufanya ushirikiano nazo.