Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-31 20:19:07    
Kuangalia ndege kwenye ziwa Qinghai

cri

Ziwa Qinghai la mkoa wa Qinghai, ulioko sehemu ya kaskazini magharibi ya China ni ziwa maarufu linalojulikana duniani. Ziwa hilo ni kama kito kikubwa kilichowekwa kwenye mbuga kubwa isiyo na upeo wa macho. Kisiwa cha ndege kilichoko kwenye ziwa Qinghai, ambacho kila mwaka wanakaa ndege kiasi cha laki moja wanaohamia sehemu ya kusini kutoka kaskazini katika majira ya baridi na kurejea kaskazini kutoka kusini katika majira ya joto, kimekuwa kivutio kikubwa kwenye sehemu hiyo.

Kisiwa cha ndege kilichoko kwenye upande wa kaskazini magharibi wa ziwa Qinghai ni visiwa viwili, ambavyo kimoja kiko kwenye upande wa mashariki na kingine kiko kwenye upande wa magharibi. Watu wanaweza kusikia milio ya ndege wa aina mbalimbali hata wakiwa mbali. Watu wakipanda kwenye mwinuko na kuangalia mandhari, wanaweza kuona kila aina ya ndege wanaorukaruka juu ya maji ya ziwa, wakati baadhi yao wanalala kwa uvivu wakiota jua.

Eneo la ziwa Qinghai ni kiasi cha kilomita za mraba 4,300, ni ziwa kubwa kabisa lenye maji ya chumvi kwenye sehemu ya ndani ya China, na pia ni ardhi muhimu oevu. Mazingira maalumu ya kijiografia na hali ya hewa, yanavutia ndege kiasi cha laki moja kwenda huko kupumzika na kuzaliana kila mwaka. Katika miezi ya Mei na Juni, ndege wanaokaa kwenye visiwa hivyo wanaweza kuzidi aina zaidi ya 30 na kufikia zaidi ya laki moja na elfu 60, kundi lao ni kubwa sana kiasi cha kushangaza. Wenyeji wa huko wanasema, kulikuwa na wakati fulani idadi ya ndege ilipungua kwa kiasi kikubwa, hata ilifikia kiasi cha 200 tu kutokana na baadhi ya watu kwenda huko kuchukua mayai ya ndege. Ili kuhifadhi mazingira ya kimaumbile ya kisiwa cha ndege, mwaka 1975 mkoa wa Qinghai ulianzisha hifadhi kisiwa cha ndege na kuweka wafanyakazi kuwalinda. Kutokana na juhudi zilizofanywa katika miaka mingi iliyopita, raslimali za ndege kwenye kisiwa cha ndege cha ziwa Qinghai zinaongezeka kwa mfululizo, takwimu zilizokusanywa na wachunguzi zinaonesha kuwa, hivi sasa idadi ya ndege wanaopumzika kwenye kisiwa cha ndege ni kiasi cha elfu 50 hivi.

Pamoja na kuongezeka kwa idadi ya ndege wanaopumzika kwenye kisiwa cha ndege cha ziwa la Qinghai, huko kumekuwa sehemu maarufu ya utalii siku hadi siku, na watalii wengi wa nchini na wa nchi za nje wanakwenda huko kwa kufuata majira. Habari zinasema tokea mwaka 2003, idadi ya watalii waliotembelea kisiwa cha ndege cha ziwa Qinghai inadumisha kiasi cha laki moja kila mwaka.

Mtalii kutoka mji wa Xian, ulioko sehemu ya kaskazini magharibi ya China Bw. Li Shehui alisema, safari hii yeye akiambatana na mkewe na binti yao mwenye umri wa miaka 6 walifika kule kwa matembezi, binti yao hakuwahi kuondoka mji wanaokaa, na ni mara ya kwanza kwake kuona idadi kubwa ya ndege na alifurahi sana. Bw. Li alisema,

"Tumefika kwenye kisiwa cha ndege pamoja na mtoto wetu kuangalia ndege. Nilimwambia mtoto watu kuwa ndege kama cormorant wameishi hapa kwa muda mrefu, binadamu wakihifadhi vizuri mazingira ya sehemu hiyo, itakuwa sawa na kuwahifadhi vizuri ndege, wakaweza kuishi hapa pamoja na binadamu."

