Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-31 20:44:41    
Mwai Kibaki achaguliwa kuwa rais wa Kenya katika kipindi kijacho

cri

Tume ya uchaguzi ya Kenya tarehe 30 mwezi Desemba ilitangaza, rais wa sasa wa Kenya Bw Mwai Kibaki ameshinda katika upigaji kura wa uchaguzi wa urais uliofanyika tarehe 27 mwezi Desemba. Kisha Bw. Kibaki aliapishwa kuwa rais wa kipindi kijacho.

Tarehe 27 mwezi Desemba, Kenya ilifanya kwa mara ya nne uchaguzi mkuu tangu nchi hiyo irejeshe utaratibu wa vyama vingi vya kisiasa mwaka 1992, katika uchaguzi huo, walipatikana rais wa nchi, wabunge wa taifa 210 na madiwani zaidi ya 2,000 wa mikoa na miji. Kutokana na kuchelewa kutangazwa matokeo ya upigaji kura, hali ya wasiwasi ilijaa nchini Kenya, na vurugu zilitokea katika baadhi ya miji ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu wa Nairobi. Chama cha PNU kinachoongozwa na Mwai Kibaki kinashutumu chama cha ODM cha upinzani kuchochea waungaji mkono wake kufanya vurugu, kikijaribu kukataa matokeo ya upigaji kura. Kiongozi wa chama cha ODM Bw. Raila Odinga analaumu chama cha PNU kufanya udanganyifu wakati wa kuhesabu kura, akitaka kura zilizopigwa zehesabiwe upya. Tume ya uchaguzi ya Kenya imekataa ombi la kuhesabu upya kura zilizopigwa, na ilitangaza ushindi wa Kibaki alasiri ya tarehe 30.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Kenya Bw. Samuel Kivuitu alasiri ya tarehe 30 alitangaza matokeo ya hesabu ya kura kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ya kimataifa wa Kenyatta, lakini mkutano ulisitishwa kutokana na vurugu iliyotokea kwenye mkutano huo, na Bw. Kivuitu aliondoka kwenye ukumbi huo chini ya ulinzi wa askari polisi. Hapo baadaye Bw. Kivuitu alionekana kwenye matangazo ya televisheni ya taifa na kutangaza idadi za kura walizopata wagombea 9 wa urais. Alisema Kibaki alipata kura zaidi ya milioni 4.58, kiasi hicho kinazidi kwa kura zaidi ya laki 2.3 kuliko alichopata Bw Raila Odinga, ambaye alichukua nafasi ya pili katika uchaguzi, hivyo Kibaki atakuwa rais katika kipindi kijacho. Bw. Kivuitu alitoa wito wa kutaka watu wa nchi hiyo wakubali matokeo hayo ya uchaguzi na kuepusha matukio ya kimabavu.

Baada ya kutangazwa habari hiyo, chama cha ODM, ambacho ni chama muhimu cha upinzani, kilifanya maandamano mjini Nairobi, baadhi ya watu waliwasha moto kuteketeza nyumba na kunyang'anya vitu vya madukani. Habari zinasema, hadi hivi sasa watu 15 wamepoteza maisha yao katika matukio ya kimabavu.

Haukufikia muda wa saa moja tangu kutangazwa matokeo ya upigaji kura, Kibaki aliapishwa kwa haraka kuchukua madaraka ya urais mjini Nairobi. Katika sherehe ya kuapishwa kwake, Bw Kibaki alisema kulikuwa na ushindani mkali kwenye uchaguzi huo, sasa matokeo ya uchaguzi yametangazwa, sasa ni wakati wa wananchi kutupilia mbali migongano yao ili kujitahidi kwa pamoja kujenga nchi yenye nguvu na umoja. Bw Kibaki aliahidi kuwa atajitahidi kujenga serikali isiyo na ufisadi katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Alisema serikali mpya licha ya kuundwa na wanachama wa chama anachokiongoza cha PNU, pia itaundwa na wanachama wa vyama vingine vya kirafiki.

Rais Kibaki alipata mafanikio makubwa katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuhimiza maendeleo ya uchumi katika kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano iliyopita. Kipindi hicho kimekuwa kipindi cha mabadiliko ya maendeleo ya uchumi wa Kenya, katika kipindi hicho, uchumi wa Kenya ulikuwa na wastani wa ongezeko la 5% kwa mwaka. Licha ya hayo, alitekeleza utaratibu wa elimu ya lazima ya shule ya msingi nchini kote, pia alipata mafanikio dhahiri katika kupambana na ugonjwa wa ukimwi na maradhi ya aina nyingine. Lakini serikali ya Kibaki haikuwaridhisha watu katika kurekebisha katiba ya nchi, kupambana na ufisadi, kupunguza umaskini na kuboresha hali ya usalama. Hali hiyo ilimfanya Bw Kibaki kushindwa na Odinga katika kura za maoni ya umma uliofanywa mara kadhaa kabla ya uchaguzi mkuu, na kufanya uchaguzi mkuu huo kuwa na ushindani mkubwa zaidi katika miaka ya karibuni. Masuala hayo yatakuwa masuala yanayopaswa kutatuliwa katika kipindi chake cha pili cha miaka mitano cha urais wa nchi.