Waziri mkuu wa zamani ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Umma cha Pakistan Bibi Benazir Bhutto tarehe 27 aliuawa katika mji wa Rawalpindi, mji ulio karibu na Islamabad, mji mkuu wa Pakistan. Jumuyia ya kimataifa imelaani vikali kitendo hicho. Wachambuzi wanaona kuwa kuuawa kwake ni pigo kubwa kwa hali inayoelekea kuwa tulivu nchini Pakistan.
Tukio hilo lililotokea baada ya tu Bibi Bhutto kumaliza hotuba yake kwenye mkutano wa hadhara na kutaka kuondoka, alipigwa risasi shingoni na kifuani, kisha muuaji alijilipua kwa bomu alilofunga mwilini. Saa 12 na dakika 16 jioni alifariki dunia katika hospitali kuu ya Rawalpindi akiwa na umri wa miaka 53. Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Pakistan, watu wasiopungua 10 waliuawa katika tukio hilo. Habari iliyotangazwa na vyombo vya habari vya Pakistan kabla ya tukio hilo zilisema kundi la Al-Qaida, wanamgambo wa Taleban na kundi la watu wenye siasa kali walituma watu kumfuatilia Bibi Bhutto.
Jioni ya siku hiyo Rais Pervez Musharraf kwenye televisheni alitangaza serikali ya Pakistan itamfanyia Bibi Bhutto maombolezo ya siku tatu, alilaani sana kitendo hicho cha kigaidi na kutaka wananchi wote wawe watulivu na kuhakikisha amani. Baada ya kutokea kwa tukio hilo mara Rais Musharraf aliitisha mkutano wa viongozi wakuu akiwemo waziri mkuu wa muda Bw. Soomro. Hivi sasa nchi nzima ya Pakistan imekuwa katika hali ya ulinzi mkali.
Jumuyia ya kimataifa imelaani vikali kitendo cha kumwua Bibi Bhutto. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Bw. Qin Gang alisema, China imeshtushwa na kulaani kitendo hicho cha kigaidi, na inatoa mkono wa pole kwa jamaa waliofiwa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon alitoa taarifa akisema lengo la tukio hilo ni kuharibu utulivu na mchakato wa demokrasia nchini Pakistan, na watu waliohusika ni lazima waadhibiwe kisheria. Taarifa imewataka wananchi wa Pakistan wajidhibiti na kuhakikisha utuluvu na umoja. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliamua kufanya mkutano wa dharura katika usiku wa siku hiyo kujadili tukio hilo. Rais George Bush wa Marekani alilaani tukio hilo na kusema hicho ni kitendo cha "woga" cha watu wenye siasa kali kutaka kuharibu demokrasia ya Pakistan na kusisitiza kuwa Marekani inaunga mkono mapambano ya Pakistan dhidi ya ugaidi na watu wenye siasa kali. Naibu waziri wa mambo ya nje wa Russia alisema kuuawa kwa Bi. Bhutto kutasababisha vurugu nchini Pakistan. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia alisema, Russia inatumai kuwa serikali ya Pakistan itachukua hatua ili kuhakikisha utulivu. Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Ulaya alitoa taarifa akisema, tukio hilo ni mashambulizi dhidi ya taifa zima la Pakistan, alitumai kuwa Pakistan itaendelea na juhudi zake za kurudisha mfumo wa demokrasia. Katibu mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu pia alitoa taarifa ikisema hilo ni tukio la kusikitisha na kuhuzunisha.
Wachambuzi wanaona kuwa kuuawa kwa Bibi Bhutto ni pigo kubwa kwa hali inayoelekea kuwa tulivu, hali ya usalama inafuatiliwa sana na watu duniani. Baada ya Bibi Bhutto kuuawa watu wanaounga mkono chama chake cha umma wanakiyooshea kitole Chama cha Muungano wa Waislamu, walikasirika kwa kuchoma moto magari katika miji kadhaa ya kusini ya Pakistan, vitendo kama hivyo visipodhibitiwa hali ya vurugu itatokea kote nchini Pakistan, na kutokana na vitendo vya ugaidi vinavyoongezeka, Rais Musharraf pengine atafikiri kurudisha tena hali ya hatari nchini Pakistan.
Zaidi ya hayo uchaguzi wa bunge jipya ulipangwa kufanyika tarehe 8 Januari, tukio la kuuawa kwa Bibi Bhutto limeuletea wingu jeusi uchaguzi huo. Kabla ya kuuawa kwa Bibi Bhutto suluhisho la kisiasa kati ya Pervez Musharraf na Bibi Bhutto lilikuwa ni msaada mkubwa kwa hali nzuri ya kisiasa nchini Pakistan, lakini sasa kifo cha Bibi Bhutto huenda kitasababisha vyama vya upinzani kuungana na kuupinga uchaguzi huo na kuiingiza Pakistan kwenye hali ya vurugu.
|