Kama alivyosema Bw. Li Shehui, ndege na binadamu wana uhusiano mkubwa. Ikiwa sehemu moja muhimu ya uwanda wa juu wa Qinghai na Tibet, ziwa Qinghai ni sehemu dhaifu ya mfumo wa viumbe na ni rahisi kuathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Kuendeleza utalii kwenye sehemu hiyo ni lazima kuzingatia sana suala la uhifadhi wa mazingira. Naibu mkurugenzi wa idara ya utalii ya mkoa wa Qinghai Bw. Xu Hao alisema, wao kamwe hawaruhusu kuharibu mazingira kutokana na kuendeleza utalii, alisema:-

"Tunaona utalii wa kuangalia viumbe unatakiwa kutegemea mazingira bora ya viumbe, na kuendeleza utalii kwa utaratibu wa mwafaka. Ziwa Qinghai ni mandhari nzuri ya kipekee, kamwe hatakubali itoweke au kuharibiwa mikononi mwetu. Kwa upande mwingine, pindi ikiharibiwa, matokeo yake ni ya kutisha, hata maisha ya binadamu yatakabiliwa na shida kubwa, sembuse uendelezaji wa utalii."

Ili kuepusha shughuli za binadamu kuathiri mazingira ya maisha ya ndege kwenye ziwa Qinghai, idara ya usimamizi ya hifadhi ya maumbile ya ziwa la Qinghai imeweka hatua mbalimbali. Kwa mfano, kisiwa cha ndege ni sehemu muhimu zaidi ya hifadhi ya ziwa Qinghai, ingawa kimefunguliwa kwa watalii wanaopenda ndege, lakini shughuli zao zinadhibitiwa kwa kanuni kamili. Watalii baada ya kuingia kwenye kisiwa cha ndege, wanapaswa kukaa ndani ya magari ya betri na kufuata njia iliyowekwa kwa shughuli za utalii. Watalii wanaruhusiwa tu kuangalia ndege kwa kutumia darubini wakiwa mbali kwenye kando ya kushoto ya ziwa. Naibu mkurugenzi wa idara ya usimamizi ya hifadhi ya ziwa Qinghai, Bw. He Yubang alisema,

"Binadamu hawaruhusiwi kuwa karibu sana na ndege, kupatana kati ya binadamu na maumbile siyo kuwa lazima binadamu wasimame katika makundi ya ndege, huku sio kupatana, bali ni kuvuruga mazingira wanayopenda."

Ili kupunguza kadiri iwezekanavyo usumbufu unaoletwa na binadamu kwa ndege walioko katika kipindi cha kuzaliana, kwenye sehemu yenye mayai mengi ya ndege, watalii wanapangwa kuangalia ndege kwa kupitia matundu ya mashimo yaliyochimbwa ardhini. Sehemu ya juu ya mashimo imesetiriwa kwa manyasi, na inaonekana kama ni ya mazingira ya huko, ili kuwafanya ndege wasiwaone binadamu wakati wanapowachunguza.

Ingawa njia hiyo ya kuangalia ndege siyo ya kufurahisha sana watalii, lakini inaungwa mkono na watalii wengi. Bw. Li Shehui kutoka mji wa Xian alisema,

Njia hiyo ni kwa ajili ya kukwepa kadiri iwezekanavyo kusumbua maisha ya ndege ili waishi vizuri na kuzaliana katika mazingira ya asili, naona njia hiyo ni nzuri ambayo inastahili kuenezwa.

Hivi sasa hatua mbalimbali zenye utaratibu za kuwalinda ndege na kuwawezesha binadamu na ndege waishi katika hali ya mapatano zinatekelezwa kwenye Ziwa Qinghai, na kisiwa cha ndege kimekuwa maskani ya pamoja ya ndege na binadamu